Na Khamis Mohammed
JAJI Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, amesema Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), ni sehemu muafaka ambayo migogoro inayohusiana na utekelezaji wa itifaki ya soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki, inaweza kushughulikiwa.
Jaji Makungu aliyasema hayo jana, alipofungua mafunzo maalum kwa watendaji wa EACJ kuhusu masuala ya itifaki ya soko la pamoja ya EAC, yaliyofanyika hoteli ya Zanzibar Beach Resort.
"Hivi sasa ni muda muafaka kwa watendaji wa mahakama hiyo kuwa na elimu ya kutosha juu ya utatuzi wa migogoro inayotokana na utekelezaji wa itifaki hiyo", alisema Jaji Mkuu.
“Naamini kwamba utekelezaji wa itifaki ya soko la pamoja itasababisha migogoro mengi zaidi itakayofikishwa EACJ na wakati mtangamano wa EAC unaimarika zaidi, kuna haja mamlaka ya EACJ kupanuliwa zaidi”, alisisitiza.
Alisema kwa vile itifaki ya soko la pamoja inatoa uhuru na haki kwa wananchi kutoka nchi wanachama na kwamba inatoa haki ya kudai haki hizo zinapovunjwa, EACJ ni chombo muafaka ambacho wananchi hao watakimbilia.
Aidha, Jaji Makungu, alisema, itafiki hiyo itatoa changamoto mbalimbali kwa wananchi wanachama wa jumuiya ya EAC, hivyo wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wakaielewa itifaki hiyo.
Wakati huo huo, Majaji hao wa EACJ, wametoa rambirambi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufuatia maafa ya kuzama kwa meli ya MV.Skagit yaliotokea wiki iliyopita na kusababisha vifo vya watu kadhaa.
Walisema, maafa hayo yanawagusa wananchi wote wa Afrika Mashariki kutokana na ukaribu na udugu uliopo baina ya watu wa mataifa hayo yanayounda EAC.
"Kwa nianba ya EACJ, tunatoa pole kwa wafiwa wote na serikali kwa ujumla juu ya tukio hilo lililogusa nyoyo za wananchi wote", alisema, Rais wa EACJ, Harold Nsekela.
No comments:
Post a Comment