Habari za Punde

Serikali Kuwajengea Uwezo Wananchi Kupitia Zakka


Na Rajab Mkasaba, Ikulu

SERIKALI  ya Mapinduzi Zanzibar imedhamiria kwa dhati kuitumia fursa ya utoaji wa Zaka kuwa ni mojawapo ya vianzio vya kuwajengea uwezo wananchi katika jitihada za kuongeza mapato yao na kuwapunguzia umasikini.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema aliyasema hayo leo katika hafla ya uzinudizi wa Mfuko wa Zaka Zanzibar, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Bwani mjini Zanzibar.


Katika hotuba yake Dk. Shein alisema kuwa Uislamu unafundisha kuwa utoaji wa Zaka katika jamii una mchango mkubwa katika kuinua hali ya maisha ya watu.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuwa tayari Serikali imeshajitayarisha na utekelezaji wa azma hiyo huko chombo maalum cha kuratibu shughuli za Zaka Zanzibar kimeshaanzishwa na kitaendesha shughuli zake chini ya Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana.

Dk. Shein alitoa wito kwa kila mwananchi wa Zanzibar kuitumia fursa ya kutoa Zaka na kuuchangia Mfuko wa Zaka ili kutekeleza wajibu kwa MwenyeziMungu na kuzingatia manufaa mengine.

Alieleza kuwa vigezo vya namna ambayo mfuko kama huu unaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuinua maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi yanaonekana katika mataifa mbali mbali yakiwemo Sudan, Afrika Kusini, Uturuki na nchi nyenginezo.

Dk. Shein alisema kuwa inadhirisha kusikia kuwa tayari kuna kiasi cha fedha ambazo zimeshachangwa na watu mbali mbali kwa ajili ya Mfuko huu na mipango imeshatayarishwa juu ya namna bora zaidi ya kuzihifadhi amana hizo, kuzitumia kwa utaratibu na maelekezo maalum na pia kuwepo kwa utaratibu wa kuhakikisha kuwa Mfuko wa Zaka Zanzibar unakuwa endelevu.

“Ni wajibu wetu kuziunga mkono jitihada hizi iwe kwa kuchangia, kusimamia na wale watakaopewa Zaka hii waitumie katika malengo yanayomridhisha MwenyeziMungu na ufike wakati na wao wanapopewa waanze kupata uwezo wa kuwapa wengine kama lengo kuu la Mfuko huo linavyokusudiwa”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alitoa wito wa kufikishiwa ujumbe wananchi wote wa Zanzibar juu ya hatua hiyo na kueleza kuwa vitabu vya Muongozo wa Zaka na Muongozo wa Sadakatul Jariya ambao nao uko njiani vitumiwe vizuri katika kuwaelimisha wananchi.

Pia, Dk. Shein alitoa shukurani kwa uonghozi wa Ofisi ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar na Wizara ya Katiba na Sheria kwa jitihada zao katika kuifanikisha hatua hiyo ya kuzinduliwa rasmi kwa shughuli za Zaka Zanzibar.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ipo pamoja nao katika utekelezaji wa shughuli hizi na wakati wote itakuwa tayari kupokea ushauri wa namna bora ya kuziendeleza shughuli hizo kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa jumla.

Nae Kaimu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria ambaye pia ni Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, alisema kuwa  juhudi za makusudi zitafanywa katika kuhakikisha walengwa ndio wanaofaidika na Zaka hiyo.

Waziri huyo alitoa wito kwa waumini na wadau mbali mbali kuimarisha mashirikiano katika kuimarisha azma hiyo.

Mapema  Katibu  Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana, Sheikh Abdalla  Talib alisema kuwa shughuli za Zaka azinazinduliwa rasmi wakati tayari muongozo umeshaandaliwa, akaunti maalum ya zaka imeshafunguliwa, baadhi ya Waislamu wameshaanza kutoa zaka zao na utaratibu wa kukiendeleza kitengo cha Zaka hatua kwa hatua hadi iwe ni Mamlaka kamili (Diwani ya Zaka) inayojitegemea umeshawekwa.

Alisema kuwa  kwa kutambua Makusudio ya Sharia ni kumpa mtu Zaka na kumuongoza ili imkombowe kiuchumi na kumfanya hatimae nae awe ni mtoaji wa Zaka, Kamisheni itashirikiana na taasisi nyengine za kiserikali na jumuiya ya dini ili kuhakikisha kuwa inawafikia watu wanaostahiki kutoa na kupokea Zaka katika sehemu zote za Unguja na Pemba.

Katibu huyo aliahidi kuelimisha, kuongoza, kukusanya na kugawa kwa uadilifu kwa kuzingatia uwezo wa mfuko na vigezo vilivyomo katika muongozo ambavyo vimejengeka kwa mafundisho ya Kurani, Sunna na Ijitihadi za wanachuoni.

Katika hafla hiyo viongozi mbali mbali wa dini na serikali walihudhuria akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.

1 comment:

  1. SMZ itafanya KOSA kubwa kuukabidhi mfuko wa zakka kwa Idara ya Wakfu na mali ya Amana.

    Idara hii imeshindwa kazi kabisa! na mkitaka kujua tazameni namna wanavyosimamia mali za wakfu kama vile nyumba kule mji mkongongwe.

    Nyingi kati ya nyumba za wakfu zimeanguka na kuchakaa vibaya kwa kukosa matunzo na hivyo kuwakosesha wahusika 'swadakatul-jariyya' zao.

    Jengine ni namna walivyoshindwa kusimamia mfumo wa elimu ya madrassa hapa Z'bar.
    Hadi leo hii hakuna utaratibu unoeleweka ktk kuanzisha Madrassa au namna ya kufundisha mfano: alieko alifu, Surati qafiruun, au surati bakara wote darassa moja!

    Na anehitimu hapewi utambulisho wowote! na walimu wa vyuo wanashindwa kubalance elimu ya skuli na qur-ani.

    Matokeo ya uzembe huu leo hii tabu sana kukuta mtoto aliyekhitimu qur-ani ndio akina sisi wa 'ABU TAUSI'

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.