Habari za Punde

Hotuba ya Bajeti ya Serikali 2012/13

HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS
FEDHA, UCHUMI NA MIPANGO YA MAENDELEO
MHESHIMIWA OMAR YUSSUF MZEE

KUHUSU MPANGO WA MAENDELEO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA WA 2012/13 KATIKA BARAZA LA WAWAKILISHI

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena umefika wakati wa kutimiza matakwa ya Kifungu cha 105 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Kifungu hichi kinamtaka Waziri mwenye dhamana ya fedha kuwasilisha katika Baraza lako tukufu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka unaofuata wa fedha kabla ya kumalizika mwaka unaoendelea.

Mheshimiwa Spika, ili kutimiza matakwa hayo ya Katiba, naomba sasa kutoa hoja kwamba Baraza lako tukufu likae kama Kamati Maalum ya kujadili na hatimae kuidhinisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha wa 2012/13.

Mheshimiwa Spika, kama ilivyo desturi, sambamba na hotuba hii, naomba kuwasilisha pia Kitabu cha Kwanza kinachoelezea Mapitio ya Hali ya Uchumi na Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2011/12, Kitabu cha Pili kinachotoa Mwelekeo wa Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2012/13 na Kitabu cha Tatu ambacho ni Mswada wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2012/13. Naomba maelezo ya vitabu hivi nayo yawekwe katika kumbukumbu za Baraza.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza kusoma hotuba hii, naomba nitangulize shukurani kwa Muumba wetu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima wa afya na uwezo wa kukutana kwa mara nyengine tena leo hii. Namuomba atujaalie sote hekima ili tuendeshe kikao chetu kwa maelewano makubwa, utulivu na upendo.

Mheshimiwa Spika, naomba pia nimshukuru mkuu wa nchi yetu, Mheshimiwa Rais, Dr. Ali Mohamed Shein, kwa busara na juhudi kubwa anazozichukua katika kuiongoza vyema Zanzibar kwa lengo la kuiletea maendeleo pamoja na watu wake. Namshukuru pia kwa imani yake kwangu na kuendelea kunipa jukumu hili kubwa la kusimamia masuala ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo. Napenda kumuahidi kuwa nitatekeleza jukumu hili kwa uwezo wangu wote niliopewa na Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Spika, kupitia Baraza lako tukufu, naomba kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa utaratibu alioanzisha wa kufuatilia kwa ukaribu zaidi matatizo ya wananchi kupitia ziara zake za Mikoa na usimamizi mahiri wa utendaji wa Serikali hasa kwa kukutana na Wizara na Taasisi zake ili kupata taarifa za mipango na utekelezaji wake pamoja na namna fedha za umma zilivyotumiwa. Utaratibu huu umeimarisha zaidi ufanisi katika utendaji wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, naomba pia kuchukua fursa hii kuwapongeza wasaidizi wakuu wa Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamo wa Kwanza wa Rais na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamo wa Pili wa Rais kwa ushauri wao mkubwa kwake ambao umesaidia sana katika kufikia maamuzi yenye hekima na busara. Namuomba Mwenyezi Mungu awazidishie hekima na busara ili waweze kumsaidia vyema Mheshimiwa Rais wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, tokea tumalize kikao chetu cha Bajeti cha mwaka jana, kuna matukio mengi ya kuhuzunisha ambayo yametokea nchini kwetu na hapa Barazani. Sote bado tunakumbuka vyema tukio kubwa la msiba lililoikumba nchi yetu, usiku wa tarehe 10 Septemba 2011 lililohusisha kuzama kwa meli ya MV Spice Islander II. Mamia ya wananchi wenzetu; wazee, ndugu na watoto wetu, tuliokuwa karibu nao sana walipoteza maisha katika tukio lile. Tumelia, tumenyamaza, lakini hatujasahau. Kwa mara nyengine tena tunamuomba Mwenyezi Mungu Muweza wa yote azipokee roho za wapendwa wetu na awape malazi mema Peponi, AMIN.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Baraza lako tukufu, kipindi hichi cha mwaka mmoja tumewapoteza wenzetu wawili ambao nao wametangulia mbele ya haki, Marehemu Mussa Khamis Silima, aliekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Uzini na Marehemu Salum Amour Mtondoo aliekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Bububu, wote kupitia Chama Cha Mapinduzi, CCM. Tunaungana na familia zao kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wepesi wa kurudi kwake na malazi mema katika pepo yake tukufu, AMIN.

Mheshimiwa Spika, naomba pia kuchukua fursa hii kumpongeza sana Mhe. Mohammedraza Hassan Dharamsi kwa kuchaguliwa kwa kishindo na wananchi wa Jimbo la Uzini kuziba pengo lililoachwa na marehemu Mussa. Sina wasiwasi kuwa wananchi wa Jimbo la Uzini wamepata uwakilishi mwengine mzuri kupitia kwa Mhe. Raza. Nae tunamtakia kila la kheri katika kuwatumikia Wananchi wa jimbo hilo. Aidha, tunasubiri kwa hamu kupata tena uwakilishi wa Jimbo la Bububu wakati utakapokamilika mchakato wa uchaguzi mdogo.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, naomba sasa nianze kwa kuwasilisha Mapitio ya Hali ya Uchumi, Bajeti na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2011/12.

MAPITIO YA HALI YA UCHUMI, BAJETI NA MPANGO WA MAENDELEO 2011/12

Hali ya Uchumi Duniani na Kikanda

Mheshimiwa Spika, dunia imeendelea kushuhudia kudorora kwa uchumi ukijidhihirisha katika kupungua kwa kasi ya ukuaji wake, kwa ujumla na kwa kila Kanda. Kwa mwaka 2011, uchumi wa dunia umekua kwa wastani wa asilimia 3.9 ikilinganishwa na ukuaji wa wastani wa asilimia 5.3 kwa mwaka 2010. Hali kama hiyo ya kupungua kasi ya ukuaji imejitokeza kwa nchi zilizoendelea ambapo uchumi wake umekua kwa wastani wa asilimia 1.6 kwa mwaka 2011 ambayo ni nusu tu ya ukuaji wa wastani wa asilimia 3.2 mwaka 2010. Aidha, uchumi wa nchi zinazoendelea umekua kwa wastani wa asilimia 6.2 kwa mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 7.5 iliyoripotiwa mwaka 2010.

Mheshimiwa Spika, hali katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, zikiwemo zile za Afrika ya Mashariki haina tofauti sana na taswira hiyo ya dunia. Kasi ya kukua kwa uchumi wa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara imepungua kutoka wastani wa asilimia 5.3 ya mwaka 2010 hadi asilimia 4.9 kwa mwaka 2011. Upunguaji wa kasi ya ukuaji wa uchumi umejitokeza zaidi katika nchi za Afrika ya Mashariki ambapo ukuaji halisi umepungua kutoka wastani wa asilimia 5.9 mwaka 2010 hadi asilimia 4.6 mwaka 2011 ambapo kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi ilionekana zaidi katika Sekta ya umeme, maji, ujenzi, madini, biashara na uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, mwenendo huu usioridhisha wa uchumi duniani unaendelea kusababishwa na matatizo ya kifedha katika nchi za Ulaya, mabadiliko ya tabia nchi, bei kubwa za mafuta na chakula duniani na machafuko ya kisiasa Mashariki ya Kati na baadhi ya maeneo ya Afrika ya Kaskazini kama vile Tunisia, Misri na Libya.

Mwenendo wa Bei Duniani

Mheshimiwa Spika, mwaka 2011 haukuwa mzuri katika utulivu wa bei. Kasi ya mfumko wa bei kwa nchi zilizoendelea na zinazoendelea imepanda kwa bidhaa za chakula na zisizo za chakula. Mfumko wa bei kwa nchi zilizoendelea umepanda hadi kufikia wastani wa asilimia 2.7 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 1.6 kwa mwaka 2010. Kwa nchi zinazoendelea, Mfumko wa Bei umefikia wastani wa asilimia 7.2 kutoka wastani wa asilimia 6.1 kwa mwaka 2010. Kusini mwa Jangwa la Sahara, Mfumko wa Bei umepanda na kufikia wastani wa asilimia 8.2 mwaka 2011 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 7.4 mwaka 2010. Kwa upande wa nchi za Afrika ya Mashariki, Mfumko wa Bei umefikia wastani wa asilimia 9.6 mwaka 2011 kutoka wastani wa asilimia 6.1 mwaka 2010. Kwa ujumla hali hii imetokana na kupanda kwa bei za mafuta na bidhaa za chakula hasa bidhaa za mchele, sukari, mahindi na ngano.

Uchumi wa Zanzibar

Mheshimiwa Spika, kinyume na mwenendo wa uchumi wa dunia na kikanda, mwaka 2011 uchumi wa Zanzibar umeonekana kukua vizuri. Pato halisi la Taifa limekua kwa asilimia 6.8 na kufikia TZS 1,198 bilioni (mwaka 2011) kutoka TZS 946.8 bilioni kwa mwaka 2010. Kasi hiyo ya ukuaji wa asilimia 6.8 ni ya juu zaidi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Sababu zilizochangia kasi nzuri ya ukuaji wa uchumi wetu ni pamoja na hizi zifuatazo:

Kuimarika kwa Sekta ya Huduma kulikochangiwa zaidi na Sekta ndogo za Biashara na Hoteli na Mikahawa. Kuimarika kwa Sekta ndogo ya Biashara kumechangiwa zaidi na kuongezeka kwa uzalishaji na bei nzuri ya Karafuu katika soko la dunia. Jumla ya Tani 2,539 za Karafuu zilisafirishwa mwaka 2011 ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 19 kutoka Tani 2,132 zilizosafirishwa mwaka 2010. Usafirishaji huo umepelekea kukua kwa thamani ya usafirishaji nje kwa asilimia 77 kutoka TZS 11.2 bilioni mwaka 2010 hadi TZS 50.0 bilioni mwaka 2011. Kwa ujumla, Sekta ya Biashara ilikuwa kwa asilimia 21.5 mwaka 2011 ikiwa ni mara tatu ya ukuaji wa asilimia 7.0 mwaka 2010. Kwa upande wa Sekta ndogo ya Hoteli na Mikahawa, kumejitokeza ukuaji wa kuridhisha wa asilimia 10.2 ambao ni mara tatu ya ukuaji wa mwaka 2010 wa asilimia 3.0. Ukuaji huu umechangiwa na ongezeko la idadi ya watalii kwa asilimia 31.8 kutoka watalii 132,836 mwaka 2010 hadi kufikia watalii 175,067 mwaka 2011.

Ongezeko la asilimia 30.2 la uwekezaji rasilimali, hususan katika ujenzi wa barabara na madaraja.

Kuimarika kwa Sekta ya Viwanda iliyokua kwa asilimia 5.8 mwaka 2011 ukilinganisha na ukuaji wa asilimia 1.9 mwaka 2010 kutokana na mwenendo mzuri katika maeneo ya nishati, uchimbaji wa mawe na mchanga pamoja na ujenzi.

Mheshimiwa Spika, ukuaji mzuri wa Pato la Taifa uliopindukia kasi ya ongezeko la watu umepelekea kupanda kwa kiwango cha wastani wa Pato la Mtu Binafsi kutoka TZS 782,000 (USD 560) mwaka 2010 na kufikia TZS 960,000 (USD 617) mwaka 2011. Kiwango hiki cha pato la mtu binafsi kimevuka lengo lililowekwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi cha TZS 884,000 ifikapo mwaka 2015. Hali hii inatoa matumaini ya kuwa Ilani ya CCM inatekelezeka.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mfumo wa uchumi wetu, bado hakuna mabadiliko makubwa. Sekta ya huduma inaendelea kuongoza na kwa mwaka 2011 mchango wake umeongezeka kutoka asilimia 42.8 mwaka 2010 hadi asilimia 44 ya Pato la Taifa. Ongezeko hilo limepelekea kupungua kidogo kwa mchango wa Sekta ya Kilimo kutoka asilimia 32.4 mwaka 2010 na kufikia asilimia 32.2 mwaka 2011 na ule wa Sekta ya Viwanda kutoka asilimia 12.6 mwaka 2010 hadi asilimia 12.0 mwaka 2011. Mfumo wetu wa uchumi unaonesha kuwa bado tuna kazi kubwa ya kushajiisha maendeleo ya Sekta ya Viwanda nchini.

Mfumko wa Bei

Mheshimiwa Spika, kutokana na mtangamano mkubwa wa uchumi wetu na ule wa dunia hususan katika uagiziaji wa chakula na mafuta na matatizo ya uharamia katika “Pembe ya Afrika”, athari za mwenendo wa mfumko wa bei duniani na katika Kanda zimeleta msukumo wa bei kwenda juu hapa nchini. Kupanda kwa Mfumko wa Bei katika nchi tunazofanya nazo biashara nako kumechangia kupanda kwa Mfumko wa Bei nchini. Kasi ya mfumko wa bei kwa mwaka 2011 imepanda na kufikia asilimia 14.7 ikilinganishwa na asilimia 6.1 kwa mwaka 2010. Kwa ndani ya nchi, kushuka kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu nyingine kumechangia ongezeko hilo la kasi ya mfumko wa bei.

