Habari za Punde

Chukueni Wanafunzi Wanaofundishika-Kificho

Na Khamis Amani


UONGOZI wa Chuo cha Zanzibar School of Health, umepewa changamoto ya kuchukua wanafunzi wenye sifa ya kuweza kufundishika, ili waweze kutoa huduma nzuri wamalizapo masomo.

Umefahamishwa kuwa haitakuwa sahihi hata kidogo Chuo hicho kikachukua wanafunzi ambao wameshindwa katika afya ya wananchi, au kufikia kiwango kilicholengwa katika malengo ya milenia.

Wito huo umetolewa na Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho, katika hafla ya ufunguzi wa Chuo hicho zilizofanyika Mombasa nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Spika Kificho alisema kuwa, fani ya afya ni muhimu katika jamii na inahitaji wataalamu wakubwa wenye sifa, ili waweze kutoa huduma nzuri zenye upendo na heshima kubwa kwa wagonjwa.

"Umuhimu wake unakuja kwa sababu wataalamu wa afya ni watu ambao watakuwa wanashughulika na afya za binaadamu, mnapofika kushughulika na afya za watu, jambo hilo halitaki kubahatisha", alifahamisha.

Katika ufunguzi huo, Kificho ameupongeza uongozi wa Chuo hicho, kwa kujua umuhimu wa afya za binaadamu na kuwa na wazo la kukianzisha, hatua ambayo ni ya kiazalendo na inapaswa kuungwa mkono.

"Na ndio maana sikushangaa jwamba Wizara ya Afya na Baraza la Uuguzi walihakikisha kuwa Chuo hichi kinasimama, kutokana na umuhimu wake mkubwa", alisema.

Alisema kuwa, Chuo hicho ni cha kwanza cha binafsi cha hatua ya diploma hapa Zanzibar, na pia ni cha pili kufundisha fani za mambo ya afya zaidi ya kile kikubwa cha Mbweni, ambacho ndicho kulichokuwa kikitegemewa na kwa hakika Chuo hicho hivi sasa kimezidiwa kutokana na hali ya mahitaji.

Alifahamisha chuo cha Afya kina mahitaji makubwa kama vile nursing, clinical officers na na wengineo, n kiasi kinachozalishwa katika chuo cha Mbweni hakiwezi kuendana na mipango ya serikali ya afya ya wananchi wake, au kufikia kiwango kilicholengwa katika malengo ya milenia.

Alisema chuo cha Zanzibar Health ni msaada na baraka kwa Zanzibar, japokuwa pengine hakutatosheleza mahitaji ya afya, lakini kitaweza kupunguza mahitaji kwa kiasi kikubwa kama ambapo imeshaonekana kwa chuo hicho kuweza kuanza na wanafunzi zaidi ya 80.

Aidha amekipingoza chuo hicho kwa mashirikiano makubwa na Chuo cha Afya cha Tumaini kwa kuanzisha fani ya Counselling Pyschology ambayo ilikuwa ikihitajika sana.

"Katika kupanua wigo chuo mna fursa kubwa ya kujipanua kwa njia ya mashirikiano na vyuo mbali mbali na kuendesha kozi mbali mbali kwa niaba ya vyuo hivyo,", alisema.

Aidha ameufahamisha uongozi wa chuo hicho kuwa wakati hivi sasa umefika wa kufanya juhudi ili chuo hicho kitambuliwe na taasisi NACTE, suala ambalo ni muhimu kutokana na chuo hicho kujishughulisha na afya za binaadamu.

Nae Mkuu wa Chuo hicho Dk. Amour Abdallah Amour alisema kuwa chuo hicho kwa mashirikiano na vyuo mbali mbali vya ndani na nje ya nchi, watahakikisha kinakuwa mfano bora kwa nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Madola.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.