UONGOZI wa klabu ya Azam FC, umesema madai ya Simba kuwa imekamilisha usajili wa mchezaji Ibrahim Rajab 'Jeba' anayekichezea kikosi cha 'U-20' cha Azam, ni kujidanganya.
Wakati kinda huyo alionekana jana asubuhi kwenye mazoezi ya viungo (gym) ya Simba maeneo ya Chang'ombe, uongozi wa Azam FC umesema nyota huyo ni miongoni mwa wachezaji walisoajiliwa na matajiri hao, ambapo msimu uliopita, walimpeleka Villa Squad kwa mkopo ili ajifue zaidi.
Meneja wa Azam FC Patrick Kahemele, amekiita kitendo cha Simba kudai kuwa imefanya uhamisho wa mchezaji huyo kuwa ni uhuni, kwani bado ana mkataba na klabu hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini Salim Said Bakhresa.
"Jeba ni mchezaji wetu halali na bado tuna mkataba naye. Ikumbukwe kuwa Ibrahim Jeba alisaini mkataba wa kuichezea Azam kwa miaka miwili mwezi Desemba 2011 na akachukua fedha kama ada ya usajili, na baadae akapelekwa Villa Squad kwa mkopo ili apate nafasi ya kujifua ili msimu huu arudi Azam FC", alisema Meneja huyo.
Alieleza kuwa Azam ilifahamu kuwa Simba imemrubuni Jeba asicheze Villa, na kwa kuwa kijana huyo bado mdogo ilikuwa rahisi kumrubuni, na kuongeza kuwa Azam haikutaka malumbano kwa vile ina mkataba uliosajiliwa na TFF, ambayo alidai kuwa iliwahakikishia kuwa haki za timu hiyo zitalindwa.
Kahemele alisema hakuna njia yoyote ya kumalizana na timu yake ili kumtwaa kinda huyo, kwani Azam ilishatangaza mapema kwamba hakuna mchezaji yeyote aliyeachwa au anayeuzwa msimu ujao.
Hata hivyo, alisema kama Simba wanamtaka mchezaji huyo kihalali, itabidi igharamike sana kwani Azam inamuona Jeba kuwa ana thamani ya shilingi milioni 50, na ili Simba impate, itabidi iwatoe Jonas Mkude na Shomari Kapombe kwa Azam ili kumtia mikononi kinda huyo kutoka Zanzibar.
Wachezaji waliomo kwenye orodha ya Azam FC kwa ajili ya msimu ujao, ni Mwadini Ali, Deo Munishi 'Dida' Aishi Salum na Jackson Wandwi (magolikipa), Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Samih Haji,Luckson Kakolaki, Said Moradi, Joseph Owino na Aggrey Morris.
Wengine ni Kipre Bolou, Abdulhalim Humoud, Himid Mao, Salum Abubakar, Abdi Kassim, Ramadhani Chombo, Abdulghani Ghulam, Ibrahim Rajab 'Jeba', Jabir Aziz 'Stima', Ibrahim Joel Mwaipopo, Kipre Tchetche, Mrisho Ngasa, Zahoro Pazi, Khamis Mcha, George Odhiambo 'Blackberry', Gaudence Mwaikimba na John Bocco 'Adebayor'.
No comments:
Post a Comment