Na Haji Nassor, Pemba
TIMU ya skuli ya Wingwi Sekondari, imefanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Mazingira baada ya kuivuruga bila huruma skuli ya Mchanga Mdogo Sekondari kwa magoli 7-1 kwenye mchezo wa nusu fainali uliofanyika uwanja wa Gombani Pemba.
Nyota ya ushindi kwa timu hiyo ilianza kuonekana mapema pale mchezaji Mohamed Ali alipoandika bao la kwanza mnamo dakika ya saba kabla Suleiman Salim kuongeza la pili dakika tatu baadae.
Magoli mengine ya Wingwi Sekondari, yalifungwa na Seif Mohamed (matatu), Juma Mbarouk na Mohamed Ali tena, huku goli la kujiliwaza kwa Mchanga Mdogo likifungwa na mchezaji Iddi Mbarouk kwa njia ya penelti mnamo dakika ya 70.
Mwamuzi wa pambano hilo Hassan Gerie, alimtoa nje mchezaji Hamad Said wa Wingwi kwa kadi nyekundu, kutokana na mchezo mbaya.
Kwa matokeo hayo, Wingwi inasubiri mshindi wa mchezo mwengine wa nusu fainali uliotarajiwa kuchezwa jana kati ya Skuli ya Vikunguni na Uweleni.
No comments:
Post a Comment