Habari za Punde

Rashid Seif Apongezwa kuteuliwa Waziri na Wazanzibari waliopo Diaspora



       Tunakutakia kazi yako  iwe nyepesi na rahisi
        Usafiri wa anga pia utafutiwe ufumbuzi
       The International Airlines of Zanzibar (IAZA) izaliwe

Na Geofrey Kimbitikiri

Wazanzibari waishio nje ( wana diaspora)  na ambao jamaa zao walipoteza maisha yao na wengine kuathirika katika msiba wa kuzama  boti ya MV Skagit wamejitokeza, kwa kumpa mkono wa hongera waziri mpya wa Mawasiliano na Miundombinu Bw. Rashid Seif, pale walipopeleka barua pepe kwa Wagagagigikoko News Network (WANENE).

"Tunampongeza Mhe Rashid Seif kwa kuikubali kazi hii ngumu kwa moyo mkunjufu hasa kwa wakati huu mgumu. Sisi sote Wazanzibari tunaoishi nje tunamtakia waziri mpya kila la kheri katika kazi yake hii ngumu  na Mola amsaidie ili iwe nyepesi na rahisi", walielezea Wazanzibari hao.


"Pamoja na hongera zetu tunamuomba waziri Rashid Seif aangalie pia usafiri wa anga kwa umakini na kwa jicho la karibu zaidi. 

Tunajua  baadhi ya ndege za charter zinazokuja Visiwani zinasajiliwa Bara, lakini madamu wanatumia anga na uwanja wetu ni lazima utendaji wao wa kazi utizamwe vizuri ili usije kutuathiri huko mbele", waliendelea Wazanzibari hao.

"Wengine tuliwahi kupanda charter kuenda Dar ambayo kioo kilikuwa kimevunjika na upande wa ubao ulikuwa umepachikwa. Hii ni hatari na hatujui ndege kama hii vipi iliruhusiwa kupaa angani. 

Safety equipments kwenye ndege na kwenye airport yetu ya Zanzibar pia ziangaliwe, ili tuwe tayari kwa lolote lile", waliendelea Wazanzibari hao. 

Walisisitiza tuliwahi kuona siku za nyuma yakifanyika mazoezi eneo la bandari (Malindi) kama kungelitokea ajali ( Drill) lakini hatujawahi kuona hata mara moja mazoezi ya aina hii kufanyika viwanja vyetu vya ndege ili kuangalia uwezo wetu na kasoro zetu kukabiliana na ajali za aina hii.

"Mhe Rashid, sisi Wazanzibari tuliopo nje tupo nyuma yako na tupo tayari kununua hisa kama Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaanzisha kampuni ya Taifa ya ndege na kuanza japokuwa kwa ndege moja ya kuaminika ili shida na usumbufu wa wananchi wanaosafiri kwa anga uondolewe pia. 

Ahadi hii iliwahi kutolewa huko nyuma kwamba na Makamu wa kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad kwamba Zanzibar iwe na shirika lake la ndege.

Wenzetu Ethiopian Airlines walianza kidogo kidogo hivi hivi na leo ni shirika la ndege la Afrika ambalo wengi wa wanadiaspora huwa tunalitumia tunaposafiri kuja nyumbani na sehemu nyengine za dunia.

Japokuwa nia iwe ni kuwa na 'The International Airlines of Zanzibar (IAZA)' lakini tunaweza kuanza na ndege ndogo ambazo zitaruka kati ya Unguja, Pemba na Tanzania Bara", walimalizia Wazanzibari hao kwenye barua yao pepe.

Source: Wagagagigikoko News Network (WANENE)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.