Habari za Punde

ZOP Yatoa Matibabu Bure ya Masikio kwa Watoto

Na Madina Issa

WAZAZI na walezi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto wao katika matibabu yanayotolewa na jumuiya ya ZOP ambayo inasaidia jamii kwa kutoa matibabu ya koo, pua, presha, macho, masikio na maradhi ya sukari kwa ajili ya kupunguza au kumaliza matatizo yanayowakabili watoto wao.

Mganga msaidi wa kitengo cha pua, koo na masikio kutoka Hospitali kuu ya Mnazi mmoja, Mwanana Kassim Ali, alitoa wito huo juzi wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwafanyia baadhi ya watoto upasuaji wa masikio.

Alisema endapo wazazi na walezi watajitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya afya wataweza kugundua matatizo yanayowakabili watoto wao na hivyo kupatiwa matibabu yanayostahilki kwa mujibu wa matatizo wanayoyasumbua.

Alifahamisha kuwa matibabu hayo yanayotolewa na jumuiya hiyo yatawanufaisha watoto ambao wanaokabiliwa na matatizo ya usikivu ambapo pia masikio yao hayatoi uchafu.

Hata hivyo, alisema kuwa matibabu hayo yanatolewa kwa watoto kuanzia umri wa miaka kumi na kuendelea ambapo yamekuwa yakitolewa bure na kumalizika keshokutwa.

Kwa upande wa wagonjwa waliopatiwa matibabu hayo walisema wanaishukuru Jumuiya hiyo kwa kutoa matibabu hayo kwa wananchi wataweza kuepukana na matatizo hayo.

Nae mmoja wa mzazi aliyepatiwa matibababu, Elizabet Buhuyu, kutoka Kibaha, alisema amelazimika kutoka Kibaha kwa ajili ya kufuata huduma hiyo baada ya mtoto wake kusumbuliwa kwa muda mfrefu

"Niliposikia taarifa ya matibabu ya matatizo hayo niliona bure nije nimpeleke mtoto wangu ambapo tayari ameshapatiwa matibabu ya masikio yanayomsumbua kwa muda mrefu baada ya kuhangaika katika hospitali nyingi," alisema.

Hata hivyo, aliitaka jumuiya hiyo kuendeleza matibabu hayo kwani yataweza kutokomeza magonjwa hayo ambayo yanawasumbuwa watoto kwa kipindi kirefu.

Matibabu hayo ya upasuaji wa masikio yameandaliwa na jumuiya ya Zanzibar Outreach Program (ZOP) kwa kushirikiana na kitengo cha ENT cha hospitali ya Mnazi Mmoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.