Habari za Punde

Vuai:CCM Imewachoka Wabinafsi

Na Mwandishi wetu
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, amesema chama hicho hakitowavumilia viongozi wabinafsi na wale wenye tabia ya kupuuza maamuzi ya vikao vya kikatiba vinavyoandaliwa na chama hicho.

Naibu huyo alieleza hayo jana alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Halmashauri kuu ya majimbo ya wilaya ya Mjini Unguja ambapo alisema viongozi wa aina hiyo hawana nafasi ya kuendelea kuwemo ndani chama.

Alisema Mbunge, Mwakilishi, Diwani au Kiongozi yeyote kutoka CCM anayeshindwa kuheshimu na kusimamia maamuzi ya vikao, hutia mashaka juu ya utendaji wake na dhama alizopewa.

Aliwaeleza wajumbe hao kuwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi wasiotaka kulinda na kutetea maslahi ya chama hicho, wajitoe mapema na kuacha nyadhifa zao zote walizonazo.

Alifahamisha kuwa kiongozi asiyeweza kukitetea chama kwa nguvu za hoja hatoshi kuonekana kuwa mwanachama mtiifu kwa mujibu wa katiba ya chama hicho kwani uanachama wake haukidhi vigezo.

Naibu huyo alishangazwa kujichomoza tabia ya badhi ya wanachama na viongozi wa CCM kushabikia kushabikia sera na misimamo ya vyama vya upinzani, huku akisema watu wa aina hiyo wanapaswa kuangaliwa upya uanachama wao.

Akizungumzia vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na kikundi cha Uamsho, Naibu huyo alisema alisisitiza msimamo wake wa kumtaka waziri wa Sheria na Katiba wa serikali ya Mapinduzi, Abubakary Khamis Bakary, ajiuzulu wadhifa wake, kutokana na kujiegemeza upande wa jumuiya hiyo.

Alisema hakumtaka waziri huyo ajiuzulu kutokana na kumchukia kama inavyosemwa na baadhi ya watu, bali waziri huyo ameshindwa kumsaidia na kumshauri ipasavyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, kuhusiana na mambo ya kisheria, ambalo ndio jukumu lake la msingi.

“Mimi simchukii hata kidogo waziri wetu wa Sheria na Katiba wa Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya Mfumo wa Umoja wa Kitaifa, bali ameshindwa kumshauri ipasavyo Rais wa Zanzibar kuhusu hatua za kisheria zilizofaa kuchukuliwa dhidi ya kikundi cha Uamsho, kwani vitendo vinavyofanywa na kikundi hicho ni vya kuvunja sheria, na vina lengo la kuvuga amani ya nchi”, alisema Vuai.

Mapema Mwenyekiti wa CCM Mkoa Mjini Magharibi Yussuf Mohamed Yussuf alisema chama chake kimeathiriwa na matukio ya ghasia na maandamano yaliyofanywa na jumuiya ya Uamsho.

Alisema matukio hayo, kwa sehemu kubwa yamejenga taharuki na kuwapa wasiwasi usiomithilika wananchin kwa muda wa siku tatu mfululizo, jambo lililorejesha nyuma juhudi za kujiletea maendeleo.

Aidha Mwenyekiti huyo alisema maandamano hayo yaliyoambatana na ghasia yalichochea kwa kiasi kikubwa chuki na hasama zisizo na ulazima miongoni mwa wananchi wa Unguja na Pemba.

“Zanzibar sio chaka wala halitakuwa chaka la vikundi vya kigaidi duniani kama vile Al Qaeda, Al Shabab, Boko Haramu, hivyo tunaviomba vyombo vya dola kusimamia kikamilifu suala la amani ya nchi na watu wake, ili Zanzibar iendelee kuwa miongoni mwa nchi zenye amani duniani”, alisema Yussuf.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.