Habari za Punde

Taasisi Zahimizwa Kuwatumia vyema Wajasiriamali Nchini


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikagua bidhaa ya mmoja wa Wajasiriamali Tatu Suleiman wa Chukwani Zaidat Oil ambaye ni Mjasiri wa mwanzo kutoka Zanzibar aliyefikiwa kiwango cha juu cha ushindi katika Mpango wa Faidika Kibiashara Nchini Tanzania.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi Hundi ya Shilingi Milioni 697,000,000/- kwa Wajasiri Amali watano kwa niaba ya wenzao 213 wa Mikoa Mitano ya Zanzibar walioshindia kwenye Mafunzo ya Faidika Kibiashara Tanzania. Sherehe hizo zilifanyika katika Viwanja vya Victoria Garden Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar.

Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika Picha ya Pamoja na Viongozi wa Taasisi zilizofadhili na Kuendesha Mafunzo ya Faidika Kibiasha Nchini Tanzania kwenye Sherehe za utoaji zawadi kwa washindi wa mafunzo hayo hapo victoria Garden Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar.

Na Othman Khamis Ame

 Taasisi zinazowawezesha Wananchi Kiuchumi Nchini zimehimizwa kuwatumia vyema Wajasiri Amali wanaopata Mafunzo kwenye Mpango wa Faidika Kibiashara kwa lengo la kujenga mazingira bora zaidi ya ajira ndani ya Sekta Binafsi. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa Himizo hilo katika sherehe ya utoaji zawadi kwa Wajasiri Amali walioshiriki Mafunzo ya Mpango wa Faidika Kibiashara zilizofanyika kwenye Viwanja vya Victoria Garden Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar. 

Balozi Seif alisema mafanikio yaliyokusudiwa ndani ya Mpango huo yataweza kupatikana pindipo Taasisi hizo zitatumia ujuzi wa Wajasiri Amali hao na hatimae kukuza Uchumi wa Taifa. 


Aliziomba Taasisi zilizopo kwenye Sekta Binafsi kufikiria kuwa na Umoja imara kupitia Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar utakaoiwezesha Sekta hiyo kufikia malengo ya Taifa ya kukuza Uchumi Nchini. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Serikali itajitahidi kusaidia Sekta Binafsi ili ikue na kuchangia kwa kiasi kikubwa Maendeleo ya Nchi. 

Alieleza kuwa Mpango mzima wa Faidika Kibiashara umedhihirisha namna ya mafanikio baina ya Serikali na Sekta Binafsi yanavyowezekana pindipo itakuwepo mikakati imara. Mpango huo ni chem Chem ya Elimu ya Biashara ambayo Wafanyabiashara walengwa ni wale wadogo wadogo ambapo pia aliwaomba kutumia vyema fursa hiyo. 

“ Biashara bila ya Elimu, jawabu lake ni kufilisika. Nani kati yenu anataka kufilisika? Kama jawabu hapana maana yake tujitokeze kwa wingi kila fursa za mafunzo zinapotokea kwani Biashara ukiijumlisha na Mafunzo jawabu yake ni Mafanikio”. 

Alisisitiza Balozi Seif. Balozi Seif alilikubali ombi la Wajasiri Amali hao la Nchi kuwa na Wafanyabiashara wengi ambao wataliwezesha Taifa kuwa na Rasilmali na Hakiba ya kutosha ya Pato la Nchi. 

Alisena uimarikaji wa Sekta hiyo sambamba na Mafunzo ya Uwezeshaji kwa Umma utajenga hatma njema hasa kwa wafanyakazi wanaomaliza muda wao wa Utumishi Serikalini kuweza kujiendeleza Kibiashara. 

Alisema Wastaafu wengi hivi sasa wamekuwa wakibabaika kwa kukosa mtaji wa kuendeleza Maisha yao ya Uzeeni kutokana na ukosefu wa mafunzo ya Ujasiri amali. 

Katika Risala yao Wajasiri Amali hao wa Faidika Kibiashara wamezishukuru Taasisi za Benki ya Watu wa Zanzibar, Chuo cha Uongozi wa Fedha Chwaka pamoja na ZIFA zilizowawezesha kuwapatia Mtaaji wa Biashara zao ikiwemo Mafunzo na Mtaji. 

Hata hivyo Wajasiri amali hao wameelezea changa moto zinazowakabili katika harakati zao za Kiutendaji ikiwa ni pamoja na Uwezo mdogo wa kusomea Stadi za Biashara, Ruzuku pamoja na ukubwa wa Riba. 

Mapema Rais wa Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar Bwana Mbarouk Mohd alisema lengo Kuu la Mpango wa Faidika Kibiashara ni kuandaa mazingira ya Ushindani utakaoimarisha Uchumi kupitia Sekta ya Biashara. 

Bwana Mbarouk alizipongeza Taasisi za Benki ya Watu wa Zanzibar, ZIFA na Chuo cha Uongozi wa Fedha Chwaka kwa mchango wao wa kuendeleza Wajasiriamali wadogo wadogo hapa Nchini. Alisema Juhudi za Taasisi hizo zimepelekea Wajasiri amali wa Zanzibar kufaidika na Mpango huo kwa zaidi ya Shilingi Bilioni Mbili na kuwafanya kufikia asilimia 11% ya fedha zote zilizotolewa Nchini Tanzania katika Mpango huo wa Faidika Kibiashara. 

Akitoa Salamu zake Mwenyekiti Mtendaji wa Taasisi inayoziunganisha Jumuiya na Taasisi zote za Kibiashara Tanzania { TPSF } Bwana Simbei Jofrey alisema nguvu ya Kiuchumi ya Taifa lolote Duniani inategemea Biashara. 

Bwana Simbei aliziomba Serikali zote mbili kuandaa Mtaala katika Skuli za Sekondari Tanzania utakaofundisha Elimu ya Ujasiri amali ambayo itasaidia kupunguza wimbi la Vijana wasio na ajira ambao hivi sasa wanakadiriwa kufikia miioni Nane. 

Katika sherehe hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi hundi ya zaidi ya Shilingi Bilioni Mbili kwa Wajasiri Amali Watano kwa niaba ya wenzao 213 kutoka Mikoa yote Mitano ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.