HALI YA BIASHARA



Biashara na Nchi za Nje

Mheshimiwa Spika, kutokana na mwenendo mzuri wa zao la karafuu kwa mwaka 2011, mwenendo wa sekta ya nje ulikuwa wa kuridhisha ukiambatana na kuongezeka kwa thamani ya bidhaa na huduma. Nakisi katika urari wa biashara ya bidhaa kati ya Zanzibar na nchi za nje imepungua kwa asilimia 8 na kufikia TZS 102.9 bilioni mwaka 2011 kutoka nakisi ya TZS 111.2 bilioni mwaka 2010. Hali hii imetokana na ukuaji mzuri wa Usafirishaji wa bidhaa ambapo usafirishaji ulikua kwa asilimia 242.5 kutoka TZS 17.9 bilioni mwaka 2010 hadi TZS 61.3 bilioni mwaka 2011. Ukuaji wa usafirishaji ulipindukia ukuaji wa uagiziaji ambao ni asilimia 27.2 kutoka TZS 129.1 bilioni mwaka 2010 hadi TZS.164.2 bilioni kwa mwaka 2011.

Uwekezaji Binafsi

Mheshimiwa Spika, ukuaji wa uchumi wetu umechangiwa pia na kukua kwa kiwango cha uwekezaji binafsi kilichopanda kwa asilimia 40.2 na kufikia Dola za Marekani (USD) 161.6 milioni mwaka 2011 kutoka USD 115.2 milioni mwaka 2010. Ongezeko hili limetokana na miradi ya biashara ya jumla na reja reja, usafiri, usarifu wa bidhaa, hoteli na mikahawa, maghala na mawasiliano, kilimo uwindaji na misitu, ukodishaji wa nyumba na bidhaa nyenginezo.

Maendeleo ya Kiuchumi

Mheshimiwa Spika, ukuaji wa uchumi pekee hautoshi. Kinachotakiwa ni kuwa na ukuaji unaoleta manufaa kwa Wananchi walio wengi. Ukuaji wa uchumi utafsirike katika maendeleo ya watu. Kwa upande wetu, juhudi mbali mbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kupitia utekelezaji wa MKUZA zimesaidia sana katika kuimarika kwa hali na ustawi wa kimaisha kwa wananchi wa Zanzibar. Miongoni mwa mafanikio hayo ni haya yafuatayo:

Kupungua kiwango cha uzazi kwa kina mama wenye umri wa miaka 15 - 49 kutoka wastani wa watoto 5.4 mwaka 2004/05 hadi kufikia watoto 5.1 mwaka 2009/10.

Kupungua vifo vya kinamama vinavyotokana na uzazi kutoka vifo 473 mwaka 2006 hadi 279 mwaka 2009 kwa kila mama 100,000.

Kushuka kwa vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja kutoka 61 mwaka 2004/05 hadi vifo 54 mwaka 2009/10 kwa kila vizazi hai 1000.

Kuongezeka kwa wastani wa kuishi wa Mzanzibari wakati wa kuzaliwa hadi kufikia miaka 60 mwaka 2011.

Kupungua kiwango cha umasikini wa kipato cha Wazanzibari kwa upande wa huduma za msingi (Basic Needs Poverty) kutoka asilimia 49.1 mwaka 2004/05 hadi asilimia 44.4 mwaka 2009/10.

Kuimarika kwa wastani wa uwiano wa walimu kwa wanafunzi na kufikia mwalimu mmoja kwa wanafunzi 27 mwaka 2011 ukilinganishwa na wastani wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 28 mwaka 2010.

Wananchi wanapata huduma za afya ndani ya kilomita tano.

Kushuka kwa kiwango cha watoto chini ya miaka mitano ambao uzito wao haulingani na kimo chao (Under 5 – Underweight) kutoka asilimia 39.9 mwaka 1990 hadi asilimia 8.1 mwaka 2010.

Kuongezeka kwa wastani wa watoto waliopata chanjo ya shurua kufikia asilimia 95.8 mwaka 2009 ambapo lengo ni kufikia asilimia 100 mwaka 2015.

Kiwango cha watoto chini ya umri wa mwaka mmoja ambao wamepata chanjo zote imefikia asilimia 91.8 kwa mwaka 2009. Ingawa kiwango hichi kilishuka katika mwaka 2010, kupitia juhudi maalum za kuhamasisha jamii kushiriki kwenye chanjo mbali mbali kwa watoto kama shurua, polio na utoaji wa matone ya vitamini A hali iliimarika. Taarifa za mwaka 2012 zinaonyesha kwamba asilimia 92 ya watoto chini ya miaka mitano wamepatiwa chanjo ya polio, asilimia 95 wamepatiwa matone ya vitamini A na asilimia 94.2 wamepatiwa dawa za minyoo.



SEKTA YA FEDHA



Huduma za Benki

Mheshimiwa Spika, matokeo mengine mazuri yaliyojitokeza mwaka 2011 ni kuimarika kwa huduma za fedha nchini. Wakati Amana za benki ziliongezeka kwa aslimia 12.9 kutoka TZS 311.88 bilioni Machi 2011 na kufikia TZS 352.07 bilioni Machi 2012, mikopo kwa sekta binafsi imekuwa kwa asilimia 46.4 kutoka TZS 100.36 bilioni hadi TZS 146.89 bilioni katika kipindi hicho. Uwiano wa mikopo na amana ulifikia asilimia 41.7 mwezi wa Machi 2012, kutoka asilimia 32.2 mwezi Machi 2011.

Mheshimiwa Spika, jambo la kufurahisha ni kuona kuwa wananchi wamehamasika katika kuchukua mikopo. Hadi kufikia mwezi Machi 2012 mikopo iliyotolewa kwa matumizi ya watu binafsi (personal loans) imefikia TZS 53.40 bilioni ambayo ni zaidi ya thuluthi moja ya mikopo yote (36.4%). Sehemu nyengine ya mikopo hii imeelekezwa zaidi katika Sekta za kiuchumi ambapo Sekta ya Biashara imeongoza katika kundi hili kwa kukopa TZS 28.18 bilioni sawa na asilimia 19.2 ya mikopo yote na Sekta ya Utalii ilikopa jumla ya TZS 22.38 bilioni, sawa na asilimia 15.2. Aidha mikopo katika sekta ya ujenzi ilifikia TZS 6.51 bilioni, sawa na asilimia 4.4 na sekta ya usafiri ilifikia TZS 3.06 bilioni, sawa na asilimia 2.1. Hali hii inaashiria kuongezeka kwa matumizi ya benki sio tu kwa kuhifadhi fedha za wateja na kujiwekea akiba, lakini pia katika kujiletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali 2011/12

Mheshimiwa Spika, Serikali ilikadiria kukusanya na kutumia jumla ya TZS 613.08 bilioni katika mwaka wa fedha 2011/12 unaoendelea. Kati ya mapato hayo, TZS 241.84 bilioni ikiwemo mapato ya kodi na yasiyo ya kodi pamoja na mikopo ya ndani na kiasi kilichobakia cha TZS TZS 371.24 bilioni zilitarajiwa kutokana na Washirika wa Maendeleo. Kwa upande wa Matumizi, TZS 234.18 bilioni ziliidhinishwa kutumika kwa kazi za kawaida na TZS 378.90 bilioni kwa kazi za maendeleo. Muhtasari wa mwenendo wa mapato na matumizi kwa kipindi cha miezi tisa hadi Machi 2012 ni kama hivi ifuatavyo.

Mapato ya Ndani

Mheshimiwa Spika, Kati ya mapato ya ndani yaliyokadiriwa ya TZS 221.2 bilioni sawa na asilimia 18.5 ya Pato la Taifa, TZS 210.2 bilioni zilitarajiwa zitokane na vianzio vya kodi na TZS 11.02 bilioni ni kutokana na vyanzo visivyokuwa vya kodi. Kati ya TZS 210.2 bilioni zilizotokana na kodi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikadiriwa kukusanya TZS 100.6 bilioni zikiwemo TZS 18 bilioni kutokana na Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaofanya kazi Zanzibar. Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ilitarajiwa kukusanya kiasi kilichobakia cha TZS 109.6 bilioni. ZRB ilitarajiwa pia kukusanya TZS 11.02 bilioni za mapato yasiyo ya kodi.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi tisa (Julai 2011 hadi Machi mwaka 2012), Serikali ilikadiria kukusanya mapato ya ndani ya TZS 170.3 bilioni. Makusanyo halisi yalifikia TZS 169.6 bilioni sawa na asilimia 99.6 ya makadirio ya kipindi hicho. Ikilinganishwa na mwaka uliopita (2010/2011) katika kipindi kama hicho, kunajitokeza ukuaji wa mapato wa asilimia 27.6. Kati ya makusanyo hayo, mapato kutokana na kodi yalifikia TZS 152.1 bilioni ambazo sawa na asilimia 94.1 ya makadirio. Mapato yasiyokuwa ya kodi yalifikia TZS 17.5 bilioni sawa na asilimia 198.9 ya makadirio ya kipindi hicho. Kati ya mapato yasiokuwa ya kodi, TZS 7.8 bilioni ni gawio la faida kutoka Benki Kuu na TZS 9.7 bilioni ni mapato ya kutoka Mawizarani.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ukusanyaji wa mapato kitaasisi, katika kipindi cha miezi tisa (Julai – Machi 2011/12), TRA imekusanya jumla ya TZS 67.1 bilioni sawa na asilimia 88.6 ya makadirio ya kipindi hicho ya TZS 75.7 bilioni. Kutofikiwa kwa lengo hilo kumetokana zaidi na kutolipwa kwa TZS 15.5 bilioni za kodi ya mapato kwa wafanyakazi wa SMT waliopo Zanzibar. Ikilinganishwa na mwaka uliopita (2010/2011) katika kipindi kama hicho, kunajitokeza ukuaji wa mapato wa asilimia 20.4. Aidha Bodi ya Mapato Zanzibar ilikusanya jumla ya TZS 94.7 bilioni sawa na asilimia 100.7 ya makadirio kutokana na mapato ya kodi na yasiyokuwa ya kodi sawa na ukuaji wa asilimia 22.7 ikilinganishwa na mwaka uliopita katika kipindi kama hicho. Kati ya TZS 94.7 bilioni, mapato ya kodi yalifikia TZS 84.9 bilioni sawa na asilimia 99.0 ya makadirio.

Mheshimiwa Spika, Kodi ya Ongezeko la Thamani, Ushuru wa bidhaa za Petroli na Ushuru wa bidhaa zimechangia TZS 64.8 bilioni sawa na asilimia 38.2. Mchango wa Ushuru wa Forodha ni TZS 43.0 bilioni sawa na asilimia 25.4, Kodi ya Mapato kutokana na ajira TZS 12.9 bilioni sawa na asilimia 7.6, wakati mchango wa Kodi Nyenginezo ulifikia TZS 41.0 bilioni sawa na wa asilimia 24.1 ya mapato yote ya ndani.

MATARAJIO YA MAPATO HADI JUNI 2011/12

Mheshimiwa Spika, kutokana na utendaji wa miezi tisa na matarajio ya robo mwaka ya Aprili – Juni, inatarajiwa kwamba mapato ya ndani kwa mwaka mzima yatafikia TZS 217.1 bilioni sawa asilimia 98.1 ya makadirio. Mamlaka ya Mapato Tanzania inatarajiwa kukusanya jumla ya TZS 88.9 bilioni sawa na asilimia 88.4 ya makadirio, wakati Bodi ya Mapato Zanzibar inatarajiwa kukusanya jumla ya TZS 120.4 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 100.4 ya makadirio kutokana na mapato ya kodi na yasio ya kodi.

Mheshimiwa Spika, kati ya TZS 120.4 bilioni, mapato ya kodi yatafikia TZS 108.3 bilioni sawa na asilimia 98.7 ya makadirio wakati mapato yasiyokuwa ya kodi kutoka katika Wizara za Serikali yatafikia TZS 12.1 bilioni sawa na asilimia 118 ya makadirio.

Mapato ya Nje

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2011/12, Serikali ilipanga kupokea jumla ya TZS 371.24 bilioni kutoka kwa Washirika wa Maendeleo zikiwemo TZS 30.28 bilioni za Misaada ya Kibajeti (GBS) na TZS 340.96 bilioni zikiwa mikopo na ruzuku kwa Program na Miradi ya Maendeleo. Kati ya hizo, ruzuku ni TZS 124.96 bilioni na mikopo TZS 216.0 bilioni.

Mheshimiwa Spika, hadi Machi 2012, jumla ya TZS 199.0 bilioni sawa na asilimia 53.6 ya matarajio ya mwaka zilipatikana zikiwemo TZS 24.1 bilioni za Misaada ya Kibajeti sawa na asilimia 79.7. Aidha jumla ya TZS 174.9 bilioni zilipatikana kupitia programu na miradi mbali mbali ikiwa sawa na asilimia 51.3 ya matarajio.

Mheshimiwa Spika, Matarajio ni kupatikana TZS 202.1 bilioni ambazo zitakuwa sawa na asilimia 59.3 ya matarajio ya fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kwa mwaka 2011/12. Mapato kutokana na misaada ya kibajeti yanatarajiwa kufikia TZS 30.3 bilioni sawa na asilimia 100 ya makadirio ya mwaka.

DENI LA TAIFA

Mheshimiwa Spika, hadi mwezi wa Machi, 2012 Deni la Taifa limefikia TZS 209.9 bilioni sawa na asilimia 15 ya Pato la Taifa. Kati ya kima hicho cha Deni, Deni la Ndani ni TZS 49.4 bilioni linalohusisha dhamana za Hazina na Hati Fungani za TZS 30.4 bilioni zinazotarajiwa kuwa tayari kulipwa kati ya Agosti 2012 na Julai 2016. Deni la Nje ni TZS 160.5 bilion (USD 102.0 milioni). Hadi kufikia Machi 2012 deni la Kiinua Mgongo lilifikia jumla ya TZS 2.4 bilioni ambapo jumla ya TZS 4.04 bilioni zililipwa kwa wastaafu 604 katika kipindi cha Mapitio. Tunatarajia kumaliza mwaka wa 2011/12 na deni la Kiinua Mgongo kwa ujumla litafikia TZS 4.5 bilioni kwa wafanyakazi watakaostaafu mwezi wa Aprili hadi Juni 2012.

