Na Masanja Mabula, PEMBA
MWANAFUNZI wa darasa la saba skuli ya msingi Uwondwe
shehia ya Mtambwe kaskazini wilaya ya Wete, Ruwaida Khamis Muhusini (17)
amelazwa katika hospitali ya Wete akidaiwa kunywa sumu kutaka kujiua baada ya
kubainika kuwa na ujauzito.
Akizungumza na Zanzibar Leo, akiwa katika wodi alikolazwa,
mwanafunzi huyo, alisema kuwa uwamuzi wa yeye kutaka kujiuwa ni baada ya
kuhojiwa na wazazi wake juu ya ujauzito huo ambapo aliona aibu kutokana na
kitendo hicho.
Alisema wazazi wake walitaka kujua kuhusiana na mimba
hiyo ambapo alihojiwa na kumtaja aliyempa ujauzito, lakini wazazi wake
hawakuonesha kama wana hasira kutokana na hali
hiyo.
“Nimekunywa sumu ya panya nikiwa na lengo la kutaka
kujiuwa baada ya wazazi kunibaini kuwa nina ujauzito, niliona aibu na
uwamauzi huu niliuchukua baada ya baba kwenda msikitini kusali sala
la alfajiri”, alifahamisha.
Naye mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Mariam Haji Shehe
alisema kuwa mwanawe alihojiwa na baba yake juu ya ujauzito huo, lakini
hakukuwa na hali yoyote ya kutaka kumpa adhabu.
“Baba yake alimhoji na hakuchukua hatua nyingine kwani
alikuwa anaandaa utaratibu wa kumpa aliyehusika na kitendo cha kumpa mimba
mwanawe, lakini cha kushangaza mtoto alichukua uamuzi wa kutaka kujiuwa na
bahati nzuri walimuwahi na kumpa maziwa ili kuuwa sumu”, alisema.
Daktari aliyempokea mgonjwa huyo, Hamad Mohammed
Nassor wa hospitali ya Wete alisema uchunguzi wa kitaalamu umebaini kuwa
mwanafunzi huyo ana ujauzito wa zaidi ya miezi mitatu.
Alisema kuwa tofauti na wakati wanampokea hali yake
kiafya inaendelea vyema ambapo ameshapatiwa huduma zinazostahili lengo ni
kuokoa maisha yake.
Kwa
upande wake ofisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Wete, Horuob
Suleiman Hemed alikiri kupokea taarifa za mtoto huyo na kuahidi kufuatilia
ili kuhakikisha kuwa muhusika aliyempa mamba hiyo anatiwa mikononi mwa
vyombo vya sheria.
Hata hivyo alielezea wasiwasi wake kwa vyombo hivyo
kutokana na mapungufu ya ufuatiliaji wa kesi za udhalilishaji wa watoto
sambamba na jamii nayo kuwa rushwa muhali jambo ambalo linakwamisha juhudi za
kutokomeza vitendo hivyo.
Taatifa zilizopatikana zinaeleza kuwa kijana aliyehusika
na kumpa ujauzito mwanafunzi huyo anaishi kisiwani Unguja katika maeneo ya
Kibweni.
No comments:
Post a Comment