Habari za Punde

MBAROUK AONGOZA MAPOKEZI ZANZIBAR HEROES NA KUSEMA. Piga ua tunataka ubingwa Chalenji 2012. Aandaa zawadi ya vespa kwa wachezaji, makocha. Ataka BTMZ, ZFA ziepuke maandalizi ya zimamoto.

Na Salum Vuai, Maelezo
KIKOSI cha timu ya Taifa ya Zanzibar, 'The Zanzibar Heroes', kiliwasili nchini jana baada ya kushika nafasi ya tatu kwenye mashindano ya Kombe la Dunia kwa nchi ambazo sio wanachama wa Shirikisho la Fifa, yaliyofanyika nchini Kurdsitan na kupata mapokezi makubwa.

Msafara wa timu hiyo uliopanda boti ya Kilimanjaro, uliwasili katika bandari ya Zanzibar mnamo saa 5:30 asubuhi, ambapo Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk, aliwaongoza watendaji wa wizara yake na wananchi wengine kuwalaki vijana hao.

Akizungumza katika hafla ya kuwapongeza iliyofanyika baadae kwenye hoteli ya Bwawani, Waziri Mbarouk alisema hatua waliyofika si ndogo na akawasifia kwa namna walivyoonesha mshikamano, nidhamu na kujituma licha ya kukumbana na matatizo ya hapa na pale wakati wakijiandaa, na hadi wanasafiri kwenda Kurdistan.

Hata hivyo, alisema ushiriki wa Zanzibar Heroes kwenye kinyang'anyiro hicho na mafanikio waliyopata, umetoa changamoto kubwa kwa wizara yake na mamlaka zinazosimamia michezo hasa soka, katika dhamira ya kuirejeshea Zanzibar hadhi iliyokuwa nayo kisoka katika miaka ya nyuma.

Kwa hivyo, Waziri Mbarouk alisema kutokea hapo, lengo la sasa liwe kuiletea Zanzibar kombe la Chalenji ambalo mashindano yake yanatarajiwa kufanyika mwezi wa Novemba mwaka huu.

"Nawaomba viongozi wa Kamisheni ya Michezo, Baraza na ZFA mjitahidi na kushirikiana ili kuhakikisha, piga ua, kombe la Chalenji mwaka huu linakuja katika ardhi ya Zanzibar, jiandaeni mtuletee mahitaji yenu ili tujiandae mapema ", alisisitiza Waziri huyo.

Alifahamisha kuwa, maandalizi ya kutosha yasiyokuwa ya kukurupuka wala zimamoto yanahitajika ili kutimiza azma hiyo itakayowapa faraja Wazanzibari na wapenda michezo wote wa visiwa hivi.

Aliahidi kuwa, endapo Zanzibar itamudu kunyakua kikombe hicho, atawazawadia wachezaji wote watakaokuwa katika kikosi hicho pamoja na makocha wao, vespa moja kila mmoja, na kwamba kilicho mbele yake kwa sasa, ni maandalizi ya kuzitafuta vespa hizo.

Katika hatua nyengine, Waziri huyo ambaye aliwaahidi kumpa kila mchezaji shilingi milioni moja kama wangetwaa ubingwa wa VIVA, au laki tano kwa nafasi ya pili, aliwafariji kwa tunza ya shilingi 250,000 kwa kila mchezaji na makocha wao, na pia nyongeza ya shilingi laki moja kwa mwanandinga Khamis Mcha 'Viali, aliyefunga mabao matatu (hat trick) katika mechi mbili mtawalia, pamoja na Nadir Haroub 'Cannavaro', ambaye aliibuka mchezaji bora wa ngarambe hizo.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyoambatana na chakula cha mchana, nahodha wa timu hiyo Abdi Kassim 'Babi', aliishukuru Serikali ya Zanzibar kupitia Wizara inayoshughulikia michezo, kwa kuisaidia timu hiyo hadi kusafiri, na kusema kuwa changamoto kadhaa walizopata, ni miongoni mwa matukio ya kawaida pahala popote pale.

Timu ya Zanzibar Heroes, ilikuwa ikishiriki katika mashindano ya Kombe la Dunia la VIVA nchini Kurdistan, yaliyoshirikisha timu kutoka nchi tisa ambazo si wanachama wa Fifa, na kuongoza kundi B kwa kuzifunga timu za Raetia na Tamil Eelam mabao 6-0 na 3-0 mtawalia, baadae ikafungwa na Cyprus ya Kaskazini mabao 2-0 katika nusu fainali, kabla kuichakaza Provence mabao 7-2 na kushika nafasi ya tatu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.