UTEKELEZAJI WA HATUA ZA KUIMARISHA MAPATO

Mheshimiwa Spika, katika Hotuba yangu ya Bajeti ya mwaka jana nilieleza dhamira ya Serikali ya kutopandisha viwango vya kodi na badala yake kuimarisha usimamizi wa kodi zilizopo. Moja ya eneo lililokuwa likilalamikiwa sana katika kuikosesha Serikali mapato ni uingizaji wa mafuta ya petroli kwa njia ya magendo. Hatua maalum ilibidi kuchukuliwa ili kukabiliana na uhalifu huo.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hichi, Serikali imepiga marufuku utaratibu uliokuwa ukitumika wa kuingiza mafuta kwa kuuziana bahari kuu na kuhamisha meli moja kwenda nyengine. Utaratibu huu ulibainika kuwa ndio chanzo kikuu cha magendo. Sambamba na hatua hiyo, Serikali kupitia ZRB na Polisi na Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) ilifanya zoezi maalum la kupambana na magendo hayo. Matokeo ya zoezi hilo ni kukamatwa jumla ya lita 165,523 ya mafuta ya nishati yaliyokuwa yakiingizwa nchini kwa magendo.

Mheshimiwa Spika, hatua nyengine za kiutawala zililenga katika kuongeza ujuzi wa wasimamizi wa kodi wa TRA na ZRB, kusajiliwa katika mtandao wa kodi kwa wafanyabiashara wapya 290 Pemba na Unguja na kufanya ukaguzi wa pamoja baina ya TRA na ZRB kwa baadhi ya walipakodi.

Mheshimiwa Spika, hatua moja ambayo haikutekelezwa katika kipindi hiki ni kukusanywa kwa kodi ya mapato ya wafanyakazi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano waliopo Zanzibar. Hatua hii ilitarajiwa kuiingiza jumla ya TZS 18 bilioni. Utekelezaji ulitegemea kutekelezwa na SMT kwa makubaliano hayo ya Serikali mbili. Kwa bahati mbaya utekelezaji haukuanza katika mwaka wa 2011/12 na hivyo kuathiri kiwango cha utendaji cha TRA na Bajeti ya SMZ kwa ujumla. Matarajio yetu ni kuwa utekelezaji huo sasa utaanza katika mwaka ujao wa fedha baada ya marekebisho ya Sheria yanayohitajika.

MATUMIZI YA SERIKALI MWAKA 2011/12



Makadirio ya matumizi ya Serikali

Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2011/12 jumla ya TZS 613.1 bilioni zimekadiriwa kutumika. Katika kipindi cha tathmini, matumizi halisi yamefikia TZS 377.0 bilioni sawa na asilimia 117.3 ya makadirio ya miezi tisa ya TZS 321.5 bilioni. Kati ya matumizi hayo TZS 174.9 bilioni ni kwa kazi za kawaida sawa na asilimia 99.7 ya makadirio ya miezi tisa ya TZS 175.4 bilioni. Kwa upande wa kazi za maendeleo matumizi yalifikia TZS 202.1 bilioni sawa na asilimia 138.3 ya TZS 146.1 bilioni ya makadirio ya miezi tisa. Kati ya fedha hizo TZS 27.2 bilioni ni fedha za ndani na TZS 174.9 bilioni ni kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Kati ya matumizi ya TZS 469.4 bilioni yanayotarajiwa hadi Juni 2012, TZS 228.6 bilioni sawa na asilimia 48.7 ni matumizi ya Kazi za Kawaida na TZS 240.8 bilioni sawa na asilimia 51.3 ni kwa kazi za maendeleo.

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO KWA KIPINDI CHA JULAI 2011-MACHI 2012

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo 2011/12, Serikali ilikamilisha mapitio na marekebisho ya Dira ya Maendeleo ya 2020 ya Zanzibar, Utayarishaji wa Mpango wa miaka mitano wa utekelezaji wa MKUZA II, Mpango Mkuu wa Ufuatiliaji wa MKUZA II na Tathmini ya Hali ya Mahitaji ya Wataalamu Nchini. Ili mipango hii ieleweke vizuri na kufanyiwa kazi na wananchi, hatua maalum za uelimishaji na uenezi zitachukuliwa.

Mheshimiwa Spika, lengo kuu la Dira ya 2020 ni kuondoa umasikini uliokithiri, kuwa na Maendeleo endelevu pamoja na uchumi wa kisasa unaohimili ushindani. Kwa kuwa nusu ya kipindi cha utekelezaji wa Dira kimemalizika, Serikali ilifanya tathmini ya utekelezaji wa Dira 2020 na hatimae kufanya marekebisho ya muelekeo kwa miaka 10 ijayo kutokana na mambo yaliyojitokeza yakiwemo haya yafuatayo:

Kwamba uchumi wa Zanzibar umeendelea kuimarika lakini ukuwaji wake haukufikia kiwango kilichotarajiwa.

Kumepatikana mafanikio mazuri katika kupunguza umaskini usio wa kipato kutokana na kupiga hatua katika huduma za jamii hususan elimu na afya. Hata hivyo, ukuaji wa uchumi haujapunguza sana umaskini wa kipato.

Kuna Maendeleo makubwa yaliofikiwa katika kuimarisha Utawala Bora hususan katika uhuru wa kujieleza, uwajibikaji na utulivu wa kisiasa.

Mheshimiwa Spika, matokeo haya ya tathmini ya utekelezaji wa Dira yetu ya 2020 yanabainisha kuwa pamoja na mafanikio tuliyoyapata katika nusu ya kwanza ya utekelezaji, bado tuna kazi kubwa ya kutekeleza katika nusu iliyobakia. Kazi hii inahusisha kujenga uchumi imara na wenye ushindani, kukuza hali za maisha ya jamii yetu na kuimarisha utawala bora. Ili kufanikisha matarajio hayo, Taarifa ya Mapitio imependekeza mambo ya kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitano (2010-2015) yakiwemo haya yafuatayo:

Kuwekeza katika mageuzi ya kitaasisi hasa katika utumishi wa umma;

Uwekezaji stadi wa rasilimali watu;

Kuweka vipaumbele vya msingi katika uwekezaji wa miundombinu ya usafirishaji, maji, umeme na mawasiliano;

Kuimarisha taasisi, sera na sheria ili kuhakikisha kuwepo kwa uwiano baina ya shughuli za watu na miundombinu ya mtandao; na

Kuimarisha Mpango wa ufuatiliaji na tathmini wa MKUZA.

Mheshimiwa Spika, kwa bahati njema, Mapendekezo haya yanashabihiana na mambo yaliomo katika MKUZA II na hivyo tutapoutekeleza vyema tutakuwa pia tumetekeleza Mapendekezo ya Mapitio ya Dira ya 2020. Ili kutekeleza MKUZA II, Serikali imeandaa Mpango wa Utekelezaji wa miaka mitano na kubainisha Mpango wa Uwekezaji Rasilimali wenye jumla ya Programu na Miradi 165. Jumla ya Dola za Kimarekani 2.7 bilioni zinahitajika kuutekeleza. Serikali itashirikiana na Sekta binafsi kuhakikisha kuwa nayo inashiriki kikamilifu katika uwekezaji huo.

Mheshimiwa Spika, ili kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa MKUZA II pamoja na kuwezesha kuchukuliwa hatua za marekebisho kwa wakati na Serikali na watekelezaji wengine, umeandaliwa Mpango Mkuu wa Ufuatiliaji na Tathmini. Dhamira kuu ya Mpango huo ni kupata taarifa sahihi za Mpango wa utekelezaji na matumizi ya rasilimali, hali ambayo itasaidia kuchukuliwa kwa wakati hatua za kurekebisha kasoro zinazojitokeza.

Mheshimiwa Spika, tathmini ya hali ya mahitaji ya wataalamu nchini imeonesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wafanyakazi katika sekta rasmi ni wenye elimu chini ya kidato cha sita. Maeneo yaliyobainika kuhitaji kipaumbele zaidi katika Mpango wa Mafunzo wa Miaka Mitano (2012-2016) ni pamoja na Udaktari wa fani mbali mbali pamoja na watumiaji wa vifaa vya afya (medical imaging), Wafamasia, Wachumi, Uvuvi, Kilimo, Utawala wa Biashara, Ununuzi (Procurement), Mifugo (Veterinary) Utafiti, Usimamizi wa Hoteli na Utalii, Utaalamu wa Madini ikiwa ni pamoja na mafuta (petroleum), (giologia), Mipango, Usimamizi Rasilimali Watu, Usimamizi wa Fedha, Teknologia ya Habari na Mawasiliano, Ualimu wa Sayansi na Hesabati, Uhandisi, Usanifu majengo (Architecture), Takwimu na Utaalamu wa Mazingira. Fani hizo ndizo zitakazopewa kipaumbele katika utoaji wa mikopo kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU NA MIRADI

Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema, jumla ya TZS 378.9 bilioni ziliidhinishwa kugharamia utekelezaji wa Programu 27 na Miradi 77 ya Maendeleo kwa mwaka 2011/12. Kati ya fedha hizo zilizopangwa, TZS 37.9 bilioni sawa na asilimia 10.1 zilitarajiwa kutolewa na Serikali na TZS 340.9 bilioni sawa na asilimia 89.9 zilitarajiwa kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2011-Machi 2012 jumla ya TZS 202.1 bilioni sawa na asilimia 53.3 zilitolewa kugharamia utekelezaji wa Programu/Miradi. Kati ya fedha hizo, (TZS 202.1 bilioni), TZS 27.2 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 13.5 zimetolewa na Serikali na TZS 174.9 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 86.5 ni mchango wa Washirika wa Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu MKUZA umepangwa ki-Klasta. Klasta ya kwanza ya Ukuzaji Uchumi na Upunguzaji Umasikini wa Kipato ilitarajiwa kutekeleza jumla ya Program 17 na Miradi 17 na kutengewa jumla ya TZS 183.2 bilioni sawa na asilimia 48.4 ya bajeti ya ya kazi za Maendeleo. Serikali ilitenga jumla ya TZS 15.8 bilioni sawa na asilimia 8.6 na wakati Washirika wa Maendeleo walitarajiwa kuchangia jumla ya TZS 167.5 bilioni sawa na asilimia 91.4 ya bajeti ya Klasta hii.

Hadi kufikia Machi 2012, Klasta ya kwanza imepatiwa jumla ya TZS 113.2 bilioni sawa na asilimia 62 ya bajeti ya mwaka ya Klasta hiyo na sawa na asilimia 58 ya bajeti ya mwaka ya kazi za Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Serikali imetoa TZS 11.6 bilioni sawa na asilimia 74 ya makadirio yake kwa Klasta hii na Washirika wa Maendeleo wamechangia kiasi cha TZS 101.6 bilioni sawa na asilimia 61.

Mheshimiwa Spika, Klasta ya Huduma na Ustawi wa Jamii ilipangiwa kutekeleza jumla ya Program 6 na Miradi 33 ya Maendeleo kwa gharama ya TZS 151.5 bilioni, sawa na asilimia 39.9 ya bajeti ya Maendeleo. Serikali ilitenga jumla ya TZS 12.9 bilioni sawa na asilimia 8.5 ya bajeti ya Klasta na Washirika wa Maendeleo walitarajiwa kuchangia jumla ya TZS 138.6 bilioni sawa na asilimia 91.5.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi 2012, Klasta hii imepatiwa kiasi ya TZS 46.5 bilioni sawa na asilimia 27.5 ya fedha zilizotolewa kwa utekelezaji wa Programu/Miradi ya Maendeleo, ambayo ni sawa na asilimia 31 ya makadirio ya matumizi ya Klasta hii. Serikali imetoa TZS 10.4 bilioni sawa na asilimia 81 ya makadirio yake ya mwaka na Washirika wa Maendeleo wamechangia TZS 36.1 bilioni sawa na asilimia 26.

Mheshimiwa Spika, Klasta ya tatu ni ya Utawala Bora na Umoja wa Kitaifa. Kwa mwaka 2011/12 Klasta hii ina Programu nne na Miradi 27 ya Maendeleo iliotarajiwa kutekelezwa iliyopangiwa kutumia TZS 44.2 bilioni sawa na asilimia 11.7 ya bajeti ya Maendeleo. Serikali ilitenga jumla ya TZS 9.3 bilioni sawa na asilimia 21 na Washirika wa Maendeleo walitarajiwa kuchangia jumla ya TZS 34.9 bilioni sawa na asilimia 78.9 ya bajeti ya Klasta ya tatu. .

Hadi kufikia Machi 2012, Klasta imepokea jumla ya TZS 36.5 bilioni sawa na asilimia 83 ya makadirio yake ya mwaka. Kati ya fedha hizo, Serikali imetoa TZS 5.1 bilioni sawa na asilimia 55 ya makadirio yake na Washirika wa Maendeleo wamechangia TZS 31.4 bilioni sawa na asilimia 90 ya makadirio ya Klasta ya tatu.

