TAARIFA
YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS MHESHIMIWA FATMA A FEREJI
KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI TAREHE 05 JUNI 2012
Ndugu
wananchi,
Kwanza
kabisa napenda kuchukua fursa hii adhimu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kutufikisha tena katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka huu
wa 2012. Kwa kuwakumbusha ni kwamba tarehe 5 Juni ya kila mwaka ni Siku ya Mazingira
Duniani. Siku hii imeanzishwa na Umoja
wa Mataifa mwaka wa 1972 Jijini Stockholm nchini Sweden kwa lengo la
kuwakumbusha wananchi na Serikali za mataifa mbalimbali kutafakari suala zima
la maendeleo yao kwa kuzingatia mazingira. Maudhui haya yameonekana kuwa ni ya lazima baada
ya kuwepo kwa uharibifu wa mazingira ulitokana na harakati za kujitafutia maendeleo
hasa kwa Mataifa tajiri duniani. Harakati
hizo ni pamoja na shughuli za kilimo, viwanda, ujenzi, usafiri na usafirishaji,
uchimbaji wa madini, biashara, n.k. Zanzibar
ni sehemu ya Dunia, hivyo hatuna budi kuungana na nchi nyengine duniani
kuadhimisha siku hii muhimu katika mustakbali wa maisha yetu na vizazi vijavyo.
Ndugu
wananchi,
Mazingira
ya visiwa vyetu katika hali yake ya asili kimsingi yalikuwa ni mazuri yenye
fukwe zenye kupendeza, bahari iliyosheheni rasilimali za aina mbalimbali,
udongo wenye rutuba, miti na wanyama wa aina tofauti. Mambo yote hayo yametuwezesha kufikia kwenye maendeleo
tuliyonayo. Hata hivyo hali hiyo hivi
sasa imeshaanza kubadilika na changamoto za aina mbalimbali za kimazingira
zimeshaanza kujitokeza na kuwa tishio kwa mustakabali wa maendeleo endelevu ya
Zanzibar. Miongoni mwa changamoto hizo ambazo
zinasababishwa na mikono yetu ni:-
·
Ukataji ovyo wa miti ya misitu, matunda
na mikoko.
·
Ujezi holela na usiokuwa na mpango hasa
karibu na vyanzo vya maji.
·
Utupaji ovyo wa taka za majumbani,
mahotelini na sehemu za biashara.
·
Uingizaji wa bidhaa chakavu hasa za umeme
na elektroniki (e-waste) kutoka nchi za nje.
·
Uchimbaji usio wa mpangilio wa mchanga,
kifusi, udongo na mawe.
·
Kuendelea kutumiwa kwa mifuko ya
plastiki.
·
Kuendelea kwa uvuvi haramu katika maeneo
mbalimbali ya visiwa vyetu unaoharibu matumbawe na kuvua samaki wachanga.
·
Umwagaji ovyo wa maji machafu kutoka
majumbani, viwandani, na mahotelini.
Ndugu
wananchi,
Uvunaji
wa maliasili zinazotuzunguuka pamoja uendelezaji wa shughuli mbalimbali za
kimaendeleo ni suala la lazima kwa binaadamu yeyote ili aweze kuishi. Hata hivyo, pasipokuwa na tahadhari na utaratibu
mzuri wa kuvuna maliasili hizo ndipo athari mbaya za uharibifu wa maliasili
hizo na mazingira hutokea. Miongoni mwa
sababu zinazopelekea kuwepo kwa changamoto za kimazingira nilizozitaja hapo juu
ni wadau mbalimbali kutokuzingatia na kufuata taratibu, kanuni na sheria ziliopo. Kwa mfano, sheria za uvuvi, misitu, ardhi, na
mazingira zinatoa muongozo mzuri wa matumizi bora ya Ardhi na endelevu ya
maliasili ziliopo katika visiwa vya Zanzibar na kuelekeza nini kifanyike ili
kuwa salama au kupunguza athari zilipo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Suala
la utunzaji na uhifadhi wa mazingira si suala la mtu au taasisi fulani peke
yake. Ni suala letu sote na linahitaji nguvu na juhudi za pamoja. Kwa sababu
tukiyaacha mazingira yetu yakaharibika kila mmoja ataathirika kwa namna moja au
nyengine. Dunia imeweka siku maalumu ya
mazingira ili kupeana nasaha za kuhifadhi na kulinda mazingira kufuatana na kauli
mbiu ya mwaka unaohusika.
