Na Salum Vuai, Maelezo
BAADA ya timu ya Zanzibar Heroes kuibuka mshindi wa tatu kwenye michuano ya Kombe la Dunia la VIVA, ushauri umetolewa kwa mamlaka zinazosimamia michezo nchini, kuhakikisha zinaandaa mikakati endelevu kwa kuwekeza katika timu za taifa ili kuinua vipaji vya wachezaji na kuitangaza Zanzibar kimataifa.
Katika tafrija ya kuwakaribisha na kuwapongeza wachezaji wa Zanzibar Heroes waliowasili jana kutoka Kurdistan, Mkuu wa msafara wa timu hiyo Khamis Abdallah Said, alisema jitihada na uwezo uliooneshwa na wanasoka hao huko Kurdistan, umeacha gumzo kubwa miongoni mwa wananchi wa huko.
Miongoni mwa mikakati hiyo, alisema, ni pamoja na kuwawekea bima wachezaji, ili waweze kukabiliana na matatizo yoyote ya kuumia pale yanapotokezea kwa bahati mbaya.
"Wakati tukiwa kwenye mashindano, tulikuwa tukipata wasiwasi kwa kuwaza kama ingetokea bahati mbaya mchezaji akakatika mguu, hali ingekuwaje, kwani wachezaji wetu hawa hawana bima yoyote", alifafanua Said.
Alisema iko haja kwa sasa, kulipa uzito wa pekee suala la kuwekeza katika timu za taifa za umri tafauti, kuanzia chini ya miaka 15 (U-15) hadi timu kubwa, ili kuandaa mazingira mazuri ya kufanya vyema wakati zinaposhiriki mashindano ya kikanda na kimataifa.
Alivisifia vipaji vya wanandinga hao na kusema ushiriki wao katika michuano hiyo, waliitangaza vyema Zanzibar, kiasi cha kupendwa sana na mashabiki wa soka nchini Kurdistan, na kueleza kuwa wapo waliokuwa wakicheza kamari kuitabiria ushindi timu hiyo.
Aidha alisema michuano hiyo imedhihirisha hazina kubwa ya makocha waliopo Zanzibar, ambao alieleza kuwa wanaweza kufanya makubwa, kama watapata muda wa kutosha kuziandaa timu zao.
"Pamoja na jitihada ya wachezaji wetu, nidhamu na ushirikiano, lakini makocha wetu wamefanya kazi kubwa na kuwashangaza wenyeji wa mashindano na nchi nyengine zilizoshiriki", alieleza Said ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ).
Mapema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Ali Mwinyikai, aliwapongeza wachezaji hao kwa kusema licha ya misukukosuko ya hapa na pale, waliweza kuyaacha nyuma na kuingia kwenye mashindano kwa nia moja ya kuiletea heshima nchi yao.
Hongera Zanzibar Heroes kwa kupeperusha vyema bendera yetu, next time mwanachama kamili wa FIFA(sio wa nchi zisizo mwanachama) kwani michezo sio suala la muungano...
ReplyDeleteMANENO FIFA tu...yaliyobaki ni blah blah blah
ReplyDelete