Habari za Punde

Makungu apiga jeki timu Copa Coca Cola

Na Salum Vuai, Maelezo
Timu za mikoa mitano ya Unguja na Pemba zinazojiandaa
na mashindanoya Copa Coca Cola, zimefarajika baada ya kuahidiwa msaada wa shilingi milioni moja kila moja, kutokia kwa Mkurugenzi wa hoteli ya Zanzibar Ocean View Amani Ibrahim Makungu.

Hatua hiyo imekuja baada ya timu ya Wilaya ya Mjini kumuomba Mkurugenzi huyo aisaidie kwa kuwa inajiandaa na matatizo mbalimbali katika maandalizi yake.

Vijana hao walimueleza Makungu wakati walipokutana uwanja wa Amaan juzi, alipokwenda kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea urais wa Chama cha Soka Zanzibar katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Juni 30, mwaka huu.

Kutokana na maombi hayo, na ukweli kwamba Zanzibar inawakilishwa na timu za mikoa mitano kwenye ngarambe hizo, Makungu alisema haitakuwa busara kuisaidia timu hiyo pekee, na hivyo kuahidi kuzipatia timu zote hizo fedha shilingi milioni moja ili ziweze kuiwakilisha vyema nchi yao.

Katika mashindano hayo yanayoshirikisha timu za vijana walio chini ya miaka 17 kutoka mikoa yote ya Tanzania,

Zanzibar itawakilishwa na timu za mikoa ya Mjini Magharibi, Kusini na Kaskazini Unguja, Kusini Pemba pamoja na Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Baadhi ya timu hizo ikiwemo ya Mkoa wa Kusini, zinatarajiwa kuanza kuondoka leo kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya michuano hiyo.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.