Na Juma Mohammed, MAELEZO
SERIKALI ya Jamhuri ya watu wa China, imekabidhi mradi wa matengenezo ya masafa mafupi ya kituo cha Redio cha Dole kwa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).
Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Dk. Ali Mwinyikai alisema mradi huo ulioanza mwaka 2011 umekamilika baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa katika kituo cha kurushia matangazo ya masafa mafupi kilichopo Dole wilaya ya Magharibi. Unguja
“Mradi huu ulianza mwezi Septemba mwaka jana, kampuni ya China Shaanxi ndiyo iliyofanya ukarabati wa kituo hichi ambacho sasa kimerejea katika hali ya kawaida kuongeza usikivu wa masafa mafupi kwa ajili ya ZBC Radio”, alisema Dk. Mwinyikai.
Katibu huyo alisema baada ya ukarabati huo, kituo cha Dole kitaweza kutoa mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi wa matangazo ya ZBC.
Mwakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Ghang Ghiring alisema China itawajibika katika kipindi cha mwaka mmoja kuufanyia matengenezo madogo madogo baada ya makubaliano ya pande zote mbili kuamua kukabidhi mradi huo kwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya kukamilika.
Makabidhiano ya mradi huo yamefanyika jana Ofisini kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo, Kikwajuni mjini Zanzibar.
Wakati huo huo, serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Jamhuri ya China jana zimetiliana saini mkataba wa mradi wa ukarabati wa kituo cha kurushia matangazo cha Shirika la Utangazaji Zanzibar kilichopo Langoni Zanzibar.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Mwinyikai alisema, mkataba huo ni nyongeza ya mkataba wa awali uliotiwa saini mwaka 2009 kuhusu ukarabati wa kituo hicho ambao utagharimu kiasi cha RMB 784,800.
Katika hafla ya utiaji saini nyongeza ya mkataba wa awali, Jamhuri ya Watu wa China iliwakilishwa na ofisa Ubalozi katika Ubalozi mdogo Zanzibar anayeshughulikia Uchumi na Biashara, Liu Xiao Hang.
China imekuwa mshirika mkubwa katika maendeleo ya sekta mbali mbali ikiwemo ya habari Zanzibar, ambapo kwa miaka mingi imekuwa ikisaidia maendeleo ya sekta hiyo.
No comments:
Post a Comment