Habari za Punde

Barua Kutoka Muwaza Kwenda Jumiki - Uamsho


                                                                                                                                    04/07/2012


Kwa Uongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu( JUMIKI)

S.L.P  1266

Mkunazini-Zanzibar




Assalama Aleikum,
Kuhusu:  MUWAZA inapongeza Msimamo wa JUMIKI kushiriki katika Mkakati wa zoezi la kutunga Katiba Mpya



Kwa niaba ya Wanachama wa Jumuiya ya Mustakbal wa Zanzibar (MUWAZA), Muungano wa Wazanzibari ng'ambo, tunaipongeza Jumuiya ya JUMIKI kwa uamuzi wa kijasiri na kishujaa wa Viongozi wake kushiriki pamoja na Wazanzibari wenziwao wote katika mchakato wa kutafuta katiba mpya ya Tanzania na kukataa katakata suala zima la kususia zoezi hilo. MUWAZA inakubaliana kwamba ususiaji wa namna yeyote wa zoezi hilo utatoa mwanya unaotakiwa na Watu wasioitakia mema Zanzibar, na ambao wanaweza kuutumia mwanya huo kujifanya wao ndio wasemaji pekee halali wa Wazanzibari. Ni kushiriki kwa wingi na kikamilifu katika kutoa maoni mbele ya tume hiyo ya Jaji Warioba ndipo wananchi wa Zanzibar wataweza kudhihirisha hadharani chaguo gani wanalitaka kuhusu mustakbali wa maisha yao ya baadae ndani ya Zanzibar. Hii ni fursa nzuri na ya nadra ambapo Wazanzibari wataweza kurejesha heshima ya nchi yao na ya Viongozi wao.


Hata hivyo, MUWAZA inawashauri Viongozi wa JUMIKI, kama inavowashauri ndugu zetu Wazanzibari, kwamba fursa hii ya mchakato wa katiba mpya itumike kwa amani na ustaarabu wa kizanzibari unaothaminiwa duniani kote wa kustahamilia kila mmoja wetu maoni ya mwenzake, hata kama hakubaliani nayo, kikubwa kabisa ni kuweka maslahi ya juu kabisa ya visiwa vya Zanzibar na wengi wa  watu wake.

MUWAZA, kama ilivyo JUMIKI, pamoja na Wazanzibari wote wanaopenda amani na maendeleo ya visiwa vyao, kwa nguvu zote unapinga kabisa matumizi ya nguvu na mabavu dhidi ya wananchi, bila ya kujali kama vitendo hivyo vinafanywa na taasisi za dola, vyama vya kisiasa, jumuiya yeyote au mtu mmoja mmoja binafsi. Tunasisitiza haja ya vyombo vya dola, Vyama vya kisiasa, Jumuiya za kiraia na Wananchi kwa jumla kutetea na kuheshimu amani ya nchi, uhuru wa watu wote kuweza kutoa maoni yao na kukusanyika kwa njia huru, bila ya vizuwizi na vikwazo, mradi wanaambatana na sheria na kulinda amani.

MUWAZA inaamini zoezi la kuwaelimisha Wananchi juu ya haki zao za kikatiba na kuwazindua juu ya sheria ambazo hazitekelezwi vilivyo kama ilivokusudiwa, hivyo kupelekea wananchi kukandamizwa na kupoteza haki zao za kimsingi, ni harakati endelevu isiokuwa na kiwango cha wakati na kipindi. Hivyo, tunakubali kwamba ni juu ya dola kuweka mazingira mazuri kwa  jambo hilo kufanyika. Ni imani ya MUWAZA kwamba wananchi wanapozidi kuwa na mwamko zaidi wa kutambua haki zao na kuelewa namna ya kuzipigania kwa njia ya amani, pamoja na kuelewa namna nchi yao inavotawaliwa na inavofaa kutawaliwa siku za mbele ni faida kwa nchi yetu na maendeleo yake.

MUWAZA inakubaliana nanyi kwamba kuna mambo kadha ya dhuluma ndani ya Muungano, kama ulivo sasa, kwamba Muungano huo umekuwa zaidi wa kiserikali. Hivyo iko haja ya kuuimarisha zaidi Muungano wa Kijamii na kuondosha dhuluma zilizokuweko mnamo miaka 48 iliopita.

Kama ilivyo JUMIKI, MUWAZA imelikaribisha kwa  tamko la Mheshimiwa Jaji Warioba alilolitoa mbele ya Waandishi wa habari alipoizindua Tume ya kukusanya maoni juu ya katiba mpya mjini Dar es Salaam tarehe 18/06/2012 kwamba maoni yote yataheshimiwa na kuzingatiwa, likiwemo suala la Muungano ambalo kwa Wazanzibari ndilo suala muhimu.

Pia MUWAZA inatarajia, kutokana na watu waliomo ndani ya Tume ya Jaji Warioba, kwamba uadilifu, haki na uwazi utaoneshwa katika zoezi la kukusanya maoni ya Wananchi, maoni ya wananchi walio wengi yataheshimiwa na tume na baadae na Serikali ya Muungano wa Tanzania na ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.Tunaitarajia Tume ya Warioba na Serikali zote mbili zitahakikisha watu wanatoa maoni yao bila ya kutishwa waseme nini mbele ya Tume, kwamba hawataadhibiwa kwa namna yeyote juu ya usalama na ajira zao baada ya kutoa maoni yao mbele ya tume. Tunawahimiza Wazanzibari waseme wazi, tena kwa midomo mipana, pindi wanatiwa hofu ya aina yeyote wakati wa zoezi hilo.

Kama ilivyo JUMIKA, MUWAZA inatoa mwito kwa Wazanzibari wote waungane kwa kauli moja ya kurejesha heshima ya rais wa Zanzibar na nchi yao, na kwamba chimbuko la mamlaka maisha libakie  ndani ya mikono ya wananchi.

MUWAZA inapinga vikali vitendo vyovyote vya kuwabeza Wazanzibari wanaopinga mfumo ulioibakisha nchi yao nyuma kwa miaka na kuwabakisha wananchi wake wengi katika ufukara na maendeleo duni katika nyanja za elimu, afya na huduma nyingine za kijamii.

Tunawatakia Wazanzibari kila la kheri, amani na maendeleo, na hayo yatafikiwa tu ikiwa wenyewe Wazanzibari, katika mazingira yalio huru na ya amani, watafanya maamuzi sahihi kwa pamoja katika kipindi hiki muhimu cha historia ya nchi yao.

Iiishi Zanzibar.




Mwenyekiti
Jumuiya ya MUWAZA
UK

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.