Habari za Punde

Wabunge, Wawakilishi Tafuteni Ridhaa za Wananchi .Watakiwa Kuzungumza nao Kabla ya Kuwaamulia

Na Madina Issa
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai amewapiga ‘stop’ wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuzungumzia masuala ya kitaifa yanayowahusu wananchi bila ya kupata ushauri wao.

Naibu huyo alieleza hayo alipokuwa akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu za Majimbo ya wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.

Alisema haipendezi kwa Mbunge au Mwakilishi kutoa msimamo wake juu ya masuala yanayohusu taifa kupitia vyombo vya kutunga sheria huku akiwajumuisha wananchi wa jimbo lake, ilhali akijua kuwa hajawahi kwenda na kuzungumza nao.

“Nashangaa sana ninaposikia Mbunge au Mwakilishi anajitapa ndani ya Bunge au Baraza la Wawakilishi kwa kusema kwa niaba ya wananchi wa jimbo langu, tunaunga mkono au kukataa hoja, huku akijua fika kuwa hakukutana na kujadiliana na wapiga kura wake kutaka msimamo wao juu ya hoja fulani ya maslahi ya nchi”, alisema Naibu huyo.

Alisema wakati umefika kwa viongozi hasa waliochaguliwa na wananchi majimboni kuacha tabia ya kujipigia kifua na kuwasemea wananchi mambo yanayohusu mustakbali wa nchi, kwani kufanya hivyo kutaweza kuleta mitafaruku.

Akizungumzia suala la Muungano, Naibu Vuai alisema Chama cha Mapinduzi kitaendelea na sera yake ya serikali mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Aprili 26, 1964) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (Januari 12, 1964).

Akizungumzia juu ya uchaguzi mkuu wa CCM unaoendelea nchini kote aliwataka viongozi na wanachama wa CCM kuanzia ngazi za wadi, jimbo, wilaya na Mkoa, kuhakikisha wanawachagua viongozi bora, makini, wenye uwezo mkubwa wa kuchambua na kusimamia kwa nguvu ya hoja masuala mbalimbali ya kisiasa.

Hata hivyo alisema kuwa viongozi ndiyo wenye jukumu la kuhakikisha suala la umoja, maelewano na mshikamano unadumishwa ndani ya chama kwani umoja mshikamano ndio ngao na silaha thabiti itakayoweza kukipatia ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Alifahamisha kuwa nguvu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kisiasa zinaweza kupunguzwa na watu wasiokitakia mema Chama hicho na kusema hilo linaweza kufanikiwa endapo wanachama na viongozi wake watakubali kugawanywa na wenye kukubali kugawanyika.

“Iwapo viongozi katika ngazi mbalimbali wataanza kugombana wenyewe kwa wenyewe na kutoshikamana, hali hiyo itatoa mwanya kwa mahasimu wetu wa kisiasa kujijenga zaidi”. Alisema Naibu huyo.

Aidha alisisitiza kuwepo mashirikiano baina ya wanachama pamoja na viongozi wao kwa kuhakikisha wanafanya kazi ya Chama wakiwa nje ya Chama pamoja na ndani ya umma tena kwa bidiii zaidi, kwani wataweza kuleta maendeleo ya Taifa na wananchi wake.

Naibu huyo yumo katika ziara ya kisiasa ya siku sita katika wilaya zote 10 za Mikoa ya Zanzibar, kwa lengo la kuangalia na kuhimiza na uhai wa Chama cha Mapinduzi.



6 comments:

  1. Ahsante mkuu!
    Comment zako za siku za karibuni zinaashiria kubadilika kwa CCM- Z'bar!

    CCM, bado ni chama 'kubwa' Z'bar, iliharibiwa tuu na siasa za 'ujahil' za 1995-2000!

    ReplyDelete
  2. Weye vuai mbona huwambii ukweli hao wajumbe wako kwamba na hili pia wawasikilize wananchi wao kwamba hawautaki muungano nalo pia wawasikilize sio useme serikali mbili.