UTEKELEZAJI WA MAENEO YALIYOPEWA KIPAUMBELE KWA MWAKA 2011/12

Kuimarisha huduma ya afya
Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea na zoezi la mfumo wa kupeleka dawa kulingana na mahitaji halisi ya kituo, ambapo vituo 19 vimo katika Mpango huo wa majaribio. Aidha, hospitali ya Mnazi mmoja inaendelea kushirikiana na madaktari wa nje mbali mbali kuendesha kambi za operesheni. Katika kipindi cha miezi tisa cha Julai 2011 hadi Machi 2012, jumla ya wagonjwa 822 wamefanyiwa uchunguzi, kati yao wagonjwa 199 walifanyiwa upasuaji na Serikali kuokoa jumla ya Dola za Kimarekani 1.6 milioni kama wangesafirishwa nje ya nchi. Mashine mbili za kuhifadhia dawa za chanjo kwa ajili ya chanjo mpya ya kuzuia maradhi ya kuharisha pamoja na vifaa mbali mbali vya chumba cha wagonjwa mahtuti (ICU) vimenunuliwa. Ujenzi wa bohari kuu ya madawa unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Juni 2012.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio niliyoyaeleza awali, moja ya changamoto kubwa inayoikabili sekta ya afya ni idadi kubwa ya vifo vya mama na watoto. Serikali imeamua kuchukua hatua maalum za kukabiliana na hali hii. Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na malalamiko kutokana na hatua ya Serikali kutoza fedha kutoka kwa akina mama ili kuchangia huduma za kujifungua. Hali yetu ya fedha sasa imeimarika kiasi na hivyo Serikali inaweza kubeba jukumu hili bila ya kuathiri ubora wa huduma. Kama mtakavyokumbuka, wakati akiwa katika ziara Mkoa wa Kusini Unguja mnamo tarehe 9 Mei mwaka huu, Mhe. Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein aliagiza kusitishwa kwa tozo hilo kwa akina mama.

Mheshimiwa Spika, nina furaha kulijuilisha Baraza lako tukufu kuwa utekelezaji wa agizo hilo la Mheshimiwa Rais utaanza rasmi tarehe 1 Julai, 2012 na hivyo akina mama wanaojifungua katika hospitali za Serikali hawatachangia tena na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itagharamia gharama za kujifungua kwa akina mama hao.

Kuimarisha ubora wa elimu
Mheshimiwa Spika, Jumla ya madarasa 80 kati ya 200 ya skuli za msingi yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi yamekamilika na kuanza kutumika Unguja na Pemba. Aidha, jumla ya madawati 500 kwa skuli za msingi yamechongwa na kusambazwa katika skuli za Unguja na Pemba. Vile vile, skuli mpya tatu za sekondari zimekamilika na nyengine tisa ziko katika hatua za kukamilishwa. Walimu 186 wameajiriwa katika skuli mbali mbali Unguja na Pemba.

Kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama
Mheshimiwa Spika, uchimbaji wa visima vitatu katika maeneo ya Chumbuni na kisima kimoja katika Kituo Kikuu Saateni kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa huduma ya maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi umekamilika. Aidha, kazi za ulazaji wa mabomba mapya imefanyika kwa maeneo ya Kinuni, Kijichi, Magomeni, Mpendae, Chuini na Kihinani. Kwa upande wa Pemba uchimbaji wa visima, Ujenzi wa vituo, Ujenzi wa ‘wellhead’ pamoja na upelekaji wa umeme umekamilika kwa maeneo ya Chokocho, Michenzani, Junguni na Konde.

Kuimarisha sekta ya kilimo
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa miundombinu ya umwagiliaji, msingi mkubwa wa mita 670 na msingi wa ndani wa udongo wa mita 150 katika bonde la Bumbwisudi; mtaro wa saruji wa mita 200 katika bonde la Makombeni Pemba na mita 525 Kianga imejengwa. Ujenzi wa barabara ya kifusi mita 100 umefanyika Bumbwisudi; Pia tani 1090 za mbolea aina ya TSP 545 na Urea zimenunuliwa na kusambazwa kwa wakulima.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendeleza juhudi za kuimarisha kilimo cha mpunga wa NERICA baada ya majaribio ya mbegu hii kuonesha mafanikio. Katika kipindi cha Julai 2011 hadi Machi 2012 jumla ya tani 21 za mbegu zilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima na wazalishaji mbegu. Aidha mashamba ya mfano wa uzalishaji yamefanywa kwa shehia 230 Unguja na Pemba ili wananchi wapate kujifunza njia bora za ukulima na upandaji wa NERICA. Sambamba na hayo, mabwana shamba 183 na maafisa wilaya 18 pia wamepewa mafunzo hayo.

Kuanza kuweka mazingira bora ya uwezeshaji wananchi kiuchumi

Mheshimiwa Spika, mchakato wa kutayarisha Sera ya Uwezeshaji umeanza katika hatua za awali. Mafunzo ya mbinu za uandishi na utunzaji wa vitabu vya hesabu yametolewa kwa Wajasiriamali pamoja na uendelezaji wa Soko la Jumapili kwa Wajasiriamali katika eneo la Michenzani. Aidha, katika kipindi cha miezi tisa (Julai 2011-Machi 2012), jumla ya TZS 62.9 milioni zimetolewa kupitia Mfuko wa JK/AK na TZS 97.5 milioni kutoka Mfuko wa Kujitegemea.

Kuendeleza tafiti mbali mbali

Mheshimiwa Spika, jaribio la mbegu za aina tatu za mpunga zenye kustahamili maradhi ya ugonjwa wa manjano ya majani ya mpunga limefanyika pamoja na kufanya uchunguzi wa aina 15 za mbegu za mpunga; Tafiti za mbegu mpya aina 70 za mpunga zinaendelea. Uchunguzi wa udongo katika mabonde ya Mziwanda Pemba umefanyika na kuendeleza utafiti na udhibiti wa wadudu aina ya chonga.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya afya utafiti wa maradhi yasiyoambukiza (NCD) ulifanyika mwaka 2011 na kuonekana kuwa maradhi ya sukari, sindikizo la damu yameongezeka kwa kasi katika visiwa vyetu kutokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha. Aidha, katika Sekta ya Nishati, Serikali kwa msaada wa Jumuiya ya Ulaya, imefanya tathmini ya fursa ya aina ya nishati anuwai nchini kwa kuzingatia nishati kutokana na jua, upepo na taka. Matokeo ya awali yameonesha kuwa kisiwa cha Unguja kina fursa ya kuzalisha umeme kwa njia ya upepo ili kusaidiana na ule wa nguvu za maji unaonunuliwa kutoka TANESCO Tanzania Bara. Serikali inaendelea kufanya tafiti nyengine katika maeneo mbalimbali.

MWELEKEO WA HALI YA UCHUMI 2012/13



Mwelekeo wa Uchumi wa Dunia
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), hali ya kupungua kwa kasi ya ukuaji wa inatarajiwa kuendelea katika mwaka 2012. Uchumi wa dunia unatarajiwa kukua kwa asilimia 3.5 kwa mwaka 2012 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.9 kwa mwaka 2011. Uchumi wa nchi zilizoendelea nao pia unatarajiwa kukua kwa asilimia 1.4 kwa mwaka 2012 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 1.6 kwa mwaka 2011. Hii ni kutokana na kutotengamaa kwa uchumi katika nchi nyingi zilizoendelea tokea kutokea Mtikisiko wa Uchumi wa dunia mwaka 2008 na tatizo la madeni lililozikumba nchi za Ulaya.

Mheshimiwa Spika, hali ya kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi inatarajiwa pia kuonekana katika nchi zinazoendelea, ambapo uchumi wake utakuwa kwa wastani wa asilimia 5.7 kwa mwaka 2012 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.2 kwa mwaka 2011. Kwa baadhi ya nchi katika bara la Asia, hali hii itachangiwa zaidi na kushuka kwa usafirishaji wa bidhaa kwenda nchi zilizoendelea, wakati kwa nchi zilizo katika bara la Afrika na baadhi ya nchi zilizo Marekani ya Kusini, ukuaji wa uchumi unatarajiwa kupungua kutokana na kushuka kwa bei za bidhaa zinazozalishwa nchini humo katika soko la dunia.

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara unatarajiwa kuwa tofauti na mwenendo wa dunia na Kanda nyengine. Uchumi wa nchi hizo unatarajiwa kukuwa kwa kasi zaidi kufikia ukuaji wa asilimia 5.4 kwa mwaka 2012 ikilinganishwa na asilimia 5.1 kwa 2011. Kasi hii inachangiwa na kuvumbuliwa kwa visima vipya vya mafuta na upatikanaji wa madini kwa nchi kama vile Uganda, Angola na Kenya.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mwenendo wa bei, taswira inayojitokeza ni ya kutia moyo. Mfumko wa bei kwa nchi zilizoendelea unatarajiwa kushuka hadi kufikia asilimia 1.9 kwa mwaka 2012 ikilinganishwa na asilimia 2.7 kwa mwaka 2011. Aidha, mfumko wa bei kwa nchi zinazoendelea unatarajia kushuka hadi kufikia asilimia 6.2 kwa mwaka 2012 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 7.2 kwa mwaka 2011. Kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa za chakula duniani pamoja na matarajio ya kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia kutasaidia kupunguza kasi ya mfumko wa bei duniani.

Mwelekeo wa Hali ya Uchumi wa Zanzibar
Mheshimiwa Spika, uchumi wa Zanzibar kwa mwaka 2012 unatarajiwa kuimarika zaidi. Utekelezaji wa malengo ya uchumi unatarajiwa kwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2020, MKUZA II, Malengo ya Milenia pamoja na Mageuzi ya Msingi.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012, uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.5 kutoka ukuaji wa asilimia 6.8 mwaka 2011. Matarajio ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2012 yanatokana na mambo yafuatayo:

Kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya biashara hasa zao la karafuu.

Kuongezeka kwa uwekezaji binafsi ikiwa pamoja na miradi ya uvuvi wa bahari kuu, kilimo na miradi ya utalii.

Kuongezeka kwa uingiaji wa watalii nchini kutokana na hatua mbali mbali zinazoendelea kuchukuliwa na taasisi mbali mbali za kuutangaza utalii wa Zanzibar. Lengo ni utalii kwa wote, ambao utatuwezesha kila mmoja wetu kuweza kushiriki katika kuutangaza utalii wetu.

Kukamilika kwa uwekaji wa waya wa umeme wa chini ya bahari kutoka Rasi Kiromoni ya Tanzania Bara hadi Rasi ya Fumba. Ukamilikaji wa zoezi hilo litawezesha upatinakaji wa umeme wa uhakika katika Kisiwa cha Unguja ambapo utasaidia kushajihisha maendeleo ya kiuchumi.

Utekelezaji wa Program ya Mageuzi ya Kilimo Zanzibar, ambayo itashajihisha uzalishaji na kuongeza tija na kuhakikisha uhakika wa chakula.

Kuimarika zaidi kwa mashirikiano baina ya sekta za Umma na Binafsi (Public Private Partnership) ambapo sekta binafsi inatarajiwa kuwa ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, sambamba na matarajio ya kushuka Mfumko wa Bei duniani, kasi ya Mfumko wa Bei nchini nayo unatarajiwa kushuka hadi kufikia asilimia 8.7 mwaka 2012 ikilinganishwa na asilimia 14.7 mwaka 2011. Mbali na mwenendo wa bei duniani, kuimarika kwa uzalishaji wa ndani wa mazao ya chakula na biashara, kuimarika kwa Sekta ya Uvuvi na kuendelea kuimarika kwa thamani ya sarafu ya Tanzania nako kunatarajiwa kushusha msukumo wa Mfumko wa Bei.

MWELEKEO WA MPANGO WA MAENDELEO – 2012/13

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2012/13 utategemea zaidi utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2020 iliyorekebishwa, MKUZA II, pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala CCM ya mwaka 2010.

MAENEO YA KIPAUMBELE



Kuimarisha huduma ya afya
Mheshimiwa Spika, umuhimu wa huduma bora za afya sote tunaufahamu na hauhitaji kusisitizwa zaidi. Serikali ya Awamu ya saba imeweka mkazo maalumu katika kuimarisha huduma hizi hususan katika kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa na nyenzo mbali mbali za utibabu, kuvipandisha hadhi vituo vya afya na hospitali hatua kwa hatua na kuimarisha huduma za uzazi kwa mama na mtoto. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imedhamiria kuhakikisha kuwa ndani ya miaka mitatu ijayo, inabeba jukumu lote la upatikanaji wa dawa na nyenzo za utibabu na kuacha kutegemea Wafadhili katika eneo hilo muhimu. Kuanzia mwaka ujao wa fedha, bajeti ya ununuzi wa dawa itakuwa inaongezwa kila mwaka hadi lengo hilo lifikiwe. Sambamba na ununuzi huo wa dawa na nyenzo za utibabu, Serikali pia itakuwa inatenga fedha kwa ununuzi wa vifaa vyengine vya afya vinavyohitajika.

Kuimarisha ajira kwa vijana

Mheshimiwa Spika, karibu theluthi mbili (asilimia 63.1) ya watu katika jamii yetu ni ama watoto au vijana wasiopindukia umri wa miaka 24. Kwa upande mwengine, idadi kubwa ya vijana wetu wanamaliza skuli na kuingia katika soko la ajira kila mwaka. Takwimu zinaonesha kuwa kati ya vijana watano (asilimia 17 ya vijana) wenye umri wa kati ya miaka kumi na tano hadi ishirini na nne (24) mmoja hana ajira.

Mheshimiwa Spika, hali hii inamaanisha kuwa tatizo la ajira kwa vijana ni kubwa na linahitaji hatua makhsusi. Kwa mwaka ujao wa fedha, Serikali imeandaa Programu maalumu ya kuwawezesha vijana katika shughuli za kiuchumi ikiwemo uvuvi, kilimo, kazi za usafi wa mji, ujasiri amali na utalii. Programu hii ni hatua moja muhimu ya kukabiliana na tatizo la ajira. Hata hivyo, ili mafanikio kamili yaweze kupatikana, tunahitaji pia kuwafunza vijana wetu kubadilika katika mkabala wetu na kazi na kupunguza kuchagua sana aina ya kazi.

