Dar es Salaam
KOCHA wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars Marcio Maximo, anatarajiwa kuwasili leo tayari kuanza kibarua kipya cha kuinoa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga Louis Sendeu, mara baada ya kuwasili, Maximo atafanya taratibu za usajili kabla ya Alkhamisi ijayo, na kuanza maandalizi rasmi ya kukinoa kikosi hicho kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame.
Michuano ya Kagame ambayo Yanga ndio bingwa mtetezi,imepangwa kuanza kutimua vumbi mwishoni mwa mwezi huu jijini Dar es Salaam.
Wakati huohuo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart John Hall, anatarajiwa kuwasili nchini leo asubuhi kwa ajili ya kuanza programu ya maandalizi kwa mashindano ya Kombe la Kagame kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Stewart alikuwa nchini kwao Uingereza kwa mapumziko baada ya kumaliza msimu uliopita kwa mafanikio ya kutwaa medali ya fedha kwa kuwa washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom.
Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrissa, amekaririwa akisema kuwa, kwa vile kocha huyo atafika nchini waklati wa asubuhi, wanatarajia kuanza mazoezi jioni ya leo.
Idrissa 'Father', amesema wachezaji wote wa kimataifa wameshawasili, tayari kwa kuanza mazoezi hayo wakiwa pamoja na wachezaji wengine, na kuongeza kuwa wachezaji waliopo timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ watajiunga mara baada ya kumaliza michezo yao, na wale wa Zanzibar Heroes ambao wamerejea nchini jana, watarejea kikosini humo wakati wowote kuanzia sasa.
No comments:
Post a Comment