Habari za Punde

Dk. Karume: CCM Inahitaji Viongozi Makini

Na Haji Nassor, PEMBA
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume amewataka wanachama wa chama hicho, kuchagua viongozi imara na wenye ujasiri ambao wataweza kukiendeleza chama hicho kukaa madarakani.

Makamu Mwenyekiti huyo, alieleza hayo huko Shidi jimbo la Mkanyageni Mkoani Pemba, alipokuwa akizungumza na wanaCCM wa jimbo hilo, mara baada ya ufunguzi wa tawi la CCM la Shidi, kwenye ziara yale ya siku moja kisiwani humo.

Alisema CCM inahitaji viongozi makini katika kila ngazi ambao wataweza kusimama na kukitetea chama kupitia ilani yake, hivyo endapo watachagua viongozi wepesi, chama kinaweza kukosa ushujaa mbele ya vyama vyengine.

Alisema kutokana na kukamilika uchaguzi katika ngazi ya ngazi ya shina na matawi, wajitayarishe katika ngazi za wadi, jimbo, wilaya, Mkoa na kisha Taifa (NEC), huku akisisitiza kuwa hakutakiwa mzaha katika kuwachagua viongozi hao.

Alifafanua kuwa viongozi na wanachama waondoshe migawanyiko mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi, kwani jambo hilo sio jema, na linaweza kudhoofisha chama hatimaye kukosa mwelekeo madhubuti kwenye mapambano ya kisiasa dhidi ya vyama vyengine.

“Makundi ndani ya CCM yana mwisho, na ni baada ya kumalizika kwa uchaguzi, hapo makundi yote yanatakiwa yavunjike na wanachama waungane pamoja, ili nguvu ya chama izidi kuimarika’’,alifafanua Dk. Karume.

Katika hatua nyengine Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, na Rais Mstaafu wa Zanzibar aliwapongeza wanaCCM kwa kuendelea na umoja na mshikamano ambao umepelekea chama kuimarika kwani misuguano ndio adui wa chama.

Hata hivyo aliipongeza hatua wa wanaCCM hao kujenga tawi la kisasa na la kudumu na kuwataka walitumie vyema ili, liwe chanzo cha kuvuna wanachama wapya.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, aliwapongeza wanaCCM hao kwa kukamilisha vyema uchaguzi wa ngazi za shina na matawi kwa kuchagua viongozi imara na shupavu.

Aidha Vuai aliongeza kuwa, bado CCM Pemba ni imara kutokana na kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwao, ambapo hilo kwa vyama vyengine sio kazi rahisi.

Nae Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba Shija Othuman Shija, alisema CCM daima itaendelea kushikamana ikiwa ni hatua moja wapo ya kushika dola kila baada ya miaka mitano.

Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar pia alitembelea barabara za Mizingiani- Wamba, Mgagadu - Kiwani, na barabara ya Kenya -Chambani pamoja na matawi ya CCM ya Kiwani na Chambani Kwa mtoro.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.