Na Mwashamba Juma
WANANCHI wametakiwa kushawishika kutumia zaidi vyombo vya sheria ikiwemo mahakama katika kutatuliwa matatizo yao badala ya kulalamikia jamii zao au kujichukulia hatua mikononi, ili kupatiwa ufumbuzi wa kisheria katika utekelezwaji wa haki zao.
Akitoa nasaha hizo huko katika ukumbi wa Bwawani hoteli, Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Abraham Mwampashe wakati akizindua ripoti ya Haki za Binaadam ya mwaka 2011 iliyotayarishwa na kutolewa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC).
Alisema utafiti uliofanywa na taasisi za kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) na kituo cha Sheria na Haki za Binaadam (LHRC) cha Tanzania bara katika kutoa ripoti hiyo, zitalenga kuamsha jamii hasa taasisi zinazohusika moja kwa moja katika ukiukwaji wa Haki za Binaadam, watashituka, na waathirika kwa upande wao watachukua hatua.
Aidha alisema katika utekelezaji wa Haki za Binaadam baadhi ya sheria zinahitaji kuangaliwa upya na kufanyiwa marekebisho ili kuendana sambamba na Haki za Binaadam.
Akizitaja baadhi ya sheria hizo Jaji Abraham alisema, Sheria namba 6 ya mwaka 2004, pamoja na sheria ya kanuni za adhabu na mwenendo wa makosa ya jinai Zanzibar, sheria namba 7 ya mwaka 2004 sura ya tano.
Alisema Haki za Binaadamu zinaanza mara baada ya mtoto anapozaliwa, hivyo ni wajibu wa wazazi kuzitambua, kuzilinda pamoja na kuzitekeleza, sambamba na kuwatekelezea watoto wao haki za msingi kwa kuwapatia elimu, afya na upendo.
Jaji Mwampashe alisema kutochukuliwa hatua kwa kesi za udhalilishaji ni matokeo ya udhaifu wa nchi husika kwa kulindana na kuoneana aibu kwa wahalifu ambapo hupelekea ukiukwaji na uvunjwaji wa Haki za Binaadam.
Akiwasilisha ripoti hiyo mara baada ya kuzinduliwa, Kaimu Mkururugenzi wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), Mwanaharusi Miraji Mpatani, alisema changamoto mbalimbali zilizomo katika huduma za jamii ni matokeo ya ukiukwaji wa Haki za Binaadamu.
Alisema kuendelea kutumika kwa mitondoo katika vyuo vya mafunzo ni ukiukwaji wa Haki za Binaadam, hivyo alizitaka mamlaka husika kuichukulia kama ni changamoto katika utekelezaji mzima wa Haki za Binaadam.
Akizungumzia masuala ya ajali za barabani katika ripoti hiyo, Mwanaharusi alisema kwa mwaka 2011 ripoti ilibaini jumla ya watu 45 walikufa kwa ajali za barabarani na wengine 44 kupata ulemavu jambo ambalo ilimekiuka haki za msingi za Binaadamu hasa katika haki ya kuishi.
Nae Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar George Kazi, alisema kuwa wananchi hawana mwamko wa kwenda Mahakamani katika kufikisha matatizo yao kisheria.
Akijibu masuali ya mahakama kwa niaba ya Jaji wa mahakama kuu Zanzibar, kufuatia suali lililoulizwa na washiriki la kucheleweshwa na kufutwa kwa kesi za ubakaji na kupewa ujauzito kwa Wanafunzi.
Mrajis huyo alisema ucheleweshwaji na kufutwa wa kesi za kupewa ujauzito kwa wanafuzi ni kunatokana na mahakama kutokuwa na vifaa vya kitaalam na vya kisasa vya kutolea vielelezo, hasa katika masuala ya vipimo kama DNA.
Aidha Kazi alisema kuoneana muhali na aibu kwa watuhumiwa na washitaki kunapelekea kufukwa kwa kesi nyingi za ubakaji na za kupewa ujauzi kwa wanafunzi hasa waathirika waliokuwa na ujirani mwema, kwa kuziomba wenyewe mahakama kufutwa kwa kesi hizo
Wakichangia mada mbalimbali katika uwasilishaji wa ripoti hiyo, washiriki katika hafla hiyo walisema kauli chafu kwa wahudumu wa hospitali hususani wauguzi zinatokana na mazingira mabaya ya kazi katika sehemu hizo.
Ahmada Hassan Juma mmoja wa wachangiaji hao alisema uchache wa vitendea kazi, uhaba wa wahudumu wa kitengo cha uzazi pamoja na mishahara midogo kwa wafanyakazi hao, vinapelekea kufanya kazi katika mazingira magumu jambo ambalo linawasababishia jazba.
Nae Ahmed Ali Omar, mwakilishi kutoka kwa watu wenye ulemavu alisema kuwa ripoti hiyo haikuweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu wa kuona.
Katika kuangalia masuala ya Haki za Binaadam watu wa jamii hiyo hawakutendewa haki kwa kutofikishiwa ripoti hiyo.Hivyo aliwataka ZLSC kuwaandalia CD kwa kuwafikishia ili nao wawe sehemu ya jamii.
Wakichangia maada ya haki ya kumiliki mali mmoja wa wachangiaji hao kutoka Jumuiya ya Wanasheria wanawake Zanzibar ZAFELA Amina Talib Ali, alisema suala la ugawaji wa mali kwa mwanamke alie achika katika ndoa, bado ni changamoto kwa wanawake walio wengi, jambo linalopelekea kukiukwa kwa Haki za Binaadam.
Akifunga mkutano huo, Mwenyekiti wa ZLSC, Profesa Chris Maina Peter, alielezwa kuvutiwa kwake na michango iliyotolewa na washiriki ambayo ilikuwa na nia ya kujenga mustakbala mzuri kwa masuala ya haki za binadamu nchini.
No comments:
Post a Comment