Kuimarisha ustawi wa wazee

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa malengo ya Mapinduzi matukufu ya 1964 ni kuimarisha ustawi wa wananchi wote, ikiwemo wa makundi yenye mahitaji maalum kama vile Wazee. Katika hotuba yangu ya Bajeti ya mwaka jana nilitangaza kuongezwa kwa posho la Wazee wanaotunzwa na Serikali kutoka Shilingi elfu kumi na tano hadi elfu arobaini na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuimarisha hali za wazee kadiri hali ya uchumi inavoruhusu. Hata hivyo, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar alipowatembelea wazee aliifafanua dhamira ya Serikali katika kuwahudumia wazee hao.

Mheshimiwa Spika, ahadi ile ya Serikali itaendelezwa kwa mwaka wa fedha 2012/13. ili kudumisha huduma kwa wazee wanaohudumiwa na Serikali, kuanzia mwaka ujao wa fedha, Serikali itawapatia wazee wanaoishi katika kituo cha Sebleni huduma kamili ya chakula, posho na matibabu. Wazee pia watapatiwa vitambulisho vitakavyowawezesha kupata huduma mbali mbali kwa utaratibu maalum. Huduma kama hizi kwa wazee wanaoishi Welezo zinakwenda vizuri.

Kuimarisha Elimu

Mheshimiwa Spika, hakuna nchi inayoweza kuendelea bila ya kuwa na jamii iliyoelimika vya kutosha. Kwa kutambua ukweli huu, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbali mbali kuimarisha upatikanaji, usawa na ubora wa elimu nchini. Elimu ya lazima itaimarishwa kwa kuendeleza ujenzi wa skuli za ghorofa za Kiembe Samaki, Mpendae, Kwamtipura, Kibuteni na Mkanyageni pamoja na ununuzi wa madawati na vifaa vya kusomea na kufundishia. Aidha, Mfuko wa elimu ya juu utaimarishwa kwa kuongeza utoaji na urejeshaji wa mikopo ili vijana wengi zaidi waweze kufaidika na mikopo kwa ajili ya elimu ya juu.

Kuimarisha uchumi

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa uimarikaji wa ukuaji wa uchumi unaleta tija kwa wananchi, Serikali katika mwaka 2012/13 imeweka mikakati ifuatayo:

Kuendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri ikiwemo barabara na viwanja vya ndege.

Kuimarisha upatikanaji wa zana za kilimo, mbegu bora na mbolea kwa wakulima, sambamba na uimarishaji wa zao la karafuu.

Kuendeleza kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama pamoja na miundombinu ya maji machafu.

Kuhifadhi Mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi

Mheshimiwa Spika, sote tunashuhudia mabadiliko makubwa yanayoendelea duniani kwetu kutokana na “mabadiliko ya tabia nchi”. Miongo tulioizoea imebadilika sana, haitabiriki na imebadilisha pia mwenendo wa maisha yetu. Athari kamili za mabadiliko hayo bado hazijulikani, ingawa imethibitishwa kuwa hali ya joto duniani inapanda, kina cha maji ya bahari kinaongezeka, upatikanaji wa maji ya kunywa na mfumo wa afya nao unaweza kuathirika. Zanzibar kama nchi nyengine yoyote ile inahitaji kuwa tayari na hali hiyo na kuchukua hatua za kujihami na athari hizo.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa msaada wa Shirika la Misaada la Uingereza (DIfD) imefanya utafiti uliolenga kubainisha namna mabadiliko ya tabia nchi yanavyoweza kuathiri maendeleo ya kiuchumi nchini kwetu. Matokeo ya utafiti huo yamesaidia katika uandaaji wa Mpango wa Zanzibar wa Kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabia nchi na Uhifadhi wa Mazingira. Kwa kuwa suala hili ni muhimu na ni mtambuka, ni wajibu wetu sote kuchukua kila juhudi kuhifadhi mazingira yetu na kukabiliana na athari hizo za mabadiliko ya tabia nchi.

MASHIRIKIANO NA SEKTA BINAFSI



Mheshimiwa Spika, mashirikiano baina ya sekta za umma na sekta binafsi (PPP) ni muhimu katika kukuza miundombinu ya uchumi ambayo ni kichocheo kikubwa cha kuleta maendeleo ya nchi. Kwa upande wa Zanzibar, mashirikiano ya sekta ya Umma na ya Binafsi yataharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo tafauti kama vile kukuza uzalishaji wa bidhaa za viwandani, kilimo, biashara, kukuza ajira, kuimarisha miundombinu ya kiuchumi na kijamii pamoja na kuongezeka kwa mapato.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13 Serikali imekusudia kuanzisha Kitengo cha “PPP” katika Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo kwa madhumuni ya:

Kuandaa sera ya mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na ya Binafsi.

Kuandaa mkakati, mpango na muundo wa kuendeleza mashirikiano hayo.

Kutoa taaluma ya dhana ya “PPP” kwa wadau pamoja na kuandaa midahalo (debates) itakayoamsha ari za mashirikiano.

Kuingiza dhana ya “PPP” katika mipango ya wizara na taasisi za Serikali.

Kutekeleza lengo la nne la klasta ya kwanza ya MKUZA II linalotaka kuundwa kwa sekta binafsi imara hapa nchini.

KUIMARISHA MAENDELEO YA JIMBO

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/13, Serikali itaanza utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo baada ya hatua za matayarisho ikiwemo uundwaji wa sheria ya kusimamia mfuko huu kukamilika. Mfuko huu unachukua nafasi ya utekelezaji wa miradi midogo midogo ya wananchi, ambapo kila jimbo lilikuwa likipatiwa kiasi cha TZS 10 milioni. Serikali imekusudia kuimarisha maendeleo ya majimbo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo baada ya kupitishwa Sheria ya kuanzisha Mfuko huo. Jumla ya TZS 760 milioni zimetengwa na kila jimbo litapatiwa TZS 15 milioni mwaka 2012/13 kutoka TZS 10 milioni mwaka 2011/12, sawa na ongezeko la asilimia 50, ili kusaidia juhudi za wananchi katika kujiletea maendeleo.

Mheshimiwa Spika, usimamizi mzuri unahitajika kutoka kwa viongozi wa majimbo ili kupelekea kufikia malengo yaliyokusudiwa hasa katika Mkakati wetu wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini. Ni imani ya Serikali kwamba matumizi ya fedha hizi zitafuata taratibu zote za manunuzi kama zinavyoainishwa katika sheria ya Usimamizi wa Fedha na sheria ya Manunuzi na Uondoshaji wa Mali za Serikali.

MPANGO WA MAENDELEO KWA MWAKA 2012/13

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13, Serikali imepanga kutekeleza jumla ya Program 38 na Miradi 84 (Programu 6 na Miradi 18 ni mipya) katika Mpango wake wa Maendeleo. Kiasi cha TZS 341.1 bilioni zinatarajiwa kutumika kwa utekelezaji wa Mpango huo, ambapo Serikali imekadiria kuchangia TZS 47.9 bilioni sawa na asilimia 14 na Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia TZS 293.2 bilioni sawa na asilimia 86 ya Bajeti ya kazi za Maendeleo. Kati ya fedha zinazotoka kwa Washirika wa Maendeleo, TZS 187.7 bilioni ni mkopo na TZS 105.4 bilioni ni ruzuku.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka ujao wa fedha, Klasta ya kwanza ina jumla ya Program 21 na Miradi 25 itakayogharimu kiasi ya TZS 197.9 bilioni sawa na asilimia 58 ya makadirio ya bajeti ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo TZS 18.9 bilioni sawa na asilimia 10 zinatarajiwa kutolewa na Serikali na TZS 179.0 bilioni ni mchango kutoka kwa Washirika wa Maendeleo sawa na asilimia 90. Aidha, mikopo ni TZS 104.5 bilioni na ruzuku ni TZS 74.5 bilioni.

Mheshimiwa Spika, Klasta ya pili ya Huduma za Jamii na Ustawi inatarajiwa kutumia TZS 117.7 bilioni sawa na asilimia 35 kugharamia utekelezaji wa Program 11 na Miradi 33. Serikali inatarajiwa kutoa TZS 13.7 bilioni sawa na asilimia 12 ya bajeti yote ya Klasta hii na Washirika wa Maendeleo TZS 104.0 bilioni sawa na asilimia 88. Mkopo ni TZS 79.9 bilioni na ruzuku ni TZS 24.1 bilioni.

Mheshimiwa Spika, Klasta ya Utawala Bora na Umoja wa Kitaifa inatarajiwa kutekeleza Program sita na Miradi 26 yenye, jumla ya TZS 25.4 bilioni sawa na asilimia 7 ya bajeti ya Maendeleo. Serikali inatarajiwa kutoa TZS 15.3 bilioni sawa na asilimia 60 na Washirika wa Maendeleo TZS 10.1 bilioni sawa na asilimia 40 ya makadirio ya Klasta ya tatu ambapo Mikopo ni TZS 3.2 bilioni na ruzuku ni TZS 6.9 bilioni.

Miradi mikuu kwa bajeti ya 2012/13



Mheshimiwa Spika, miradi mikuu inayotarajiwa kutekelezwa kwa mwaka huu wa fedha ni pamoja na kukamilisha na kuzindua Ujenzi wa njia ya pili ya umeme kutoka Ras-Kiromoni hadi Fumba, Mradi wa Kuimarisha Njia za Umeme, Mradi wa Kuendeleza Ujenzi wa Jengo Jipya la Abiria - Uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume, Mradi wa kuimarisha Elimu ya lazima, Mradi wa Elimu Mbadala na Amali, Programu ya Kukuza Ajira kwa Vijana na Programu ya Kuimarisha Miundombinu ya Afya.

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na uhaba mkuwa wa ofisi za Serikali na uchakavu wa ofisi zilizopo, Serikali pia itaanzisha Mfuko maalum kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Serikali. Fedha za Mfuko huo zitatokana na kiasi kitakachoidhinishwa na Baraza lako tukufu na fedha zitakazotokana na mauzo ya majengo makongwe ya Serikali.

MAANDALIZI YA BAJETI INAYOZINGATIA PROGRAMU

Mheshimiwa Spika, Bajeti ni nyenzo muhimu ya kuimarisha huduma kwa wananchi na utawala bora. Serikali inaendelea na mageuzi yenye lengo la kuimarisha uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa bajeti, ili kuleta manufaa zaidi kwa wananchi. Mageuzi haya yanakusudia kuanzisha mfumo wa bajeti unaozingatia matokeo kupitia utekelezaji wa Programu. Lengo ni kuhakikisha kuwa kila Shilingi inayoidhinishwa na Baraza hili na kutumiwa na Serikali inaleta manufaa kwa walengwa na wananchi kwa ujumla. Katika utaratibu huu, bajeti za kila Wizara au Taasisi zitaandaliwa kwa kuzingatia muundo na majukumu yake na kuandaa Programu ambazo zitaainisha matokeo yanayotarajiwa kutokana na kutekelezwa Programu hizo.

Mheshimiwa Spika, matayarisho ya utaratibu huo mpya wa bajeti yanaendelea vizuri. Kwa kuanzia, utaratibu huu unatekelezwa kwa majaribio ukihusisha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo na Maliasili, Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo. Kwa hatua ya sasa, Wizara hizo zimeweza kutayarisha Muundo wa Programu na Maelezo ya programu yenye kuhusisha Malengo, Matokeo, Viashiria, shabaha na gharama za programu. Lengo kwa mwaka huu wa fedha ni kuwasilisha maelezo hayo ya Programu kwa taarifa tu sambamba na bajeti za Wizara hizo zilizo katika mfumo wa sasa.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13, Serikali itaendeleza mageuzi hayo ya bajeti kwa kuandaa muundo na maelezo kama hayo kwa wizara zote zilizobakia. Matarajio ni kwamba ifikapo mwaka 2014/15 Bajeti ya Serikali iwe inaandaliwa na kutekelezwa kwa kuzingatia mfumo huo wa Programu pamoja na uidhinishaji wa Sheria ya Matumizi.

MWELEKEO WA BAJETI 2012/13

Muundo wa Bajeti

Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kutumia jumla ya TZS 648.9 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2012/13, ikiwa ni ongezeko la asilimia 38.2 kutoka TZS 469.4 bilioni zinazotarajiwa kutumika hadi kufikia mwisho wa Juni 2012. Serikali pia inatarajia kuuanza mwaka wa fedha ikiwa na bakaa ya TZS 5.9 bilioni. Kwa kuzingatia uwezo wa sasa wa mapato kutokana na vyanzo vya ndani, inatarajiwa kuwa mapato ya ndani yatafikia jumla ya TZS 280.7 bilioni na hivyo kufanya jumla ya mapato hayo kufikia TZS 286.6 bilioni. Fedha hizo ni mjumuisho wa mapato ya Kodi na yasiyo ya kodi. Kiasi hicho cha mapato cha TZS 286.6 bilioni kitaacha nakisi katika Bajeti ya TZS 362.3 bilioni.

Mheshimiwa Spika, Katika mwaka huo wa 2012/13, Serikali inatarajia kupokea TZS 333.2 bilioni ikiwa ni Mikopo na Ruzuku kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ikiwemo Msaada wa Kibajeti TZS 40.0 bilioni na Mikopo na Ruzuku kwa ajili ya Programu na Miradi ya Maendeleo ya TZS 293.2 bilioni. Fedha hizo za TZS 333.2 bilioni zinapunguza nakisi ya Bajeti hadi kufikia TZS 29.1 bilioni.