    ReplyDelete
  3. “Nashangaa sana ninaposikia Mbunge au Mwakilishi anajitapa ndani ya Bunge au Baraza la Wawakilishi kwa kusema kwa niaba ya wananchi wa jimbo langu, tunaunga mkono au kukataa hoja, huku akijua fika kuwa hakukutana na kujadiliana na wapiga kura wake kutaka msimamo wao juu ya hoja fulani ya maslahi ya nchi”, alisema Naibu huyo.
    Akizungumzia suala la Muungano, Naibu Vuai alisema Chama cha Mapinduzi kitaendelea na sera yake ya serikali mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Aprili 26, 1964) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (Januari 12, 1964).
    My take: Wewe Vuai ulimuuliza nani kuhusu huo muundo wa Serikali mbili, wewe au CCM ulikutana na kujadiliana na wananchi! especially Zanzibar?
    Inaoneka Vuai unajichanganya tu, kwani hayo yooote yanayopitishwa BLW na Bungeni Dodoma ni lini waliulizwa wananchi?
    Ni vizuri kabla hamjaropokwa mpitie walau KATIBA ya nchi na KANUNI iwe za BARAZA or BUNGE.

    ReplyDelete
  4. Muda wa vikao vya Bunge na Baraza la wawakilishi unakaribia kwa hivyo angalau wawalikilishi na wabunge watupitie, tuna mengi ya kuwashauri.

    Kila mtu hapa, anajiuliza ni lini atatokea mwakilishi aliyesoma na kupeleka muswada wa ardhi BLW ili ardhi ya visiwani itumika vizuri.

    Kwa kweli inasikitisha, baada ya mapinduzi serikali iligawa heka tatu tatu za ardhi kwa baadhi ya W'bari, wengi kati ya waliopewa wamesha fariki, sasa watoto wao wanazikata na kuziuza viwanja,..tuseme ni haki yao. lkn. serikali ya kihadimu inashindwa hata kuwashauri namna bora ya kukata viwanja vyenyewe?.. au na hili ni tatizo la muungano?

    ReplyDelete
  5. NYINYI CCM NA CUF, 2015 MKITUWEKEA WABUNGE NA WAWAKILISHI WASIWO NA ANGALAU DEGREE 1 MJUWE HATUWACHAGUI!

    TUSHACHOKA 'VIMEO' KAZI YAO KUTULETEA TV.NA VIDEO TU LAKINI HUSIKII KUPELEKA VITABU MASKULINI AU KUWALIPIA WANAFUNZI ADA ZA KURUDIA MITIHANI KWA WALE WALIWO FELI.

    WAKATI WA KULIPA FADHILA KWA WATU WALIOSAIDIA VYAMA UMEKWISHA!
    TUNATAKA AKINA KHALIFA, MNYAA, SADIFA, MAHADHI NA WENGINE LKN. WAKINA SEREWEJI BASI!!!!!! WARUDIE KAZI ZAO ZA UGANGA!!

    ReplyDelete
  6. LLB graduate Tunguu.June 10, 2012 at 8:36 AM

    Acheni usanii na sisi tunataka katiba mpya zanzibar! mlitufanyia kiini macho mkaitia viraka, kumbe mlikwisha jua mabadiliko ya katiba ya jamhuri yanakuja msipowahi na hapa hapatatosha!

    Katika mabadiliko hayo, mawaziri wa serikali wasizidi 5, watumishi wote wa serikali wasizidi miaka 60 na wanasiasa wasizi umri wa miaka 65. wakuu wa mikoa na wilaya wapigiwe kura.

    Masheha wasipungue elimu ya fom 4 na asizidi miaka 60 na si lazima awe mstaafu wa serikali. Sisi tumemaliza vyuo tunaambiwa ajira hamna kumbe wastaafu wanarejeshwa makazini.

    Katika kila mkoa, kuwe na mganga mkuu, mchumi, mwanasheria na mtakwimu na wakabidhi ripoti za maendeleo ya kila sekta nilio itaja.

    Mbali na maendeleo mabadiliko haya yanaweza kusaidia ajira kwa vijana.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.