Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
HUKU michuano ya kuwania Kombe la Kagame ikisogezwa mbele hadi Juni 27, mabingwa watetezi klabu ya Yanga, wanatarajia kutangaza jina la kocha mpya atakayechukua mikoba ya Kostadin Papic aliyemaliza mkataba wake wiki kadhaa zilizopita.
Aidha, imefahamika kuwa, kikosi cha timu hiyo kinatarajia kuanza kambi Juni 14, kujiweka sawa kwa ajili ya kutetea taji lao katika mashindano hayo yaliyopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam kama yale ya mwaka jana.
Yanga ilitwaa ubingwa huo kwenye mashindano ya mwaka 2011, na inajiandaa huku viongozi na wanachama wake wakijaribu kumaliza mgogoro wa uongozi ambao nusura uisambaratishe timu hiyo kongwe nchini.
Katibu Mkuu wa Yanga Celestine Mwesigwa, amekaririwa akisema kuwa, kama kila kitu kitakwenda kwa mujibu wa vile kinavyopangwa, jina la kocha huyo litawekwa hadharani kesho, siku tisa kabla kikosi cha timu hiyo kujichimbia kambini.
“Yatakuwa mashindano magumu. Mgogoro ulioibuka katika kipindi cha karibuni, unaongeza ugumu wa mashindano hayo kwetu, lakini tuna imani tutashinda na ninaamini tutafikia lengo na kuweza kujipanga upya baada ya matokeo mabaya katika Ligi Kuu ya Vodacom msimu uliomalizika”, alisema Mwesigwa.
Michuano ya mwaka huu, inatarajiwa kushirikisha timu 12 kutoka nchi za Sudan, Eritrea, Uganda, Rwanda, Kenya, Djibouti, Ethiopia, Zanzibar, Somalia, Burundi na wenyeji Tanzania Bara ambao mbali na Yanga, pia itawakilishwa na mabingwa wapya wa Ligi Kuu Simba, na washindi wa pili Azam FC.
Nayo Azam FC, imepanga kuingia kambini jijini Dar es Salaam Ijumaa wiki hii, kujifua kwa ajili ya michuano yake hiyo ya kwanza ya kimataifa tangu ilipoasisiwa miaka kadhaa iliyopita.
Ofisa Habari wa timu hiyo Jaffar Idi Maganga, amesema tayari Azam imemtia mikononi mshambuliaji wa zamani wa Sofapaka ya Kenya George Odhiambo 'Blackberry', aliyesaini mkataba wa miaka miwili na matajiri hao.
“Hatutaki kushiriki, bali kujaribu kwa uwezo wetu wote kutwaa ubingwa wa Kagame katika mwaka wetu wa kwanza kushiriki mashindano hayo”, alisisitiza Maganga.
Mabingwa wa Tanzania Bara Simba, wamekuwa katika mazoezi ya nje ya kambi jijini Dar es Salaam tangu mwanzoni, ikiwakosa baadhi ya nyota wake waliokwenda Ivory Coast na timu ya Taifa Stars kwa mchezo wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 dhidi ya 'The Elephants'
No comments:
Post a Comment