Na Salum Vuai, MAELEZO
HOTELI ya Chumbe Coral Park iliyoko kisiwa cha Chumbe, imesifiwa kwa kuwa mfano mzuri wa utalii unaozingatia uhifadhi wa mazingira.
Sifa hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk. Omar Ali Amir, juzi katika maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani yaliyoandaliwa maalumu na uongozi wa hoteli hiyo, uliokwenda sambamba na kukaribisha msimu mkubwa wa utalii.
Dk. Ali alisema, hatua ya hoteli hiyo kujiendesha kwa utaratibu wa kutumia rasilimali asilia kwa ajili ya kutunza na kuhifadhi mazingira, inafaa kuigwa na hoteli nyengine nchini kwa lengo la kuinusuru Zanzibar na janga la kimazingira.
"Nimevutiwa na mfumo huu wa kutumia vitu vya asili katika kila nyanja kuanzia ujenzi wa hoteli, vifaa vya kupikia, vyoo vinavyolenga kutengeneza mbolea, kuvuna maji ya mvua kwa matumizi yenu, umeme wa nguvu za jua na mengine, na mmeonesha kwa vitendo dhamira ya kuyalinda mazingira ya nchi yetu", alifahamisha.
Alieleza kuwa, wapo watalii wengi wanaopenda kuona utalii wa kimazingira (Eco-tourism), ili kufurahia maumbile mbalimbali na uoto asili, hivyo ni vyema rasilimali hizo zilindwe na kuendelezwa ili kuvipa viumbe hai mfano wa ndege, nyoka na vyengine, kuishi na kuliingizia taifa fedha zinazosaidia kuinua uchumi.
Dk. Ali ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyojumuisha maofisa wa Idara ya Mazingira na wanafunzi wa skuli kadhaa, alisema siku ya Mazingira Duniani, isiishie kwa kukutana na kuzungumzia mazingira pekee, bali iambatane na vitendo vinavyolenga kuiepusha Zanzibar na athari za mabadiliko ya tabianchi.
"Hatuwezi kuepuka kuvuna maliasili ambazo zinahitajika kwa maendeleo na maisha yetu, lakini wakati tukifanya hivyo, tutumie njia bora na salama kwa kuvuna cha kutosha leo, na kubakisha cha kesho, keshokutwa na mtondogoo", alishauri.
Aliiasa jamii kuhakikisha kazi zao za kujiendeleza kimaisha haziharibu vianzio vya maji, mazalio ya samaki baharini, wala kufyeka ovyo misitu na kukata miti bila kupanda mipya, hali inayochangia uhaba wa mvua.
Mapema, Naibu Katibu Mkuu katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dk. Islam Seif Salum, alisema matatizo ya kimazingira yanapojitokeza, huwa hayana mipaka, kwani athari zake humgusa kila mtu.
Kwa hivyo, alishauri jamii ione umuhimu wa kutumia rasilimali za asili zinazoizunguka, kama ambavyo hoteli ya Chumbe Coral Park inavyofanya, katika suala zima la kutunza na kuhifadhi mazingira.
Naye Ofisa Uhifadhi na Elimu ya Mazingira wa hoteli hiyo Safia Masuka, aliwakumbusha wananchi kujenga utamaduni wa kuhifadhi taka sehemu maalumu kwa matumizi mengine, badala ya kuzitupa ovyo na kusababisha madhara hasa kwa watoto wanaopenda kucheza majaani.
Katika hafla hiyo, wanafunzi wa skuli za Kajificheni, Hamamni, Junior Academy na Chuo cha Afya Mbweni, walionesha sanaa mbalimbali zinazotengenezwa kwa kutumia takataka, pamoja na kutumbuiza kwa nyimbo zinazohamasisha utunzaji wa mazingira.
Aidha, wawakilishi wa kikundi cha 'Tusife Moyo' kutoka Kidoti, walionesha vitu mbalimbali vitokanavyo na rasilimali asili, zikiwemo sabuni za mchaichai, mwani, karafuu, mdalasini na nyengine.
No comments:
Post a Comment