Na Mwashamba Juma
NCHI za Afrika zimetakiwa kuweka sheria za kudhibiti na kutunza mazingira katika maeneo nyeti ya bahari ili kuzinusuru na wimbi la uchafuzi wa mazingira unaotokana na vyombo vya baharini.
Waziri wa Miundombinu Hamad Masoud Hamad, alieleza hayo jana katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Ocean View alipokuwa akifungua warsha ya siku tatu ya kimataifa iliyozungumzia utunzaji wa maeneo nyeti ya bahari.
Alisema Zanzibar haina rikodi mbaya ya uchafuzi wa mazingira kupita, bali ni wajibu wa serikali kuchukua tahadhari za hali ya juu na kudhibiti uharibifu wa mazingira usitokee hasa kwa meli zinazoingia na kutoka bandarini.
"Kinga ni bora kuliko tiba, ni vizuri tukichukua tahadhari mapema kabla uchafuzi haujatokea", alisema waziri huyo.
Alisema ajali zinazotokea baharini zinachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira hasa kumwagika kwa mafuta kutoka kwenye meli hizo, hali ambayo huharibu mfumo wa maisha ya viumbe wa baharini (ecosystem) wakiwemo samaki na mazalio yao.
Akizungumzia suala la kuzama kwa meli juu ya uchafuzi wa mazingira waziri Masoud alisema ni vizuri meli zilizozama kuopolewa hata kama hazitotumika tena ili kuwanusu samaki kuhama maeneo yao ya awali na kuanzisha makaazi mengine hali itakayopelekea uhaba wa samaki.
Alisema uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya bahari unagharimu maisha ya watu na uchumi ikiwemo utalii, pamoja na kuathiri maisha ya viumbe wa baharini ambao ni tegemeo la wananchi katika mahitaji ya kila siku.
Nae Mkurugenzi wa Usafiiri wa Maji na Nchikavu (SUMATRA), King Chiragi alisema ni vyema nchi za Afirika kujadili mambo muhimu yatakayosaidia kuzuwia uchafuzi wa mazingira katika maeneo nyeti ya bahari yaliYotengwa ili kulinda usafiri wa meli.
Alisema meli zinazozama kina kirefu cha maji hatua zichukuliwe dhidi ya mafuta yanayokuja juu ili kunusuru uharibifu wa bahari na fukwe.
Nae mwakilishi kutoka Jumuiya ya kimataifa ya usafiri wa maji IMO, alisema jumuiya yake imekuwa ikishiriki vizuri na kutoa michango juu ya utunzaji wa mazingira katika maeneo ya bahari.
Alisema warsha huyo itaibua hisia muhimu zitakazotoa mchango mkubwa katika nchi zao kutokana na kubadilishana mawazo baina yao.
Semina hiyo iliwashirikisha nchi 14 zikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Comoro, Ethiopia, Malawi, Mauritius, Mozambique, Namibia, Seychelles, Madagascar na Afrika Kusini.
No comments:
Post a Comment