Habari za Punde

Taifa Stars, Gambia zaingiza 124 m/-

DAR ES SALAAM
MECHI ya mchujo ya Kombe la Dunia Kanda ya Afrika kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Gambia (The Scorpions) iliyochezwa Juni 10 mwaka huu katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza shilingi milioni 124,038,000.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura, amesema mapato hayo yametokana na mashabiki 31,122 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya shilingi 3,000, 5,000, 10,000, 20,000 na shilingi 30,000.

Amesema asilimia 18 ya mapato hayo ambayo ni shilingi 18,921,050.85 imekwenda kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) wakati gharama kabla ya mgao zilikuwa tiketi (sh. 6,555,000) na bonasi kwa Taifa Stars (sh. 15,767,542.37).

Kwa upande wa waamuzi (sh. 13,372,000), usafi na ulinzi (sh. 2,350,000), maandalizi ya uwanja (sh. 400,000), Wachina-Beijing Construction (sh. 2,000,000), umeme (sh. 300,000) na mafuta ya jenereta (sh. 200,000).

Amesema kwa upande wa mgao asilimia 20 ya gharama za mechi ni shilingi 12,834,481, asilimia 10 ya uwanja shilingi 6,417,241, asilimia tano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) shilingi 3,208,620, asilimia 20 ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) shilingi 12,834,481 na asilimia 45 ya TFF (sh. 28,877,583).

Katika mchezo huo wa kundi C, Tanzania ilishinda kwa mabao 2-1 na kushika nafasi ya pili nyuma ya vinara Ivory Coast.



1 comment:

  1. ZFA zao ngapi kwasababu Taifa stars ni ya muungano.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.