Habari za Punde

Walimu 111 wa Sayansi Kuajiriwa

Na Hafsa Golo
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali, inatarajia kuajiri walimu wapya 111 katika mwaka 2012/2013 watakaosomesha skuli za Unguja na Pemba ili kupunguza tatizo la walimu lililopo nchini.

Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utumishi wa wizara hiyo, Vuai Ali Khamis alieleza hayo alipokuwa akizungumza na vijana wanaotarajiwa kuajiriwa katika skuli ya sekondari ya Hailesellassie.

Mkurugenzi huyo alifahamisha uajiri wa walimu hao umezingatia upungufu uliopo ambapo wengi wao watakuwa walimu wa kufundisha masomo ya sayansi.

Akitaja masomo hayo alisema kuwa ni masomo ya sayansi na hesabu na kwa upande wa masomo ya sanaa tatizo kuu ni walimu wa Geographia, Historia, pamoja na lunga ya kiengereza.

"Tutaajiri kwa awamu na walimu tutowapa vipao mbele ni walimu wa masomo ya sayansi kwani ndio tatizo lililodumu kwa muda mrefu sana na serikali imejipanga kutatua tatizo hilo",alisema.

Kwa upande wa waziri wa wizara hiyo Ali Juma Shamuhuna alisema kuwa serikali ina matumaini makubwa kutoka kwa walimu wapya wanaotarajia kuajiriwa hivi karibuni.

Shamuhuna alisema kuwa nafasi waliyoipata ina umuhimu kwao hivyo wanawajibika kufanya kazi kwa bidii na uadilifu wa kufuata miongozo ya sera ya elimu pamoja na mitaala ya elimu ili kuleta ufanisi katika utendaji wa kazi hiyo.

"Fanyeni kazi kwa uadilifu na ari zaidi na mkizingatia kufuata kanuni na taratibu na mhakikishe silabasi mnazifuata na zinakamilika kwa wakati”, alisema Shamuhuna.

Aliwataka walimu hao kuhakikisha wanakuballi kufundisha katika skuli walizopangiwa vinginevyo ajira zao zitakuwa mashakani kwani lengo la serikali ni kutatua matatizo yanayowakabili wanafunzi hususan katika skuli za vijijini na Pemba.

Aidha alisema si busara kwa walimu hao kujiingiza katika shughuli za kisiasa lakini wanapaswa kuisaidia jamii na kuzingatia watoto masikini ambao wanahitaji msada wa mchango wao ili wapige hatua kubwa kielimu vile vile taifa liwe na wasomi wazuri na wataalam wa fani mbali mbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.