Habari za Punde

Balozi Maajar: Zanzibar Itangaze Nje Utalii wake


Na Hassan Hamad, OMKR
BALOZI wa Tanzania nchini Marekani, Mwanaidi Maajar amesema Zanzibar inaweza kupiga hatua katika kukuza sekta ya utalii iwapo itaimarisha miundombinu ya uwekezaji katika sekta hiyo.

Balozi Maajar, alieleza hayo jana alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad huko nyumbani kwake Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Alisema katika kukuza sekta hiyo ni lazima serikali itenge fungu maalum litakalokidhi haja ya kuimarisha miundombinu ya utalii, ikiwa ni pamoja na kuitangaza sekta hiyo katika nchi za nje.


“Ni lazima serikali ikubali kutenga fedha nyingi kwa ajili ya kuutangaza utalii, sambamba na kuwekeza katika maeneo ambayo yanaweza kuwavutia watalii”, alifafanua Balozi Maajar.

Alisema kuwa Zanzibar ina vivutio vingi vya utalii vikiwemo mashamba ya viungo, na kwamba iwapo vitatumiwa vizuri vinaweza kuwavutia watalii wengi zaidi na kuinyanyua Zanzibar kiuchumi.

Kuhusu kilimo, Balozi Maajar aliishauri serikali kuandaa programu zinazolenga kuendeleza kilimo na kuzituma kwa taasisi zinazojihusisha na kilimo nchini Marekani, ili ziweze kutoa msukumo katika kilimo hasa cha umwagiliaji.

Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, alisema kwa sasa serikali imeweka mkazo katika kuiendeleza sekta ya utalii ambayo inatoa mchango mkubwa katika upatikanaji wa fedha za kigeni.

Alisema malengo ya serikali ni kufikia watalii milioni moja katika kipindi cha miaka 10 ijayo, na kuelezea haja ya kuimarisha miundombinu na soko la utalii nchini.

Kwa upande mwengine Maalim Seif amesema serikali inaangalia uwezekano wa kuweza kushirikiana na jumuiya za kimataifa katika kukabiliana na wimbi la uingizaji wa dawa za kulevya nchini.

Alifahamisha kuna uwezekano kwamba baadhi ya dawa zinaingizwa Zanzibar kama njia ya kupitishia dawa hizo kwenda nchi nyengine, lakini baadhi ya wafanyabiashara wakorofi wamekuwa wakitumia ujanja kuziingiza dawa hizo na kuwaathiri vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.

Makamu huyo alisema Zanzibar na Marekani zimekuwa na ushirikiano mzuri na kuipongeza misaada mbali mbali inayolewa na nchi hiyo kwa Zanzibar ambayo inasaidia kutatua kero za wananchi na kusaidia mipango ya maendeleo.

Alisema Marekani imekuwa ikitoa misaada mbali mbali hasa katika sekta ya elimu, na kuiomba nchi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika mipango yake ya maendeleo na kukuza uchumi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.