Habari za Punde

SMZ Kutekeleza Miradi 84 ya Maendeleo

Na Mwantanga Ame
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee amesema katika bajeti ya mwaka 2012- 2013, jumla ya programu 38 na miradi 84 ambayo itajumuisha programu sita itatekelezwa.

Waziri huyo alieleza hayo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa akiwasilisha bajeti ya mwaka 2012- 2013 ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo alisema miradi 18 kati ya maendeleo kati ya hiyo itakuwa mipya.

Alifahamisha kuwa miradi na programu hiyo inatarajiwa kutumia shilingi bilioni 341.1 ambapo serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachangia shilingi bilioni 47.9 ambazo ni sawa na asilimia 14 na washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia shilingi bilioni 293.2 sawa na asilimia 86 ya bajeti ya kazi za maendeleo.

Alisema kati ya fedha zinazotoka kwa washirika wa maendeleo, kwa ajili ya kutekeleza programu hizo ni shilingi bilioni 187.7 ikiwa ni mkopo na shilingi 105.4 bilioni zitakuwa ni ruzuku.

Alifahamisha kuwa kwa mwaka ujao wa fedha, klasta ya kwanza ina jumla ya program 21 na miradi 25 itakayogharimu shilingi bilioni 197.9 sawa na asilimia 58 ya makadirio ya bajeti ya maendeleo.

Alisema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 18.9 ikiwa ni sawa na asilimia 10 zinatarajiwa kutolewa na serikali na shilingi bilioni 179.0 ni mchango kutoka kwa washirika wa maendeleo ikiwa ni sawa na asilimia 90, na mikopo ni shilingi 104.5 bilioni na ruzuku ni shilingi 74.5 bilioni.

Alisema klasta ya pili itahusu huduma za Ustawi wa Jamii ambapo inatarajiwa kutumia shilingi bilioni 117.7 ikiwa ni sawa na asilimia 35 kugharamia utekelezaji wa program 11 na Miradi 33.

Alisema serikali pia inatarajia kutoa shilingi bilioni 13.7 ambazo ni sawa na asilimia 12 ya bajeti yote ya klasta hiyo na washirika wa maendeleo ni shilingi bilioni 104.0 ikiwa ni sawa na asilimia 88 na mkopo ni shilingi bilioni 79.9 huku ruzuku ikiwa ni shilingi bilioni 24.1.

Waziri huyo pia alisema klasta ya Utawala Bora na Umoja wa Kitaifa inatarajiwa kutekeleza program sita na miradi 26 yenye, jumla ya shilingi bilioni 25.4 sawa na asilimia 7 ya bajeti ya maendeleo.

Akiendelea waziri huyo, alisema serikali inatarajiwa kutoa shilingi 15.3 bilioni ikiwa ni sawa na asilimia 60 na washirika wa maendeleo ni shilingi bilioni 10.1 ikiwa ni sawa na asilimia 40 ya makadirio ya klasta ya tatu ambapo mikopo ni shilingi bilioni 3.2 na ruzuku ni shilingi bilioni 6.9.

Miradi mikuu itakayotekelezwa na serikali ni pamoja na kukamilisha na kuzindua ujenzi wa njia ya pili ya umeme kutoka Ras-Kiromoni hadi Fumba, mradi wa kuimarisha njia za umeme.

Mradi mwengine alioutaja waziri huyo alisema ni pamoja na kuendeleza ujenzi wa jengo jipya la abiria katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume, mradi wa kuimarisha elimu ya lazima, mradi wa Elimu Mbadala na Amali, programu ya kukuza ajira kwa vijana na programu ya kuimarisha miundombinu ya Afya.

Akizungumzia Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, waziri huyo alisema kwa mwaka wa fedha mpya, serikali imetenga jumla ya shilingi 760 milioni ambapo kila jimbo litapatiwa shilingi milioni 15 kwa mwaka kutoka shilingi milioni 10, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 50, ili kusaidia juhudi za wananchi katika kujiletea maendeleo.

Kuhusu Mwelekeo wa mipango ya Maendeleo Waziri huyo alisema Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2012/13 utategemea zaidi utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2020 iliyorekebishwa, MKUZA II, pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010.

Waziri huyo alisema suala la ajira kwa vijana nalo serikali inakusudia kulifanyia kazi kwani karibu theluthi mbili ya asilimia 63.1 ya watu katika jamii ni ama watoto au vijana wasiopindukia umri wa miaka 24.

Alisema Waziri huyo kuwa kwa upande mwengine, idadi kubwa ya vijana wanamaliza skuli na kuingia katika soko la ajira kila mwaka na takwimu zinaonesha kuwa kati ya vijana watano asilimia 17 ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 mmoja hana ajira.

Alisema hali hiyo inaonesha kuwa tatizo la ajira kwa vijana ni kubwa na linahitaji hatua makhsusi kwa mwaka ujao wa fedha, baada ya kuandaa Programu maalumu ya kuwawezesha vijana katika shughuli za kiuchumi ikiwemo uvuvi, kilimo, kazi za usafi wa mji, ujasiri amali na utalii.

Alifahamisha programu hiyo ni hatua moja muhimu ya kukabiliana na tatizo la ajira lambapo jitihada zitawekwa katika kuwafunza vijana namna ya kubadilika katika mkabala wa kazi na kupunguza kuchagua sana aina ya kazi.

Akizungumzia juu ya namna ya kuwatunza Wazee, alisema miongoni mwa malengo ya Mapinduzi ya 1964 kwa kuhakikisha serikali inaimarisha ustawi wa wananchi wote, ikiwemo wa makundi yenye mahitaji maalum ya Wazee.

Alisema serikali mwaka jana iliongeza fedha za posho kwa Wazee kutoka shilingi 15,000 hadi 40,000 na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuimarisha hali za wazee kadiri hali ya uchumi inavyoruhusu.

Hata hivyo, alisema katika kutekeleza hilo ili kudumisha huduma kwa wazee wanaohudumiwa na serikali, kuanzia mwaka ujao wa fedha, Serikali itawapatia wazee wanaoishi katika kituo cha Sebleni huduma kamili ya chakula, posho na matibabu.

Aidha Waziri huyo alisema pia Wazee hao watapatiwa vitambulisho vitakavyowawezesha kupata huduma mbali mbali kwa utaratibu maalum na huduma kama hiz0 kwa wazee wanaoishi Welezo zinaendelea kutolewa vizuri.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.