Habari za Punde

Kituo cha Kurushia Matangazo ya Masafa Mafupi Dole Chakarabatiwa

Na Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar 

 Serikali ya watu wa Jamhuri ya China imekabidhi mradi wa matengenezo ya masafa mafupi ya kituo cha Dole kwa ajili ya Shirika la Utangazaji Zanzibar(ZBC). 

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo, Dk. Ali Mwinyikai alisema mradi huo ulioanza mwaka 2011 umekamilika baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa katika Kituo cha kurushia matangazo ya masafa mafupi kilichopo Dole nje kidogo ya Manispaa ya Zanzibar.


 “Mradi huu ulianza mwezi Septemba mwaka jana Kampuni ya China Shaanxi ndiyo iliyofanya ukarabati wa kituo hicho ambacho sasa kimerejea katika hali ya kawaida kuongeza usikivu zaidi wa masafa mafupi kwa ajili ya ZBC Radio” Alisema Dk. Mwinyikai. 

 Katibu Mkuu huyo alisema kwamba baada ya ukarabati huo, kituo cha Dole kitaweza kuingia kutoa mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi wa matangazo ya ZBC. 

 Mwakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Ghang Ghiring alisema China itawajibika katika kipindi cha mwaka mmoja kufanyia matengenezo madogo madogo baada ya makubaliano ya pande zote mbili kuamua kukabidhi mradi huo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar baada ya kukamilika.

 Makabidhiano ya Mradi huo yamefanyika jana Ofisini kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo,Kikwajuni Zanzibar. 

 Wakati huo huo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ile ya Watu wa Jamhuri ya China jana zimetiliana saini mkataba wa mradi wa ukarabati wa kituo cha kurushia matangazo cha Shirika la Utangazaji Zanzibar kilichopo Langoni Zanzibar.

 Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Mwinyikai alisema, mkataba huo ni nyongeza ya mkataba wa awali uliotiwa saini mwaka 2009 kuhusu ukarabati wa kituo hicho. 

Gharama za mradi huo ni pesa za China RMB 784,800. Katika hafla ya utiaji saini nyongeza ya mkataba wa awali, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa china iliwakilishwa na Afisa Ubalozi katika Ubalozi mdogo Zanzibar anayeshughulikia Uchumi na Biashara,Liu Xiao Hang.

 Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ni mshirika mkubwa wa maendeleo kwa Zanzibar tangu mapinduzi ya Januari 12,1964 na ni miongoni mwa nchi za mwanzo kuyatambua mapinduzi yaliyoongozwa na Chama cha Afro Shiraz(ASP)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.