Habari za Punde

Bajeti ya Elimu yapita. Vyeti Feki Vyalalamikiwa

Na Mwantanga Ame
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali imekiri kuwapo kwa vyeti feki vilivyotolewa kwa baadhi ya wanafunzi baada ya kuibiwa vyeti hivyo katika Chuo cha Kiislam.

Waziri wa wizara hiyo, Ali Juma Shamhuna, aliyasema hayo jana wakati akijibu hoja mbali mbali za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakati wajumbe hao wakipitisha mafungu ya Bajeti hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/1013, kikao ambacho kinaendelea Chukwani Nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Hatua ya waziri huyo ilikuja baada ya Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtupura Hamza Hassan Juma, kuzuiya fungu la bajeti hiyo kwa kuhoji juu ya suala la vyeti feki katika Chuo cha Kiislamu na kueleza kwanini wizara hiyo ilishindwa kulitolea tamko.

Mwakilishi huyo katika hoja yake alisema kuna wanafunzi 405 ambao wamepatiwa vyeti hivyo baada ya kulipia shilingi 300,000 zilizokabidhiwa kwa maofisa wa wizara hiyo ambao wanadaiwa kupokea zaidi ya milioni 600.

Alisema katika hoja yake hiyo suala hilo kulikuwa na wanafunzi 775 ambao walifanya mitihani yao na kati ya hao baadhi yao waliofanya vizuri, lakini wapo waliopata mitihani ya marejeo ni wanafunzi (Supplementary) ambao ni 370 na waliopata sifuri walikuwa ni wanafunzi 405 ambao ndio wanaodaiwa kupewa vyeti feki.

Akijibu hoja hiyo, waziri Shamhuna alisema ni kweli suala hilo lipo baada ya kuipata taarifa ndani ya Baraza hilo na wizara hiyo iliamua kukaa na uongozi wa chuo hicho kuweza kupata ukweli na umekiri hilo.

Alisema mkuu wa chuo hicho aliueleza uongozi wa wizara hiyo kuwa hilo limetendeka baada ya kugundua ndani ya ghala yake ya Chuo kupungua kwa vyeti hivyo na hakuwa na taarifa ya kuwapo kwa mambo hayo.

Alisema kuhusu saini iliyokutwa ndani ya vyeti hivyo ya katibu Mkuu, alisema hiyo haina ukweli kutokana na kukataa kuweka saini vyeti hivyo na huenda ikawa waliofanya hivyo wamegushi.

“Tayari tumemkamata Mkuu wa Chuo alisema anakubaliana na suala hilo kutokana na kukiri kupungua kwa vyeti ndani ya ghala lake sasa tumeanzisha uchunguzi ili kubauni wahusika”, alisema waziri huyo.

Alisema watalifanyia kazi suala hilo kwa vile ni moja ya kosa la jinai na baada ya kupata ushahidi kamili wizara hiyo itahakikisha inalifikisha mbele ya vyombo vya sheria

Alisema Wizara hiyo itachukua hatua hiyo kwa vile tayari kuna wanafunzi ambao wameonesha nia ya kutaka kutoa ushahidi juu ya suala hilo.

Baada ya majibu hayo Mwakilishi huyo alikubaliana nayo na kueleza kuwa ni vyema serikali ikaliona tatizo hilo kwani kinachoonekana kuwapo kwa mambo yanayosikitisha kwa baadhi ya watu kuendelea na vitendo vya kuibia serikali.

Alisema ni lazima serikali baada ya kufanya uchunguzi wake kuhakikisha inawachukulia hatua bila ya kuwaonea haya watendaji hao kwani mchezo huo ukiachiwa utaendelea kuiumiza serikali.

Aidha, Mwakilishi huyo, aliiomba serikali kuona inawapatia kipaumbele baadhi ya wanafunzi ambao tayari hivi sasa wako mbioni kumaliza masomo yao katika fani ya sayansi kuona inawapa ajira ili wasiweze kukimbia kwenda Tanzania bara na kuopunguzia serikali kuajiri Walimu kutoka Nigeria.

Akijibu suala hilo, waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheir, alisema serikali hivi sasa imo katika kuhakikisha inawapa kipaumbele wanafunzi wa sayansi katika ajira ambapo inakusudia kutoa ajira kwa asilimia 90 kwa fani hiyo.

Mafungu ya bajeti hiyo kabla ya kupitishwa kwake baadhi ya Wajumbe akiwemo Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu, waliamua kutaka kuwekwa pembeni likiwemo fungu la Utafiti ambayo yalisababisha vuta nikuvute kwa wajumbe wa baraza hilo jambo ambalo lilisababisha baadhi ya mawaziri kusaidia kuinasua bajeti hiyo.

Baadhi ya Mawaziri ambao walisimama kuinasua bajeti hiyo ni pamoja na Haroun Ali Suleiman, Haji Omar Kheir, Mohammed Abod Mohammed, Omar Yussuf Mzee, huku hoja nyengine zikisaidiwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho.

Akijibu baadhi ya hoja hizo Naibu waziri wa wizara hiyo Zahra Ali Hamad, alisema upitishaji wa mafungu kwa mwaka huu ni tofauti na miaka iliyopita ambapo mwaka bajeti hiyo ilikuwa ikipitishwa kwa mfumo wa fungu kamili lakini hivi sasa mafungu hayo yanahitaji kufanyiwa uchambuzi kwa kifungu kimoja baada ya kimoja.

Hata hivyo, Mwakilishi huyo baada ya majibu hayo alikubaliana nayo kwa sharti la kuliweka upande likiwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha kwa kuhakikisha matumizi hayo yanafanyika kihalali.

Akijibu hoja hiyo Waziri wa Nchi Ofisi Fedha, Uchumi Mipango ya Maendeleo Omar Yussuf Mzee, alisema anakubaliana na Wizara hiyo na watahakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliokusudiwa baada ya Wajumbe wa Baraza hilo kulipitisha bajeti hiyo.

Mapema Naibu waziri wa wizara hiyo Zahra Ali Hamad, akichangia bajeti hiyo kwa hoja za wajumbe hao juu ya suala la hatua zilizochukuliwa na wizara hiyo kwa waliofutiwa matokeo jee upande wa walimu alisema tayari Wizara imelifanyia kazi.

Akifafanua kauli hiyo alisema hatua ya kwanza waliyoichukua ni kuwasusha vyeo walimu wakuu wawili na walimu 140 walitakiwa kujieleza ambapo hadi sasa waliofanya hivyo ni 15.

Hata hivyo, Wajumbe hao waliipitisha bajeti hiyo kwa kuiidhunishia Wizara hiyo jumla ya shilingi 110,091,291,000 ambapo kati ya fedha hizo shilingi 71,050,000,000 ni kwa matumizi ya kawaida na shilingi 5,100,000,000 za SMZ na shilingi 33,869,291,000 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.