Na Mwani Nyangasa, Dar es Salaam.
ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Marcio Maximo, amekiri kuwa ni kweli yupo katika mazungumzo na klabu ya Yanga ila bado hawajakubaliana siku ya kuja na si rahisi kama uongozi wa timu hiyo unavyodhani.
Maximo kwa sasa anainoa klabu ya Democrata F.C ya mjini Rio de Jeneiro, Brazil, baada ya kumaliza mkataba wake na TFF mwezi wa Agosti mwaka 2009 ambapo Shirikisho hilo lilishindwa kumuongezea mkataba kwa kutoridhishwa na utendaji wake na nafasi yake kuchukuliwa na Jan Poulsen wa Denmark.
Poulsen pia alishindwa kuisaidia Tanzania na kulazimika kuondoka miezi kadhaa iliyopita, ambapo TFF imemuajiri Mdenishi mwengine Kim Poulsen.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya mtandao, Maximo alisema bado yupo katika mkataba na klabu yake, hivyo si rahisi kukurupuka na kuondoka kwani anapaswa kufuata mkataba unavyoelekeza.
“Ni kweli nimo katika mazungumzo na Yanga lakini pia nina mkataba na klabu ya Democrata, si rahisi mimi kuja huko kwa sasa bila kufuata taratibu, na pia hatujapanga na Yanga tarehe ya mimi kuja huko, nashangaa kusikia kuwa watu wanasubiri kuwasili kwangu”, aliweka bayana Maximo.
“Mimi naheshimu sana mkataba na kama kuja ni lazima nifuate taratibu kwanza na si kukurupuka, si rahisi labda wasiwe wanajua nini maana ya mkataba, sijapangiwa na wala tiketi sina kwa kuwa hatujafikia huko,” alisema Mbrazili huyo.
Hata hivyo, alieleza kufurahishwa kwake na nia ya Yanga kumtaka aifundishe, na kuongeza kuwa kama wataafikiana hatakuwa na budi kuja kujiunga nayo.
Alisema anafuatilia kwa makini mchakato wa uongozi wa timu hiyo kwa sababu ameona wakurugenzi wake wana nia thabiti ya kuiendeleza klabu hiyo na hivyo hataki kuwaangusha.
Katika hatua nyengine, kocha huyo amesema amepata ofa za kufundisha klabu ya St. George ya Ethiopia na timu za Taifa za Zimbabwe na Rwanda, na kwamba anafikiria wapi anakoweza kwenda kama ataamua kuachana na Democrata.
Awali uongozi wa Yanga uliuambia umma kuwa Maximo angewasili Jumanne wiki iliyopita na baadae kudai angefika juzi Jumapili, lakini kauli ya kocha huyo inaonesha kama klabu hiyo imeingizwa mkenge.
No comments:
Post a Comment