Mheshimiwa Spika, ili kuziba pengo hilo la Bajeti, Serikali inapendekeza kuchukua hatua mbali mbali za kuimarisha mapato ya ndani kwa kurekebisha viwango vya kodi na ada za huduma mbalimbali. Kwa ujumla, hatua hizo zinatarajiwa kuingiza TZS 13.3 bilioni, ikiwemo gawio la TZS 2.7 bilioni kutoka Mashirika ya Serikali na hivyo kuzidi kupunguza pengo la Bajeti na kufikia TZS 15.8 bilioni. Serikali inatarajia kukopa ndani ili kuziba pengo hilo na hivyo kuleta uwiano wa mapato na matumizi katika Bajeti.

MAPENDEKEZO YA HATUA ZA KUIMARISHA MAPATO

Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema, Serikali inakusudia kurekebisha Sheria mbali mbali za Kodi ili kuziba nakisi ya bajeti iliyojitokeza. Kwa kuwa sio lengo la Serikali kutoza kodi itakayowaumiza wananchi, marekebisho haya yamezingatiwa kwa makini sana. Kutokana na mazingatio hayo, Serikali itaendelea na sera yake ya kutotoza Kodi ya Ongezeko la Thamani katika vyakula muhimu, huduma za afya, huduma za usafiri, mazao ya kilimo na ufugaji kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na dhamira hiyo nzuri ya Serikali ya kutoongeza kodi katika bidhaa na huduma za msingi kwa wananchi, bado tunahitaji kuchukua hatua maalum za kupunguza utegemezi katika uendeshaji wa Serikali yetu. Miongoni mwa hatua hizi zitalazimisha kuongeza kodi katika baadhi ya maeneo ili kukidhi mahitaji yetu ya matumizi na Mpango wa Maendeleo. Kwa kuzingatia dhamira hizo za Serikali, na ili kuziba nakisi ya bajeti katika mwaka ujao wa fedha 2012/13, Serikali inapendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya kodi katika Sheria zifuatazo:

Sheria ya Ushuru wa Stempu namba 6 ya Mwaka 1996.

Sheria ya Kodi ya Hoteli namba 1 ya mwaka 1995.

Sheria ya Ada za Bandari namba 2 ya mwaka 1999.



Sheria ya Ushuru wa Mafuta ya Petroli namba 7 ya mwaka 2001



Sheria ya Usimamizi na Utaratibu wa Kodi namba 7 ya mwaka 2009.



Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani namba 4 ya mwaka 1998



Sheria ya Bodi ya Mapato Zanzibar namba 7 1996 na



Sheria ya Mafunzo ya Amali namba 8 ya mwaka 2006.

Mheshimiwa Spika, Sambamba na marekebisho ya Sheria hizo, inapendekezwa kuzifanyia marekebisho Kanuni za Sheria kadhaa, ili kurekebisha viwango vya ada mbali mbali vilivyopitwa na wakati, ikiwemo vinavyohusu ukodishaji wa Ardhi kwa wawekezaji.

SHERIA YA USHURU WA HOTELI



Kurekebisha kiwango cha kodi katika huduma za mahoteli, mikahawa na kutembeza wageni

Mheshimiwa Spika, msingi mmoja muhimu wa kutoza kodi ni kuhakikisha kuwa mfumo wa kodi unakuwa na usawa kwa walipa kodi. Kwa bahati mbaya, kumekuwa na malalamiko kuwa utaratibu wa sasa, wa kutoza kiwango cha asilimia 18 kwa Wafanyabiashara waliosajiliwa chini ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na asilimia 15 kwa wenye mahoteli, mikahawa na watembeza wageni wasiosajiliwa na Kodi hiyo, haufuati msingi huo muhimu. Ili kurekebisha kasoro hiyo, inapendekezwa kuongeza kiwango cha Kodi kwa Mahoteli, Mikahawa na Watembeza Wageni wasiyosajiliwa kwenye VAT kutoka asilimia 15 ya sasa hadi asilimia 18. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato kwa jumla ya TZS 1.96 bilioni.

Mheshimiwa Spika, hatua hii ya kuleta uwiano wa viwango vya kodi itasaidia katika maeneo mengine kadhaa muhimu yakiwemo haya yafuatayo:

Kuhamasisha wafanyabiashara kujiunga kwa hiari kwenye mfumo wa Kodi ya Ongezeko la Thamani.

Kuongeza uwajibikaji wa kuweka na kutunza kumbukumbu za mauzo ambazo ni muhimili muhimu katika kulipa kodi inayostahili.

Kuimarisha ushindani miongoni mwa walipakodi zilizorekebishwa na wale wa VAT.

SHERIA YA USHURU WA STEMPU



Marekibisho ya Sheria ya Ushuru wa Stempu

Mheshimiwa Spika, moja ya Sheria ambayo viwango vyake ni vidogo na vimekaa bila ya kufanyiwa marekebisho kwa muda mrefu ni Sheria ya Ushuru wa Stempu. Serikali inapendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya Ushuru wa Stempu katika maeneo matatu ya Sheria hii kama ifuatavyo:

Kubadilisha kiwango cha utozaji wa ushuru wa stempu kwenye mikopo

Mheshimiwa Spika, Serikali imepokea na kuzingatia malalamiko kuhusu wakopaji, hususan wawekezaji kutakiwa walipie Ushuru wa Stempu kwa asilimia moja ya thamani ya mkopo. Ushuru huu umelalamikiwa kukwaza kukua kwa huduma za fedha kwa upande mmoja na uwekezaji rasilimali kwa upande mwengine. Matokeo ya mambo haya ni kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi wetu. Imebainishwa pia kuwa kuendelea kutozwa ushuru huu kwa asilimia ya thamani ya mkopo kunaathiri ushindani na nchi jirani. Ili kuondoa kasoro hiyo, Serikali inapendekeza kuweka ukomo wa kiwango cha juu cha kutoza Ushuru wa Stempu katika mikopo. Hatua hii haikusudii kuongeza mapato bali itasaidia kushajiisha uwekezaji biashara nchini sambamba na kuimarisha uwezo wa Zanzibar kiushindani (competitiveness) na usawa wa kodi miongoni mwa wakopaji.

Kurekebisha kiwango cha Ushuru wa Stempu kwa biashara

Mheshimiwa Spika, biashara zisizofikia kiwango cha mauzo cha kusajiliwa kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani pamoja na zile ambazo hazimo katika usajili wa mfumo wa ulipaji wa Kodi wa Hoteli hutozwa Ushuru wa Stempu kwa kiwango cha asilimia moja na nusu kwa mauzo yanayoanzia thamani ya TZS 1,000. Tofauti ya kiwango hichi na kile cha VAT ni kubwa sana. Inapendekezwa kuongeza kiwango cha Ushuru wa Stempu kutoka asilimia moja na nusu ya sasa hadi asilimia tatu. Hatua hivyo itaongeza mapato ya Serikali kwa TZS 2.10 bilioni.

SHERIA YA ADA YA BANDARI

Kurekebisha na kuweka kiwango kipya cha ada ya bandari

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuimarisha elimu hapa nchini. Pamoja na juhudi hizo, bado Sekta ya Elimu inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo upungufu wa madarasa na madawati na hivyo kuendelea kuathiri ubora wa elimu. Hatuwezi kutegemea Washirika wa Maendeleo pekee kwa kuondoa upungufu huo unaokadiriwa kuhitaji jumla ya TZS 27.0 bilioni kwa madawati peke yake. Ili kuanzisha juhudi za kupatikana fedha za kukabiliana na usumbufu huu unaowakabili watoto wetu, inapendekezwa kuongeza Ada ya Bandari kwa abiria wanaosafiri baina ya Zanzibar na Tanzania Bara kutoka TZS 1,000 ya sasa hadi TZS 2,000 na kutozwa ada ya TZS 1,000 kwa abiria wanaosafiri baina ya Unguja na Pemba. Hatua hiyo inakadiriwa kuingiza jumla ya TZS 2.00 bilioni. Fedha zote zitakazopatikana kutokana na ongezeko hili la Ada ya Bandari zitatumika kwa ununuzi wa madawati tu.

SHERIA YA USHURU WA MAFUTA YA NISHATI

Kurekebisha kiwango cha Ushuru wa mafuta ya nishati

Mheshimiwa Spika, Kwa kutambua umuhimu wa mafuta ya bidhaa za petrol kiuchumi na kijamii, Serikali imekuwa ikichukua hadhari katika marekebisho ya viwango vyake vya kodi. Kwa kuwa viwango vya Kodi hii ni maalum (specific) na havitegemei thamani ya bidhaa na kwa kuwa viwango vya sasa vya kodi vimekuwepo kwa muda mrefu bila ya kurekebishwa, kwa sasa vimepoteza thamani yake. Kwa mwaka ujao wa fedha, Serikali inakusudia kurekebisha kidogo kiwango cha Ushuru wa Mafuta ili kupunguza athari ya upotezaji wa thamani bila ya kuleta athari kwa mfumko wa bei kwa wananchi. Inapendekezwa kuongeza Ushuru wa Mafuta kwa TZS 50.00 kwa kila lita inayoingia nchini kwa mafuta ya Petroli na Dizeli tu. Hatua hii inatarajiwa kuiingizia Serikali TZS 3.3 bilioni.

SHERIA YA USAFIRI BARABARANI

Marekebisho ya viwango vya leseni ya njia

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanikiwa sana katika jitihada zake za kuimarisha miundombinu ya kiuchumi na kijamii nchini, mojawapo ikiwa ni mtandao wa barabara. Ujenzi wa barabara una gharama kubwa sana. Tunahitaji kuzitunza ili ziweze kutuhudumia kwa kipindi kirefu zaidi kijacho. Nyingi ya barabara hizi zimejengwa kwa mkopo na tunahitaji kuihudumia mikopo hiyo. Hata hivyo, kiwango cha sasa cha ada ya Leseni ya Njia cha TZS 24,000 kwa gari kwa mwaka hakizingatii matumizi ya njia kwa aina tofauti za gari. Inapendekezwa kurekebisha kiwango cha Leseni za Njia ili kiendane na uzito wa gari au na ukubwa wa injini yake. Hatua hii inatarajiwa kuiingizia Serikali jumla ya TZS 2.1 bilioni.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwengine, idadi ya magari nchini inaongezeka kila mwaka na hivyo kuathiri mazingira kutokana na moshi unaotoka katika magari hayo (carbon emission). Tunapaswa kuchukua hatua zaidi za kukabiliana na athari za uharibifu huo ikiwemo gharama za matibabu. Kwa mwaka ujao wa fedha, inapendekezwa kutozwa TZS 15,000 kwa kila gari kwa mwaka na TZS 3,000 kwa chombo cha moto cha magurudumu mawili au matatu. Hatua hii inatarajiwa kuingiza TZS 700 milioni. Serikali inakusudia kutumia asilimia 80 ya fedha hizo, sawa na TZS 560 milioni, kama ziada katika ununuzi wa dawa kwa ajili ya hospitali zetu wakati asilimia 20 iliyobaki sawa na TZS 140 milioni zitatumika kugharamia upandaji wa miti katika maeneo yaliyoharibiwa kimazingira kwa uchimbaji mchanga, mawe na kifusi na uharibifu wa ukanda wa pwani; kupanda Mikarafuu ili kufikia lengo la Serikali la upandaji wa mikarafuu angalau laki tano kwa mwaka; kupanda miti katika maeneo ya vianzio vya maji na kuleta haiba nzuri pembezoni mwa barabara hususan katika maeneo ya utalii.

KUREKEBISHA VIWANGO VYA ADA ZA HUDUMA MBALIMBALI

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoza ada kwa huduma zake mbalimbali katika Wizara, Idara na Taasisi zake. Serikali imesikiliza malalamiko ya muda mrefu ya Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako kuwa vingi ya viwango vya Ada hizo vimepitwa mno na wakati na vinahitaji kufanyiwa mapitio na kurekebishwa. Serikali itafanya mapitio hayo kwa Sheria na Kanuni zake na kurekebisha Ada hizo. Hatua hii inatarajiwa kuiingizia Serikali jumla ya TZS 0.5 bilioni.

KUIMARISHA USIMAMIZI NA UTAWALA WA KODI

Mheshimiwa Spika, mbali ya hatua za kuimarisha viwango vya Kodi, Ushuru na Ada mbalimbali, hatua maalum zitachukuliwa kuimarisha uwezo wa Taasisi zetu za kodi. Kwa upande wa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania, miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na hizi zifuatazo:

Kuimarisha Mfumo wa usimamizi kwa Maeneo (Block Management System):

Mheshimiwa Spika, ili kusimamia kwa karibu ukusanyaji mapato katika kila eneo, TRA kwa kushirikiana na ZRB zitagawa maeneo na kuweka usimamizi wake chini ya maofisa maalum watakaokuwa na jukumu la kuhakikisha kodi inakusanywa kwa shughuli zote za kiuchumi zilizo katika eneo husika. Ugawaji huo utatumia mfumo wa Kompyuta kutokana na database iliyopo katika Mradi wa Matumizi Endelevu ya Ardhi (SMOLE) ambao taarifa zake zinatumia mfumo wa GIS.

Kutumia mashine (Scanner) katika ukaguzi wa Kontena



Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kuweka mtambo maalum (Scanner) wa kukagulia makontena yanayoingia nchini katika bandari ya Malindi. Mtambo huu unaotarajiwa kupatikana kwa msaada wa Serikali ya Watu wa China, utasaidia kuimarisha mapato na usalama nchini kwa kutambua vitu vinavyoingizwa na hivyo kudhibiti udanganyifu unaofanywa na baadhi ya waingizaji wa bidhaa nchini wasio waaminifu.