Ndugu
wananchi,
KAULI
MBIU ya maadhimisho ya siku ya mazingira duniani kwa mwaka huu wa 2012 ni Uchumi
Endelevu: Je, unakuhusu wewe? (Green Economy: Does iyt include you?) Kauli hii ina maana pana sana na
kimsingi inahimiza Uchumi Endelevu wenye kujali uhifadhi wa mazingira na kutaka
kila mmoja wetu aweze kuhusika. Kwa ujumla Uchumi Endelevu au uchumi wa kijani ni ule
uchumi ambao unazingatia mambo matatu: uchumi, jamii na mazingira. Kwa maana Uchumuni endelevu ni uchumi ambao
unaongeza mapato na ustawi wa jamii sambamba na utunzaji na uhifadhi wa
mazingira. Kwenye Uchumi endelevu,
masuala ya ukuaji wa uchumi, jamii na mazingira ni mambo ambayo yanatakiwa yawe
yanakwenda kwa pamoja ili kuleta uwiano bila ya kuathiri kimoja wapo. Ni lazima uchumi endelevu au uchumi wa kijali uwe na uchafuzi mdogo wa
mazingira na uzalishaji mdogo wa hewa ukaa ambayo ndio chanzo kikubwa cha
kuongezeka la joto dunia.
Ndugu
Wananchi:
Kutokana
na maelezo hayo ni lazima tutafakari ni kwa kiasi gani harakati za kila mtu za
uzalishaji na kujitafutia riziki zinazingatia utunzaji na uhifadhi wa
Mazingira. Kutokana na matatizo ya
kimazingira yaliopo katika visiwa vyetu ni wazi kuwa ndani ya Zanzibar kuwa
idadi ndogo ya watu ambao wanajali utunzaji na uhifadhi wa mazingira katika
shughuli zao za kila siku za kujitafutia maisha. Jambo hili ni hatari hasa ukizingatia kuwa
Zanzibar ni visiwa vyenye maliasili chache sana ambazo zinahitajika kwa
maendeleo ya maisha ya vizazi vya leo na vijavyo.
Ndugu Wananchi
Hali
halisi ya kimazingira ilivyo hivi sasa katika visiwa vyetu ina lazimisha kila
mkaazi wa Zanzibar anze kuchukua hatua leo za kutunza na kuhifadhi Mazingira
ili kuwa na Uchumi endelevu kwa faida yetu sote. Hatua hizo ni pamoja na:
1. Kuacha
kujenga nyumba karibu na vyanzo vya maji na kwenye ardhi za Kilimo. Ni lazima tuzingatie kuwa hatuwezi kuwa na
Uchumi endelevu bila ya kuwa na maji ya kutosha na ardhi ya Kilimo iliyo bora
ambayo inazalishwa kwa wingi.
2. Kuacha
kutupa ovyo taka. Ni vyema turejeshe
utamaduni wetu wa kuhifadhi taka zenu, kufagia na kuweka maeneo yetu katika
hali ya Usafi ili tujilinde na maradhi mbalimbali ambayo yanaweza kuondoa uhai
wetu. Tukumbuke kuwa miji safi huongeza
Uchumi wa nchi kwa kuwa huwa ni kivutio cha wawekezaji mbalimbali.
