Na Khamis Mohammed
WAZIRI wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui, amesema, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejidhatiti kuhakikisha sekta ya viwanda inaendelea kutoa mchango kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii Zanzibar.
Hayo aliyaeleza wakati wa ziara ya kutembelea viwanda na vikundi vya uzalishaji katika Mkoa wa Mjini Magharibi jana.
Waziri huyo alisema, kufikia azma hiyo, serikali pia imeandaa mazingira mazuri ya uwekezeji katika sekta ya viwanda na kuondosha vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya viwanda Zanzibar.
Aidha, alisema, itaendelea kushirikisha na wawekezaji katika sekta ya viwanda sambamba na wawekezaji sekta ya binafsi kuendeleza sekta ya viwanda nchini.
“Malengo ya serikali ni kuhakikisha wawekezaji wa ndani na nje wanawekeza katika sekta ya viwanda hasa vinavyotumia malighafi inayopatikana hapa nchini na kutoa ajira kwa wingi".
Waziri Mazrui aliwashauri wawekezaji sekta binafsi kuangalia utafutaji wa masoko ya nje ambayo yatasaidia kujitangaza na kuwawezesha kuendelea na uzalishaji wa bidhaa kwa uhakika zaidi.
Wakizungumza katika ziara hiyo, baadhi ya wawekezaji waliitaka serikali kuitupia jicho sekta binafsi katika kukabiliana na changamoto inayokabiliana nayo kwenye ushindani wa kibiashara.
Mzee Mwinyi Hassan, mmiliki wa kiwanda cha uchongaji cha Mhana Contract, alisema, ipo haja kwa serikali kutoa kipaumbele fulani kwa wawekezaji wazalendo ili waweze kuchangia zaidi maendeleo ya sekta hiyo kama ilivyo kwa baadhi ya nchi.
"Sekta binafsi itakapopewa msukumo na serikali hata uchangiaji wa kodi pia utakuwa kwa kiwango kikubwa na kusaidia maendeleo ya kiuchumi", alisema mmiliki huyo.
Hassan, alieleza changamoto wanazokabiliana nazo hivi sasa ni pamoja na kuagiza malighafi ya mbao kutoka Msumbiji na hivyo kupelekea kuongezeka gharama za bidhaa wanazozizalisha. Kiwanda hicho kimeajiri zaidi ya vijana 80.
Naye Mkurugenzi Muendeshaji wa Zanzibar Botlers, Abdallah Salim Turky, alisema, changamoto ya kutokuwepo kwa umeme wa uhakika ni moja ya vikwazo wanavyokabiliana katika sekta ya viwanda hivi sasa.
Aidha aliiomba serikali kusaidia unafuu wa uletaji wa malighafi za viwanda ili kuiwezesha sekta hiyo kuzalisha bidhaa zitakazokuwa na unafuu kwa watumiaji na kuviwezesha viwanda kufanya kazi kwa ufanisi.
Leteni maendeleo tumechoka ngojera!!
ReplyDeleteZ'bar huwezi kuweka kiwanda kikubwa kwa soko la watu 1200,000. labda viwanda vya maji ya chupa, juisi, mikate nk.
Mimi nachallenge kama ingekua inawezekana kuwekeza viwanda vikubwa Mazrui kwa umaarufu wake angekwisha ingia ubia na matajiri wa nje wakaanzisha japo kimoja, mbona hoteli anayo?
Uwekezaji pekee Z'bar wenye manuufaa ni kwenye uvuvi na utalii lakn si viwanda wala kilimo manake hapa hapana malighafi wala maeneo ya kilimo wanasiasa msitudanganyeeee!!
Shughuli pekee hapa mtu anayoweza kuifanya ni kufungua duka la nguo na viatu umejitahidi sana kama ana mtaji kuleta VITU USED ie magari, mafriji tv. nk. na wateja wengi ni wabongo ambao UWAMSHO wanawafukuza.
Hapa hata ukisema ufungue kiwanda cha kuchonga mbao mpaka zitoke bara au msumbiji, wahadimu wameshindwa kutunza mazingira mpaka simba uranga wa kuezekea na mkaa unatoka bara.
Ukiacha kuajiriwa na SMZ, ukatembeze wazungu na sku hizi watembeza watalii wamekua wengi kuliko watalii wenyewe.
Ualimu nako kushajaa! Mtaji pekee uliobaki ni SMZ kumchagua Bakhressa( Mzazibari mjanja)kuwa mshauri wa uchumi kwa vile yeye amethubutu kuwekeza hadi nje ya nchi anaweza kutusaidia maarifa.
Wanasiasa mnapozungumza mambo muwe makini msidhani kila mzanzibari ni MUWAMSHO, wengine tunaona mbali! (our scop of thinking goes beyond tomorrow)!