Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kufaidika kwa ‘Utalii kwa Wote’

Na Bakari Mussa, PEMBA
WAZIRI wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk amesema serikali imeamua kuja na sera ya utalii kwa wote, ikitegemea kuwa sekta hiyo itawanufaisha zaidi wananchi katika kuinua maisha yao.

Waziri huyo alieleza hayo katika hoteli ya Manta Resort, iliyopo Pango la Watoro Makangale, alipokuwa akifunga warsha iliyozungumzia dhana ya utalii kwa wote.

Alisema dhana ya utalii kwa kwa wote ina lengo la kuufanya utalii uweze kuwanufaisha zaidi kimaslahi wananchi sambamba na kuwa na utalii utakaozingatia mila, silka na utamaduni wa Kizanzibari.

Waziri Mbarouk alisema faida ya dhana nzima ya utalii kwa wote, haitaweza kufikiwa endapo taaluma haitopewa umuhimu na kusisitiza kuwa wananchi waelimishwe vya kutosha ili utalii uweze kuleta manufaa kwa wananchi wa Zanzibar.

Aidha alisema kuwa ili sekta ya utalii iweze kuendelea na kuleta faida kwa wananchi mashirikiano yanahitajika baina ya taasisi za serikali, wawekezaji na jumuiya zenye kujishughulisha za kazi nzima ya utalii visiwani hapa.

“Tushirikiane kuifanyia kazi hii kwa pamoja tufikie tunapokusudia, naelewa sio kazi rahisi ni ngumu inahitaji mashauriano, nyenzo na muda, lakini kwa vyovyote vile ili tufikie huko lazima tushirikiane na tufanye tathmini wapi tumekosea ili kupata nafasi ya kujirekebisha”, alieleza, waziri huyo.

Waziri huyo pia alihimiza suala la vijana kupewa taaluma zaidi kuhusiana na utalii kwani sekta hiyo ndiyo tegemeo la kupunguza tatizo la ajira liliopo hivi sasa.

Waziri Mbarouk alifahamisha kuwa wizara itaunda kamati ndogo kwa Pemba ya utalii kwa wote ambayo itaweza kushauri na kuisaidia serikali juu na namna gani suala sekta hiyo itaweza kuwa na tija kwa wananchi.

Alisema anakusudia kuanzisha wiki ya utalii kwa wote, kila mwaka ambayo itafanyika kila wiki ya mwanzo ya Juni ambapo itatoa nafasi kwa wananchi kuutambua utalii kama ni sehemu yenye mchango katika maisha yao.

Waziri huyo alifurahishwa na namna ya hoteli ya Manta Resort ambapo muwekezaji wa hoteli hiyo amekuwa akiwasaidia wanayakazi kumudu mambo mbali mbali ikiwemo nyumba pamoja na kudumisha mila na desturi za Kizanzibari.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.