3. Tuache
kuchimba ovyo mchanga kwani kufanya hivyo tunaongeza mashimo na mahandani na
hivyo kuondoa uimara wa visiwa vyetu. Kila
mmoja wetu anatakiwa ahakikishe kuwa anachukua mchanga katika sehemu
zilizotengwa kwa ajili hiyo.
4. Tuache
kuvua uvuvi harama na kuharibu maliasili za baharini. Tukumbuke kuwa sekta ya uvuvi ni mhimili
mkubwa wa Uchumi wa Zanzibar na ni sekta ambayo imeajiri idadi kubwa ya watu hapa
Zanzibar. Aidha samaki ndio chanzo
kikubwa cha maadini ya protein kwa watu wengi wa Zanzibar. Kuendelea kuvua uvuvi harama maana yake fursa
zote hizo tunaziondoa na hatimae tunakaribisha umasikini na utapia mlo.
5. Tuache
kukata ovyo miti. Kwa hakika shughuli
kama vile za Kilimo, ujenzi, uchimbaji wa mchanga, ukataji wa kuni, uchomaji wa
mkaa na chokaa ni mamabo ambayo yanapelekea kutoweka kwa Msitu uliokuwepo
Zanzibar. Kama kila mmoja wetu
hatochukua hatua zinaofaa basi viswa vyetu tunaweza kuvifanya jangwa. Aidha sote kwa pamoja tunatakiwa kuongeza
juhudi ya kupanda na kuitunza.
6. Tuache
kutumia mifuko ya plastiki. Hili
tumeshalizungumza sana lakini nawaomba tena wafanyabiasha waache tabia
yakuingiza mifuko ya plastiki nchini kwa njia za panya, kwani bila wao mifuko
hiyo ingekuwa hivi sasa haipo.
Ndugu
wananchi,
Leo
tunashuhudia athari za mabadiliko ya tabianchi za ukame wa muda mrefu na
mmong’onyoko wa fukwe. Athari hizi
ambazo ni baadhi tu ya athari nyingi za mabadiliko ya tabianchi, zimekuwa
zikichangia kwenye kasi ya upoteaji wa miti katika maeneo mbalimbali ya visiwa
vyetu. Miti mingi imekufa na itaendelea
kufa kwa kukosa mvua, na mingine imeng’oka na itaendelea kung’oka kwa
mmong’onyoko wa fukwe. Hali hii
inatutahadharisha kuwa miti tutakayoipanda tuhakikishe inakuwa na usimamizi
mzuri hadi kukuwa kwake na sio kuitupa, na pia tuipande katika maeneo
yanayostahiki ili kuepusha kuanguka kwa mmong’onyoko.
Ndugu
wananchi,
Maadhimisho
ya siku Mazingira Duniani kwa hapa Zanzibar yanafikia kilele chake siku ya
tarehe 5 Juni 2012. Kwa mwaka huu Ofisi
ya Makamu wa Kwanza wa Rais imeamua kuadhimisha siku hii kwa utaratibu tofauti
na ule miaka ya nyuma. Kwa mwaka huu
wafanyakazi wa taasisi za Serikali wameshirikiana na wananchi kupitia vikundi
vya mazoezi na vya mazingira kutoka Shehia mbalimbali Unguja na Pemba na
kufanya usafi kwenye maeneo mbalimbali.
Serikali kupitia OMKR imenunua vifaa mbalimbali vikiwemo mabero na pauro
na kuwakabidhi wananchi ili kuendeleza shughuli za usafi katika maeneo yao. Aidha, OMKR imeshirikiana na wananchi kupanda
miti ipatayo ELFU HAMSINI huko Pemba hasa katika eneo la Uwandani ambalo
limeathirika kwa kuchimbwa matofali ya mawe.
Zaidi ya hayo, OMKR imeendelea kutoa elimu ya mazingira kupitia michezo
kwa wadau wa michezo ambapo skuli NANE zilishiriki mashindano ya kombe la mazingira
huko kisiwani Pemba. Mechi ya fainali ya
mashindano hayo itafanyika siku ya kilele.