Kurahisisha ulipaji wa kodi kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kwa kutumia simu za mikononi

Mheshimiwa Spika, katika miaka ya karibuni huduma za simu za mikononi zimesaidia sana katika kuimarisha huduma za fedha kwa wananchi ambao hutumia simu katika kutuma fedha na kufanyia malipo ya huduma mbali mbali. Serikali, kupitia TRA na kwa mashirikiano na Benki ya Watu wa Zanzibar, itaanza kutumia teknolojia hiyo ya simu za mikononi katika ulipaji kodi. Njia hii inatarajiwa kuimarisha ufanisi katika ulipaji wa kodi kwa hiari kwa upande wa Wafanyabiashara wadogo wadogo na kuokoa muda wao na hivyo kuwapa fursa zaidi za kuendeleza biashara zao.

iv. Marekebisho ya kiwango cha Mauzo kwa usajili wa VAT

Mheshimiwa Spika, kupitia ZRB, Serikali pia imefanya mapitio ya kiwango cha mauzo ambacho Mfanyabiashara hutakiwa kujisajili na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). Lengo la mapitio hayo ni kuhakikisha kuwa kiwango hicho kinakwenda na wakati, kinasaidia kuongeza ufanisi kwa kuhakikisha kuwa wanaosajiliwa ni wale tu wenye mauzo na biashara kubwa, na kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati (SMEs) kupata fursa ya kukua kwanza kabla ya kuingizwa katika mfumo wa VAT. Kutokana na mapitio hayo, inapendekezwa kupandisha kiwango cha mauzo ambacho Mfanyabiashara asiekifikia hatosajiliwa kwenye VAT kutoka kiwango cha sasa cha TZS 15 milioni kwa mwaka hadi kiwango cha mauzo ya TZS 30 milioni kwa mwaka.

SHERIA YA MAMLAKA YA MAFUNZO YA AMALI

Kurekebisha Sheria ya Mamlaka ya Mafunzo ya Amali

Mgawanyo wa mapato yatokanayo na kodi ya ufundi stadi (SDL)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kabla, kuwa hakuna nchi inayoweza kuendelea bila ya watu wake kuelimika vya kutosha. Katika maendeleo, elimu ya juu na ile ya mafunzo ya amali ina nafasi maalum. Hata hivyo, elimu hizi zina gharama kubwa katika upatikanaji wake.

Mheshimiwa Spika, kwa dhamira ya kusaidia katika ugharamiaji wa elimu ya juu na mafunzo ya amali nchini, Serikali ilianzisha Ushuru wa Kuendeleza Ujuzi. Katika utekelezaji wa hilo, mahitaji ya fedha kwa kuhudumia maeneo haya mawili ya elimu nchini yamekuwa yakiongezeka kwa kasi mwaka hadi mwaka. Ili kuondoa utata uliojitokeza kuhusiana na matumizi ya Ushuru wa Kuongeza Ujuzi (SDL), Serikali itaweka utaratibu bayana wa mgao wa fedha hizo baina ya mafunzo ya amali na elimu ya juu. Inapendekezwa kurekebisha Sheria ya Mamlaka ya Mafunzo ya Amali ili asilimia 60 ya ushuru huo itumike kwa ajili ya Elimu ya Juu na asilimia 40 iliyobaki kwa Mafunzo ya Amali. Mgao huu utasaidia sana kwa maeneo yote mawili kufaidika.

Kusamehe Serikali kulipa Ushuru wa Mafunzo ya Amali

Mheshimiwa Spika, kumejitokeza pia tatizo la kuhasibu mara mbili malipo ya Serikali katika Ushuru wa Kuongeza Ujuzi. Kwa hali ilivyo sasa, Serikali inapokea ushuru huo kutoka kwa sekta binafsi na pia kujilipa pale inapochangia. Ili kurekebisha kasoro hii, inapendekezwa kurekebisha Sheria ya Mamlaka ya Mafunzo ya Amali kwa kutoa msamaha kwa Serikali na Taasisi zinazotegemea fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali. Hata hivyo, ili kutoathiri mapato yaliyokusudiwa kwa dhamira hii, Serikali itakuwa inatenga kiasi kisichopungua asilimia tatu na kisichozidi asilimia tano ya matumizi yake ya mishahara kwa madhumuni ya elimu ya juu na mafunzo ya amali.

SHERIA YA KAZI

Kupanga kiwango cha chini cha kutozea kodi ya PAYE kwa wataalamu wa kigeni

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Uwekezaji imetoa ruhusa kwa Wawekezaji kuajiri wageni kujaza nafasi nyeti ambazo utaalamu au ujuzi wake ni adimu kupatikana nchini. Kwa bahati mbaya, fursa hii imekuwa ikitumiwa vibaya na Wawekezaji karibu wote kwa kutoa taarifa ya kiwango ambacho ni cha chini cha mshahara wanacholipa wafanyakazi hao wageni. Matokeo ya taarifa hizo ni kuikosesha Serikali mapato yake halali. Hali hii haiwezi kuvumiliwa tena. Ili kudhibiti udanganyifu huo, Serikali kupitia Kanuni za Sheria ya Kazi Namba 3 ya Mwaka 2011 iliweka viwango vya chini vinavyokubalika kama mshahara kwa Wataalam hao wageni ambacho ni baina USD 500 mpaka USD 1,300 kwa mwezi kutegemea na nafasi ya ajira. Imebainika kwamba bado wawekezaji hutumia viwango hivyo vya chini kama ndio viwango halisi vya mishahara kwa wafanyakazi wao hata wale wa nafasi za juu.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kupitia Mamlaka ya Uwekezaji (ZIPA), Idara ya Kazi, Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato (TRA) inatarajia kuvipitia upya viwango hivyo na kuvirekebisha ili (1) kukabiliana na udanganyifu uliopo; (2) kuhakikisha kuwa wataalam wageni wanalipa kodi kulingana na kipato chao na (3) kuhakikisha kuwa ajira zisizo na ulazima wa kuajiriwa wageni zinabaki kwa wananchi wetu.

SHERIA YA ZIPA

Kupunguza misamaha ya kodi ya mapato (Tax Holiday) kwa miradi ya kibiashara.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa vivutio mbali mbali vya kodi na visivyo vya kodi ili kushajiisha uwekezaji nchini. Vivutio hivyo vinagusa maeneo ya uwekezaji kwa ujumla hasa mahoteli na vivutio maalum kwa maeneo huru ya uwekezaji ikiwemo miradi ya viwanda na shughuli za kibiashara. Serikali tayari imechukua juhudi kubwa za kuimarisha Miundombinu ikiwemo mfumo wa barabara, huduma za umeme na maji katika maeneo mengi ya uwekezaji. Serikali katika mwaka ujao wa fedha itafanya mapitio ya vivutio vilivyopo ili kuvirekebisha kwa kuondoa visivyohitajika tena na kuangalia haja ya kuweka vivutio vipya katika maeneo maalum kama vile miradi mikubwa na nyeti.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia imekusudia kuongeza vivutio zaidi katika uwekezaji wa maeneo makhsusi ya kiuchumi kama vile viwanda na ya kijiografia ikiwemo kushajiisha uwekezaji katika kisiwa cha Pemba. Kwa kuanzia, Serikali itaondoa Msamaha wa Kodi ya Mapato (Tax Holiday) kwa miradi mipya ya kibiashara (trading activities) katika Maeneo Huru ya Uwekezaji na Bandari Huru. Ili kutokuathiri taswira ya Serikali kwa Wawekezaji waliokwishawekeza, hatua hii haitahusisha Miradi ambayo imeidhinishwa na ipo nchini tayari.

SHERIA YA USIMAMIZI WA KODI



Kurekebisha Sheria ya Usimamizi wa Kodi (Tax Administration Procedure Act) ya mwaka 2009

Mheshimiwa Spika, baadhi ya Miradi ya hoteli iliyosajiliwa chini ya Sheria ya ZIPA na kupata msamaha wa kodi wakati wa ujenzi, imebainika kuwa baada ya kukamilika hukodishwa kwa kampuni nyengine kwa uendeshaji bila ya dhima maalum kwa malipo mbali mbali ikiwemo mapato ya Serikali. Hatua zitachukuliwa kurekebisha upungufu huu. Inapendekezwa kurekebisha Sheria ya Usimamizi wa Kodi (Tax Administration Procedure Act) ya mwaka 2009 ili iwapo mwekezaji atakodisha ama kuteua Kampuni ya kuendesha Hoteli yake, dhamana ya masuala yote ya mapato ya Serikali itabaki kwa mmiliki wa hoteli husika. Endapo deni la kodi halikulipwa na kampuni iliokodishwa au kukabidhiwa uendeshaji, dhamana au dhima hiyo itaweza kulipwa kwa dhamana ya hoteli yenyewe.

SHERIA YA MITAJI YA UMMA



Kuasisi utaratibu wa Mashirika ya Serikali kulipa gawio kutokana na Faida

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu hakujawa na utaratibu maalum kwa Mashirika ya Serikali kuchangia katika bajeti ya Serikali tokea kusitishwa utaratibu wa zamani uliokuwa ukiyataka Mashirika kuchangia bajeti ya Serikali bila ya kujali kuwa yanapata faida au la. Kuanzia mwaka ujao wa fedha, Mashirika ya Serikali yatapaswa kulipa gawio kutokana na faida (dividend) inayopatikana baada ya kulipa kodi husika katika biashara zao. Hatua hiyo itaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha TZS 2.7 bilioni.

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, hatua zote hizi zinatarajiwa kuimarisha ufanisi katika usimamizi wa mapato na kuiingizia Serikali TZS 13.3 bilioni.

SURA YA BAJETI BAADA YA MAREKEBISHO

Mheshimiwa Spika, baada ya marekebisho yote hayo, katika mwaka ujao wa fedha Serikali inakadiria kukusanya jumla ya TZS 294.1 bilioni kutokana na vyanzo vya ndani sawa na asilimia 21.3 ya Pato la Taifa. Ikilinganishwa na matarajio ya makusanyo ya TZS 217.1 bilioni hadi mwisho wa Juni 2012, kunajitokeza ongezeko la TZS 77.0 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 35.5. Kati ya mapato hayo, jumla ya TZS 274.1 bilioni zitatokana na makusanyo ya vyanzo vya kodi na TZS 20.0 bilioni ni mapato yasiyo ya kodi. Kati ya mapato yasiyokuwa ya kodi, TZS 1.0 bilioni ni gawio kutoka Benki Kuu, TZS 2.7 bilioni ni gawio la faida kutoka Mashirika ya Serikali na mapato ya Wizara za Serikali ni TZS 16.3 bilioni.

Mheshimiwa Spika, kati ya TZS 274.1 bilioni zitakazotokana na kodi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inakadiriwa kukusanya TZS 106.7 bilioni, Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) inatarajiwa kukusanya TZS 146.0 bilioni na TZS 21.4 bilioni zitakusanywa na Mhasibu Mkuu wa Serikali kama Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi wa SMT waliopo Zanzibar.

MAPATO YA NJE



Ruzuku na Mikopo ya Nje

Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2012/13 inatarajia kupata jumla ya TZS 293.2 bilioni kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kupitia programu na miradi mbali mbali. Kati ya hizo, TZS 187.8 bilioni ni mikopo na TZS 105.4 bilioni ni ruzuku. Aidha, misaada ya kibajeti (GBS) inatarajiwa kufikia TZS 38.1 bilioni ikiwa ni asilimia 4.5 ya misaada yote ya kibajeti itakayotolewa Tanzania katika mwaka 2012/13. Kati ya fedha hizo, TZS 28.3 bilioni ni ruzuku na TZS 9.8 bilioni ni mikopo ya kibajeti. Aidha, Serikali itatumia TZS 1.9 bilioni ikiwa ni fedha kutokana na misamaha ya madeni (MDRI).

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kiwango cha matumizi, na mchanganuo wa mapato kutokana na vyanzo vyake, utegemezi wa bajeti kutoka kwa Washirika wa Maendeleo umeendelea kupungua hadi kufikia asilimia 21 mwaka 2012/13 kutoka asilimia 24 mwaka 2011/12 sawa na kupungua kutoka asilimia 12 ya Pato la Taifa mwaka 2011/12 hadi kufikia asilimia 9 katika mwaka wa fedha wa 2012/13.

MATUMIZI YA SERIKALI

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13, Serikali inatarajia kutumia TZS 307.8 bilioni sawa na asilimia 47.4 kwa ajili ya kazi za kawaida na TZS 341.1 bilioni sawa na asilimia 52.6 kwa kazi za maendeleo na hivyo kufanya jumla ya matumizi kuwa TZS 648.9 bilioni.

Mambo Muhimu yanayozingatiwa katika ugawaji wa fedha za Matumizi

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, kati ya mapato yote yanayotarajiwa, kuna mapato ambayo huelekezwa katika matumizi maalum kabla ya kuwa na kiwango kinachogawiwa kwa Taasisi za Serikali kwa ajili ya matumizi mengineyo ya kazi za kawaida. Kwa mwaka 2012/13, kati ya mapato yote yanayotarajiwa ya TZS 648.9 bilioni, TZS 293.2 bilioni ni kwa ajili ya utekelezaji wa program na miradi ya maendeleo kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Aidha, mapato yote ya TZS 40 bilioni kutokana na Misaada ya Kibajeti na MDRI yanaelekezwa katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, tunafahamu kuwa kuna matumizi ya lazima kwa Serikali kama vile maslahi ya wafanyakazi wa sasa na waliostaafu (mishahara, kiinua mgongo na pencheni) na malipo ya deni la umma na riba yake. Kwa mwaka ujao wa fedha, matumizi ya lazima kwa kazi za kawaida yanatarajiwa kufikia TZS 200.6 bilioni. Aidha, matumizi ya TZS 2.7 bilioni yametengwa kwa matumizi maalum kama nilivyoeleza awali, ikiwemo TZS 2.0 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa madawati ya skuli na TZS 0.7 bilioni zitatumika kwa ajili ya kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira, ambapo kati ya hizo TZS 0.56 bilioni zitatumika kwa ajili ya ziada ya ununuzi wa dawa na TZS 0.14 bilioni ni kwa ajili ya upandaji miti.

