Husna Mohammed na Mwanajuma Mmanga
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zazibar Balozi Seif Ali Iddi, amesema serikali itazifanyia mapitio sheria zinazohusu usafiri wa baharini ili kuepusha majanga ya ajali yanayojitokeza.
Balozi Seif alieleza hayo jana katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo mjini haka alipokuwa akitoa taarifa ya serikali kufuatia kuzama kwa meli ya Mv. Skagit, Jumatano iliyopita.
Balozi Seif alisema sheria za vyombo vya usafiri wa baharini zitapitiwa ili kuweka viwango vya aina ya meli zitakazoruhusiwa kuingizwa nchini kwa ajili ya kubakia abiria.
Mbali ya hatua hiyo, Balozi Seif alisema serikali inaendelea na juhudi za kununua meli zake ambazo zitaweza kutoa huduma ya usafiri wa abiria na mizigo kwa wananchi wa maeneo ya mwambao.
Alifahamishisha kuwa tume itaundwa kuchunguza sababu za kuzama kwa meli karibu na kisiwa cha Chumbe ambapo watu 78 wamepoteza maisha yao.
Alisema watu 146 wameokolewa ambapo taarifa zinaonesha kuwa kati ya hao kulikuwa na raia wa kigeni 17 ambapo waliokolewa kati ya hao ni 15 mmoja amefariki na mwengine hajulikani alipo.
Alisema kwa mujibu wa fat-wa iliyotolewa na masheikh, maiti zitakazo okotwa zitalazimika kwenda kuzikwa katika eneo la Kama lililotengwa na serikali.
"Kwa wakati huu imeamulika maiti zilizokuwa hazjijapatikana kuanzia sasa zitapelekwa moja kwa moja katika eneo la Kama kwa ajili ya mazishi", alisema.
Balozi Seif aliwataka wananchi wote wenye uhakika wa kupotelewa na jamaa zao ambao wanasadikiwa kupanda meli hiyo kutoa taarifa kwa masheha, wakuu wa Wilaya na hata vituo vya polisi vilivyo karibu nao.
Alisema jitihada za kuitafuta meli hiyo zinaendelea kwa kutumia wataalamu wa uzamiaji kutoka kikosi cha KMKM, Jeshi la Wananchi, Polisi pamoja na wazamiaji wa kujitolea wa Ki-Israel waliopo Nungwi.
Alisema wazamiaji hao wamefika umbali wa 48 chini ya bahari lakini bado hawakufanikiwa kuiona meli hiyo na kueleza kuwa jitihada zinaendelea.
Wakati huo huo, Mwanajuma Mmanga anaripoti kuwa maiti watano waliokotwa jana katika kisiwa cha Chumbe, idadi ya miili hiyo iliyookotwa inafanya jumla ya maiti kufikia 78.
Miongoni wa maiti hao mmoja wa miongoni ni Suleiman Pandu Jape ambaye ni sajenti wa JWTZ na ametambulika kufuatia kukutwa na kitambulishi kwenye mfuko wake wa suruali.
Aidha katika maiti hao mwengine alikutwa akiwa na kibunda cha shilingi 167,000 pamoja na simu ya mkoni.
Ofisa wa habari wa jeshi la polisi Zanzibar Mohammed Muhina alisema kuwa ni vyema watu wakatembea na vitambulisho kutokana na kutambulika kwa urahisi.
Nae Daktari kutoka hospitali ya Mnazi Mmmoja Msafiri Marijani ambae maratu baada ya uchunguzi wa maiti hao katika kipimo cha DNA aliyekuwa akichunguza maiti hao na kuenda kuzikwa mmoja mmoja katika makaburi ya serikali.
No comments:
Post a Comment