Na Kunze Mswanyama, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe ameendelea kugundua madudu katika shirika la ndege la Tanzania (ATCL), ambapo katika ziara aliyoifanya jana kwenye ofisi za shirika hilo yameibuka mapungungu kadhaa.
Katika zaiara hiyo jana iliyolenga kuzungumza na wafanyakazi wa shirika hilo, Dk. Mwakyembe alibaini kuwepo kwa mikataba mibovu sambamba na ajira zilizokiuka utaratibu.
Akizungumza na wafanyakazi hao, Dk. Mwakyembe alisema wakati wa watumishi wababaishaji kuondoka katika shirika hilo umefika na hakuna wa kuliliwa.
Mwanzoni mwa wiki hii, waziri huyo alitengua nafasi ya Kaimu Mkurugenzi iliyokuwa ikishikiliwa na Paul Chizi toka 2010.
Alisema kama wapo wafanyakazi ambao hawakuridhika na maamuzi na kama wapo wenye kuona kuwa haki haikutendeka waende mahakamani.
Alifahamisha kuwa mahakama ndicho chombo chenye kuweza kutoa haki, lakini hatarudi nyuma katika kutetea mali za umma zinazotafunwa na wajanja wachache.
Waziri Mwakyembe alisema serikali imechoka kulibeba shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na kulipa muda wa miezi mitatu liwe limeshatoa taswira ya kujiendesha wenyewe bila ya kutegemea fedha kutoka serikalini.
Alisema wanaolalamika katika vyombo vya habari juu ya kutofuatwa kwa utaratibu wa kumuondosha Chizi hawajui kwani tayari Kaimu huyo Mkurugenzi alikwishastaafu tangu mwaka 2002, lakini alirejeshwa kinyemela kazini 2010 bila ya nafasi hiyo kutangazwa.
Alifahamisha kuwa wapo watu wameingiza suala hilo na ukabila na kwamba hakuna mtu wa kabila lake aliyempa nafasi.
Akizungumzia ufisadi uliopoteza mamilioni ya fedha alisema mwaka jana Wakurugenzi wawili wa ATCL walikwenda China kusimamia ushonwaji wa sare za wahudumu 17 wa ndege ambapo walikaa nchini humo siku 49 na kutumia kiasi cha shilingi milioni 77.5
Alibainisha kuwa tayari serikali imepata shilingi bilioni 4.5 za kulipia matengezo ya ndege nyingine aina ya 5H-MWF ambayo inafanyiwa ukarabati kwenye karakana ya shirika hilo jijini Dar es salaam.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Kapt. Lazaro, akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa shirika hilo alimshukuru waziri kwa kutoficha maovu na kuahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuliokoa shirika hilo na kuliondoa kwenye utegemezi.
Hiyo ndio Tanganyika
ReplyDeleteNatamani sana na sisi tuwe na viongozi wanaojiamini kama hao.
ReplyDeleteWawatimue viongozi na wafanyakazi wazembe ktk wizara, idara na mashirika yetu mbali mbali.