Na Abdi Suleiman, Pemba
MICHUANO ya kuwania Kombe la Pemba (Pemba Cup), imeanza kutimua vumbi nje ya uwanja wa michezo Gombani Chake Chake.
Mashindano hayo yanashirikisha timu saba za mchezo wa mpira wa netiboli zinazowania ubingwa huo.
Katika ufunguzi wake, timu ya Chake Boys ilitoana jasho na Wete Boys mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Meja Mstaafu Juma Kassim Tindwa, aliyekuwa mgeni rasmi.
Wakicheza kwa kujiamini, vijana wa Chake Boys waliweza kuwatungua majirani zao wa Kaskazini, Wete kwa magoli 16-14 huku mchezaji wake Mfamau Lali aking’ara katika nafasi ya ushambuliaji (GA), na kupachika mabao kumi peke yake.
Nao mabanati wa Chake Girls, wakafuata nyayo za kaka zao kwa kuwarusha roho warembo wa Wete Girls baada ya kuwachapa mabao 23-13, huku Asha Khamis (GA) akitamba katika kutundika magoli kwa kupachika 19 peke yake.
Hata hivyo, mchezo kati ya Chake Boys na Wete Boys ulitawaliwa na ungomvi katika dakika za mwisho kutokana na wachezaji wa timu hizo kudai kuwa waamuzi hawakuwa wakichezesha kwa haki.
No comments:
Post a Comment