Na Hafsa Golo
SERIKALI YA Mapinduzi Zanzibar, imetiliana saini na Kampuni ya Ms United Builders LTD na Kampuni ya Rans Co. LTD kwa ajili ya ujenzi wa skuli mbili za kisasa zitakazojengwa Unguja na Pemba.
Kwa upande wa Serikali ya Zanzibar, imewakilishwa na Katibu Mkuu wa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mwanaidi Saleh Abdalla, ambapo kwa upande wa Kampuni ya Ms United Builders Limited na Mkurugenzi wa Ufundi wa Kampuni hiyo, Anolo Kileo ambapo kwa upande wa Kampuni ya Rans Co Ltd imewakilishwa na Nassor Salim Miskry.
Hafla ya utiliaji saini huo umefanyika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali iliyopo Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar ambapo dola za kimarekani 6,600,000 zitatumika katika ujenzi huo.
Akizungumza baada ya uwekaji wa saini hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abdalla Mzee, alisema skuli hizo kwa upande wa kisiwa cha Pemba itajengwa katika kijiji cha Mkanyageni wilaya ya Mkoani Pemba na kwa upande wa Unguja skuli kama hiyo itajengwa katika kijiji cha Kibuteni Mkoa wa Kusini Unguja.
Alifahamisha kuwa ujenzi huo utakuwa wa ghorofa ambao utajumuisha madarasa 16, maabara mbili, chumba cha Kompyuta kimoja, nyumba za walimu, dakhalia moja ya wanawake, jengo la utawala pamoja na maktaba moja.
Naibu Katibu Mkuu huyo, alisema kila skuli kiwango ambacho kwa upande wa skuli ya Kibuteni itagharimu shilingi 3,945,229,420 bila ya ongezeko la thamani VAT ya shilingi 710,141,295.60 ambayo itajengwa na Kampuni ya Ms United Builders Limited ya Dar es Salaam ambapo watajenga Skuli ya Kibuteni iliyopo Unguja.
Kwa upande wa ujenzu wa skuli ya Pemba itajengwa katika kijiji cha Mkanyageni ambayo itajengwa na Kampuni ya Rans itagharimu 4,697,648,200 bila ya ongezeko la VAT ya shilingi 845,576,676.
Abdalla alisema ujenzi wa skuli hizo unatarajiwa kuanza Ogasti 28 mwaka huu na kukamilika Oktoba 19, 2013 kwa skuli ya Kibuteni Unguja na Pemba katika kijiji cha Mkanyageni ujenzi wake utakamilika Julai 31, 2013.
Wawakilishi wa Kampuni hizo, waliahidi kutekeleza masharti ya ujenzi wa skuli hizo sambamba na kukamilisha kwa wkati unaotakiwa.
Pia walihakikisha bajeti ya Fedha hizo zinatumika kama ilivyokusudiwa ili kuona hakuna vikwazo katika ujenzi wa skuli hizo.
Nae Waziri wa Elimu Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamhunna aliwataka kuonesha uzalendo katika kutekeleza ujenzi huo, na wafanye kazi kwa ushirikiano ili ikitokea changamoto walitatue kwa pamoja.
Na kwa upande wa Mwakilishi wa majimbo hayo Haroun Ali Suleiman wa Makunduchi na Haji Faki Shaali jimbo la Makanyageni, waliwataka wakandarasi hao kuzingatia uzalendo katika utendeji wa kazi hiyo.
Walisema kuwa kuna wajuzi wa fani mbali mbali katika majimbo hayo hivyo ni vyema kuwatumia ipasavyo.
“Wapeni ajira watu wanaoishi maeneo ya karibu kuna wataalamu wa kila fani ikiwemo fundi umeme,maji, vibarua “alisema Haroun.
No comments:
Post a Comment