Katika siku hiyo pia kutafanyika mdahalo kwa skuli mbili za sekondari
kisiwani Pemba ili kujadili suala la mazingira ambapo hoja na ufafanuzi wa
masuala ya kimazingira utatolewa.
Ndugu
wananchi,
Pamoja
na juhudi zote zinazoendelea kuchukuliwa za kuhifadhi kulinda mazingira yetu,
mafanikio halisi yatapatikana kama kutakuwa na ushiriki wenu katika juhudi
hizi. Nawapongeza wananchi walioamua kuunda
vikundi vyenye kujishulisha na uhifadhi wa mazingira mjini na vijijni. Muda hauturuhusu
kuvitaja kimojakimoja lakini naomba kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar wapokee shukurani hizi.
Aidha
nachukua fursa hii kuzipongeza taasisi zinazofanya kazi bega kwa bega na OMKR
katika kuhakikisha kuwa mazingira yetu hayaharibiwi. Nitakua mwizi wa fadhila
ikiwa nitasahau mchango wa Wanahabari katika kutoa taarifa na taaluma
zinazohusu mazingira kwa wananchi hapa nchini na nje ya nchi. Naomba pia nitaje Hoteli ya RENCO ya Nungwi, Pemba
Misali Sunset Beach, Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), United Petroleum Ltd., Stone
Town Traders, na Drop of Zanzibar, bila kusahau miradi ya MACEMP na SMOLE kwa msaada
wao katika kufanikisha wa maadhimsho haya ya siku ya Mazingira kwa mwaka huu wa
2012.
Ndugu
wananchi,
Kwa
mara nyengine tena, naomba kuwashauri juu ya haja ya kutekeleza wajibu na
jukumu la kulinda mazingira kwa mustakbali wa maisha yetu na vizazi vyetu
vijavyo. Naomba kila mmoja wetu achukue
hatua leo za kuhakisha kuwa analinda na anahifadhi Mazingira kwayake na kizazi
kijachi
Shime sote tushiriki
katika tuhifadhi Mazingira yetu
Ahsanteni
sana kwa kunisikiliza.
Mimi mtu akiniambia anashughulikia mazingira Z'bar hata simuelewi. Naona nchi inamalizika, kujengwa kwenye vyanzo vya maji na maeneo ya kilimo.
ReplyDeleteSijawahi kuona kampeni za upandaji miti wala nini huyo fereji sijui anatwambia nini?
Hivi wewe ni mkaazi wa Zanzibar au vipi? Wazanzibar sasa tumehamasika katika masuala ya kimazingira, kila Wilaya kuna vikundi vingi tu vinavyoshughulika na uhifadhi wa mazingira ikiwemo uhifadhi wa misitu na vianzio vya maji, uhifadhi mzuri wa taka, uvunaji endelevu wa maliasili zetu na vyengine vingi tu vinavyohamasisha uimarishaji mzuri wa mazingira ya visiwa vyetu.
DeleteTatizo liliopo sio Fereji ila mashirikiano baina ya taasisi mbalimbali mfano wizara ya Maji, Ardhi, Kilimo, Mifugo, Tawala za Mikoa, Baraza la Manispaa pamoja na wananchi wengi wa Zanzibar yamekuwa ni madogo. Naamini ikiwa taasisi zote hizi zitatoa ushirikiano mzuri na Fereji(Mazingira), Zanzibar tutafika pazuri sana.
Huu si wakati wa kulaumiana bali kushirikiana kwa hali na mali kulinda na kuhifadhi mazingira ya viswa vyetu sawa na tunavyoshirikiana katika mambo mengine ya kimaendeleo
LABDA MAZINGIRA KWAO NI NI MIFUKO YA PLASTIKI TU.
ReplyDelete