Habari za Punde

Dk. Shein atuma rambi rambi Saud Arabia



Na Rajab Mkasaba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za rambi rambi Mfalme Abdullah bin Abdulaziz Al-Saud wa Saud Arabia,  kufuatia  kifo cha Prince Nayef bin Abdulaziz al-Saud aliyetarajiwa kurithi kiti cha Mfalme na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saud Arabia.

Katika salamu hizo za rambi rambi Dk. Shein alisema kuwa yeye mwenye binafsi wananchi wa Zanzibar wamepata mshtuko na huzuni kubwa baada ya kupata taarifa ya kifo cha Prince Nayef bin Abdulaziz al-Saud.


Kwa upande wake Dk. Shein pamoja na wananchi wa Zanzibar wanatuma salamu za pole na rambi rambi kwa wananchi wa Saud Arabia kufuatia kifo cha kiongozi huyo.

Aidha, salamu hizo za rambirambi ziliwapa pole familia, marafiki, ndugu na jamaa pamoja na wananachi wote wa Saud Arabia na kueleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanaungana na ndugu zao hao wa Saudi Arabia katika msiba huo.

Salamu hizo zilieleza kuwa Price Nayef atakumbukwa kwa wema wake mkubwa kwa umma wa Wailamu walio wengi katika juhudi zake za kuendeleza na kuiimarisha din i ya Kiislamu pamoja na kuimarisha maendeleo katika nchi yake.

Sambamba na hayo salamu hizo zilimuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi. Amin.

Prince Nayef alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudia Arabia tangu mwaka wa 1975, na mwezi Oktoba mwaka jana, akiwa na umri wa miaka 78, aliteuliwa kuwa ndiye atakayemrithi Mfalme wa sasa, Mfalme Abdullah.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.