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa matumizi yaliyoelezwa, tunabakiwa na TZS 112.4 bilioni. Kati ya bakaa hiyo, inayoweza kugawiwa kwa matumizi ya kazi za maendeleo ni TZS 7.9 bilioni na TZS 104.5 bilioni kwa ajili ya kazi za kawaida ikiwemo matumizi mengineyo ya Mfuko Mkuu wa Serikali. Kati ya fedha hizo zinazoweza kugawiwa kwa kazi za kawaida, TZS 2.3 bilioni zimepangwa kwa ajili ununuzi wa pembejeo za kilimo. Aidha, Serikali imepanga pia kununua vifaa maalum kwa kusaidia makundi mbali mbali ya Watu Wenye Ulemavu kama vile viti vya magurudumu, visaidizi vya kusikia kwa walemavu wa masikio na fimbo za kutembelea kwa wasioona. Kwa kuanzia, Serikali imepanga kutumia TZS 0.3 bilioni kwa kusaidia wenzetu wenye ulemavu katika mwaka ujao wa fedha. Bakaa iliyobaki ya TZS 101.9 bilioni ni kwa ajili ya maeneo mengine ya matumizi mengineyo.

Mheshimiwa Spika, ahadi ya Serikali ni kuongeza maslahi ya wafanyakazi wake kila hali ya uchumi itaporuhusu. Serikali inaelewa kuwa kipato cha wafanyakazi wake walio wengi hakilingani na mahitaji yao ya maisha. Baada ya marekebisho makubwa ya mshahara yaliyofanywa mwezi Oktoba 2011, Serikali haikusudii kupandisha kima cha chini cha mshahara mwaka ujao wa fedha. Badala yake, imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha marekebisho kulingana na mahitaji ya muundo wa utumishi (Scheme of Service), nyongeza za mwaka, ajira mpya za lazima na upandishaji vyeo kwa watumishi wa Umma.

Mheshimiwa Spika, sura halisi ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/13 ni kama inavyoonekana katika jadweli liliopo hapo chini.



Mfumo wa Bajeti ya mwaka 2012/13



Maelezo Makisio Makisio Ongezeko (%) 2011/12



(TZS Bil.) 2012/13

(TZS Bil.) Mapato Mapato ya ndani 221.24 294.1 32.9 4.5% Msaada wa kibajeti (GBS) 30.28 39.9 32.1 Dhamana za Hazina na Hati Fungani 15.00 15.8 5.5 Mikopo ya Kibenki 1.60 0.0 -100.0 Bakaa iliyoletwa 4.00 5.9 46.7 Mikopo na Ruzuku 340.96 293.2 -14.0 Jumla ya Mapato 613.08 648.9 5.9 Matumizi G. Matumizi ya Kawaida 234.18 307.8 31.4 Mishahara (Mawizara) 105.78 139.6 32.0 Mishahara (ruzuku) 20.56 17.7 -13.4 Matumizi mengineyo (Mawizara) 47.17 71.1 50.3 Matumizi mengineyo (ruzuku) 13.05 26.6 103.9 Mfuko Mkuu wa Serikali (CFS) 47.62 52.8 10.9 H. MAENDELEO 378.90 341.1 -10.0 Mchango wa Serikali 37.95 47.9 26.3 Washirika wa Maendeleo 340.96 293.2 -14.0 Jumla ya Matumizi 613.08 648.9 5.9 Chanzo: Ofisi ya Rais - Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo

MAMBO MUHIMU MWAKA 2012/13



Sensa ya Watu na Makaazi

Mheshimiwa Spika, mipango yote tutayoipanga na kuidhinishwa na Baraza lako tukufu inalenga katika kuwaletea maisha bora wananchi wenzetu. Kama ilivyo nchi yoyote, jamii yetu inaundwa na makundi mbalimbali yakiwemo kina mama, vijana, watoto na wazee. Kwa ujumla wake, makundi ya rika na jinsia mbalimbali ndio yanaunda idadi ya watu katika nchi yetu. Makundi yote haya yana mahitaji maalum, hivyo ni muhimu kujua, sio tu idadi halisi ya watu bali pia mgawanyo wake kwa makundi na kijiografia.

Mheshimiwa Spika, njia inayotumika kupata taarifa hizo muhimu ni kupitia Sensa ya Watu na Makaazi, ambayo nchini kwetu hufanyika kila baada ya miaka kumi. Sensa ya mwisho ilifanyika mwaka 2002 na hivyo tayari tumetimiza kipindi cha miaka kumi. Kwa kutambua umuhimu wa kujua idadi ya watu nchini, tayari Serikali imeandaa Sensa nyengine ambayo imepangwa kufanyika tarehe 26 Agosti mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa tunashiriki kikamilifu katika Sensa hiyo na kuhimiza wengine ili wakaazi wote wa Zanzibar wahesabiwe. Kufanya hivyo kutarahisisha mipango ya kuwaletea maendeleo kwa mujibu wa mahitaji. Wito wangu ni kuwa ifikapo tarehe 26 Agosti mwaka huu kusiwe na mkaazi yeyote wa Zanzibar ambae hatahesabiwa, mara moja tu, kipindi cha Sensa. Ni jukumu letu viongozi, wakuu wa kaya na wananchi kuhakikisha lengo hili linatimia.

ii. Uandaaji wa Katiba Mpya ya Jahmuri ya Muungano wa Tanzania

Mheshimiwa Spika, nchi yetu imepitia vipindi mbalimbali vya demokrasia na mageuzi yake. Leo hii tunajivunia mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kufanya maamuzi kwa njia ya kidemokrasia, kwa kudumisha umoja wetu, na kwa uvumilivu wa mawazo yanayotofautiana na ya mmoja wetu. Kwa mara nyengine tena, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekabiliwa na mtihani mwengine muhimu na adimu katika ujenzi wa demokrasia yake. Mtihani huu ni mchakato wa uandaaji wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu kuwa Katiba ndio Sheria kuu ya nchi; sote tunafahamu kuwa Katiba ndio mkataba wa wananchi kwa viongozi wao na hivyo sote tuufahamu umuhimu wa Katiba. Haijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu, wananchi kupata fursa ya kushiriki moja kwa moja katika uandaaji wa Katiba wanayoitaka. Fursa iliyopo mbele yetu ni adimu na tunapaswa kuitumia vyema. Haiwezekani kuwa wananchi wote tuna mawazo yanayofanana juu ya mustakabali wa nchi yetu. Tabaan mawazo yetu lazima yatatofautiana katika mambo mengi ya Katiba hii. Sehemu muhimu ya demokrasia ni kustahamiliana pale tunapotafautiana kimawazo na kifikra.

Mheshimiwa Spika, katika kuwa na fikra tafauti juu ya Muundo wa Muungano wetu, wapo wanaotaka Muundo wa Muungano uendelee na wapo wanaotaka marekebisho katika muundo wa sasa. Wote hawa wana haki na mawazo yao. Lakini ni dhahiri kuwa haiyumkiniki Katiba ikabeba mtazamo zaidi ya mmoja. Kinachotarajiwa ni kuwa Katiba ibebe na kukidhi matakwa ya wananchi walio wengi kwa kuzingatia masuala yetu ya kiuchumi, kijamii, kihistoria na kijiografia.

Mheshimiwa Spika, tofauti hizo za mitazamo na kutokubaliwa mtazamo aupendao mmoja wetu au kikundi miongoni mwetu hazipaswi kuwa chanzo cha vurugu, kuvunjika kwa amani au kupotezwa kwa fursa yenyewe ya kuandaliwa Katiba mpya. Kwa mara nyengine tena, Serikali inatoa wito kwa Wazanzibari wote tudumishe mila na desturi zetu za upole, ustaarabu na uvumilivu wa kisiasa, kidini na kijamii ambao Zanzibar imenasibishwa nao kwa karne nyingi. La muhimu kwa upande wetu Wazanzibari ni kuhakikisha kuwa tunajitokeza kwa wingi na tunashiriki kikamilifu katika kutoa maoni yetu kwa kujenga hoja na bila ya jazba hadi kupatikana kwa Katiba tunayoitaka. Tayari Tume ya kukusanya maoni imeshaundwa na inajumuisha wajumbe kutoka pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano. Nachukua fursa hii kumshukuru sana Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar kwa kuwateua wajumbe ambao ni weledi kitaaluma na wenye uzoefu na maadili ya kupenda nchi yao. Ni imani yangu kuwa watakuwa nguzo kuu ya kupata maoni.

SHUKRANI
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kukupongeza wewe binafsi kwa umahiri wako wa kuliendesha Baraza hili katika hali ya amani na utulivu. Ni matumaini yangu kwamba busara na hekima zako zitaendelea kuongoza vyema majadiliano ya vikao vya Baraza hili. Aidha, kwa kupitia kwako napenda kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Baraza, Mheshimiwa Hamza Hassan Juma, Waheshimiwa Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Baraza lako na Waheshimiwa wajumbe wote wa Baraza kwa mashauriano, maoni na miongozo katika mchakato mzima wa maandalizi ya bajeti ninayoiwasilisha mbele ya Baraza lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, maandalizi ya bajeti hii yamehusisha wadau wengi wa ndani na nje ya Serikali. Napenda kuwashukuru wote waliochangia kwa kutoa maoni ambao ni pamoja na Watendaji Wakuu na wafanyakazi wa Wizara mbali mbali, Idara zinazojitegemea, Mikoa, Halmashauri za Wilaya, Manispaa, Asasi zisizo za Kiserikali pamoja na Sekta Binafsi. Michango yao ilisaidia sana katika kufanikisha utayarishaji wa bajeti hii. Aidha, napenda kuwashukuru watendaji wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha miswada na nyaraka mbali mbali za sheria ambazo ni sehemu ya bajeti hii.

Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Ofisi ya Rais – Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, napenda kutoa shukurani za pekee kwa Katibu Mkuu ndugu Khamis Mussa Omar, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Bi Amina Khamis Shaaban na Naibu Katibu Mkuu, Ndugu Abdi Khamis Faki. Aidha, napenda kuwashukuru Wakuu wa Idara na wafanyakazi wote wa Ofisi ya Rais - Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha na hatimae leo hii kuiwasilisha hotuba hii.

Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii adhimu kuwashukuru kwa dhati kabisa Washirika wetu wa Maendeleo katika kuchangia maendeleo ya nchi na wananchi wetu. Kwa hakika misaada yao imekuwa ni kichocheo kikubwa cha harakati za maendeleo nchini kwetu. Washirika wa Maendeleo waliochangia bajeti ya mwaka 2012/13 ni pamoja na Canada, Cuba, Denmark, Finland, India, Ireland, Jamhuri ya Watu wa China, Jamhuri ya Watu wa Korea, Japani, Marekani, Misri, Norway, Oman, Sweden, Ubelgiji, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani na Uturuki.

Mheshimiwa Spika, mashirika ya kimataifa yaliyojitokeza kuchangia katika bajeti yetu ya mwaka 2012/13 ni ACBF, ACCRA, AfDB, AGRA, BADEA, CARE INTERNATIONAL, CDC, CHAI, CIDA, DANIDA, DFID, EGH, EU, EXIM Bank of China, EXIM Bank of Korea, FAO, FHI, GAVI, GEF, GLOBAL FUND, IAEA, ICAP, IDB, IFAD, ILO, IMF, IPEC, JICA, JSDF, KOICA, MCC, NORAD, OPEC, ORIO-Netherlands, PRAP, SAUDI FUND, Save the Children, SIDA, UN AIDS, UN, UNDP, UNESCO, UNFPA, UN-HABITAT, UNICEF, UNIDO, USAID, WB, WHO na WSPA .

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2020, MKUZA II na Malengo ya Milenia ya 2015. Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/13, kama ilivyo kwa miaka mingine, imeandaliwa kwa kuzingatia malengo ya Mipango na Mikakati hiyo mikuu.

Mheshimiwa Spika, taswira inayojitokeza ni kuwa pamoja na jitihada zinazochukuliwa za kuongeza mapato ya ndani, bado mahitaji yetu ya kuleta maendeleo kwa haraka yanapindukia sana uwezo wetu wa kuyahudumia. Kutokana na hali hiyo, Taasisi zote za Serikali zinalazimika kuwa makini zaidi katika kubainisha na kuteua vipaumbele ili kukidhi gharama za utekelezaji wake kulingana na rasilimali zilizopo. Serikali itasisitiza udhibiti wa matumizi na kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa Maofisa Wahasibu wote.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, kwa heshima, taadhima na unyenyekevu naomba sasa Baraza lako tukufu lipokee, lijadili na hatimae lipitishe mapendekezo juu ya Mwelekeo wa Uchumi, Mpango wa Maendeleo na Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2012/13, ili yawe muongozo wa utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa mwaka 2012/13.

Mheshimiwa Spika, Serikali inapendekeza mbele ya Baraza lako tukufu kwa mwaka wa fedha 2012/13 kukusanya jumla ya shilingi bilioni mia sita na arobaini na nane na mia tisa na arobaini na nne milioni (TZS 648,944 milioni) pamoja na matumizi ya shilingi bilioni mia tatu na saba na mia saba tisini na saba milioni (307,797 milioni) kwa kazi za kawaida na shilingi bilioni mia tatu na arobaini na moja na mia moja na arobaini na saba milioni (341,147milioni) kwa kazi za maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa hoja.
13 Juni, 2012

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.