HOTUBA YA MWENYEKITI WA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA UTAWALA YA BARAZA LA WAWAKILISHI,ZANZIBAR KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA AFISI YA RAISI UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013.
Mheshimiwa spika, awali ya yote, ninaaza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Azza wa Jalla kwa kutujaalia uhai na afya njema na kuweza kufika hapa na kuendelea na kazi ya kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya mwaka wa fedha 2012/2013 kwa Wizara za Serikali na Mashirika yake na leo hii tukiwa tunaijadili na hatimae kuiidhinishia Wizara ya nne kati ya Wizara kumi na sita za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, pili napenda kuendeleza shukrani zangu za dhati kwako wewe binafsi kwa kuniruhusu nitowe maoni kwa niaba ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala na pia kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mfenesini. Aidha, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa heshima na busara zake za kuiongoza nchi yetu ya Zanzibar, kwa kuheshimu misingi ya Utawala Bora.
Mheshimiwa Spika, naomba pia nimshukuru Mheshimiwa Waziri na Watendaji wake wote wakiongozwa na Katibu Mkuu kwa kutekeleza malengo waliyojipangia pamoja na majukumu yao kwa bidii kubwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/2012, lakini pia, kwa mashirikiano yao makubwa waliyotupatia wakati tulipopitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya mwaka wa fedha 2012/2013.
Mheshimiwa Spika, nitakuwa sikutenda haki ikiwa sitowashukuru Wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala ya Baraza la Wawakilishi kwa ushirikiano wao waliouonesha wakati wote ambao Kamati ilikuwa inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Kifungu cha 88 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Kanuni ya 113 ya Kanuni ya Baraza la Wawakilishi, Toleo la mwaka 2012 kwa lengo la kuimarisha utendaji na kukuza uwajibikaji katika Serikali.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwatambua Wajumbe hao kwa kuwataja kama ifuatavyo:-
1. Mhe. Ali Abdalla Ali – Mwenyekiti
2. Mhe. Panya Ali Abdalla – Makamo Mwenyekiti
3. Mhe. Ismail Jussa Ladhu – Mjumbe
4. Mhe. Mussa Ali Hassan – Mjumbe
5. Mhe. Mtumwa Kheir Mbarak – Mjumbe
6. Mhe. Suleiman Hemed Khamis – Mjumbe
7. Mhe. Wanu Hafidh Ameir – Mjumbe
8. Mhe. Mohammedraza Hassanali Mohammedal – Mjumbe
9. Ndg. Nasra Awadh Salmin – Katibu
10. Ndg. Abubakar Mahmoud Iddi – Katibu
Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi na shukurani hizo napenda sasa nitoe maoni ya Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kama ifuatavyo:-
IDARA YA MIPANGO, SERA NA UTAFITI
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala inaipongeza Idara hii kwa kuwa na lengo la kuimarisha mfumo wa teknoloji ya habari na mawasiliano Serikalini (e – Government). Hii ni hatua muhimu iliyokusudiwa kutoa nafasi kwa Viongozi, Watumishi wa Umma na wananchi kwa ujumla katika kuharakisha mawasiliano pamoja na kupata taarifa mbali mbali.
Mheshimiwa Spika, Kamati yako inaomba kuwasilisha mbele ya Baraza hili sikitiko lake dhidi ya Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo ya kutokuipatia Kamati hii gharama halisi zitakazotumika kwa mradi huo tokea kuanza kwake hadi kumalizika kwake na gharama kwa kila ‘component’ kwa kuwa mradi huu unajumuisha Wizara nyingi, baada ya Watendaji waliokuwepo Afisini pale kushindwa kutupatia gharama hizo na badala yake walituelekeza kwamba gharama hizo tutazipata Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo.
Kwa mnasaba huo, Kamati yako kupitia barua yenye kumbukumbu BLW/K.10/4 VOL.I/2 ya tarehe 16 Mei, 2012 iliiomba Ofisi hiyo itupatie gharama hizo ili zitusaidie katika kutelekeza majukumu yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa huzuni natamka kwamba hadi nawasilisha hotuba hii gharama hizo hatujapatiwa. Kwa kuwa Wajumbe wako wana haki ya kupewa taarifa mbali mbali wanazozihitaji kwa mujibu wa kifungu cha 9 cha Sheria Namba 4 ya mwaka 2007 tunaiomba Ofisi hii itoe taarifa hizo katika Baraza hili, ili Waheshimiwa Wawakilishi na Wananchi ambao ndio walipa kodi wajue.
IDARA YA NYARAKA NA KUMBUKUMBU ZA TAIFA
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu inaishukuru Serikali kwa kuipatia Idara hii baadhi ya vitendea kazi zikiwemo kompyuta. Hii ni kutokana na kuwa hapo kabla Idara hii ilikuwa na kompyuta moja tu inayofanyakazi, jambo ambalo ni kinyume au haliendani na majukumu mazito ya Idara hii.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa ina jukumu la kutunza na kuhifadhi nyaraka mbali mbali za Taifa, Kamati hii inawaomba Watendaji wa Idara hii kupanga vipaombele vyeo kwa kuzingatia majukumu yao.
Mheshimiwa Spika, tunashauri hili baada ya kubaini kuwa Watendaji wa Idara hii hubaki afisini kwa takriban miezi sita bila ya kuwa na shughuli yoyote na hupokea mishahara bure kutokana na ukosefu wa vitendea kazi zikiwemo dawa za kuhuwishia nyaraka.
Kwa kuwa Zanzibar inasifiwa katika kuhifadhi nyaraka zake duniani ni vyema sifa hii tukaienzi ili tusigeuke Wagema.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa jengo la Idara hii ni dogo na limezungukwa na nyumba za wananchi na hata Idara hii kudiriki kutumia mlango mmoja na raia, na kwa kuwa wamiliki wa nyumba hizo wamehitaji kiwango kikubwa cha fedha ikiwa ni fidia ya kuliachia eneo hilo Serikali.
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala inaishauri Serikali kubadilisha miundombinu ya jengo hili ili mmiliki wa nyumba hiyo asitumie mlango huo kwa lengo la kuimarisha usalama wa Idara hii.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo Kamati yetu imebaini kuwa baadhi ya eneo linalomilikiwa na Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa limechukuliwa na wananchi na tayari wamejenga majengo yao.
Kwa kuwa wananchi hao wamelitumia eneo hilo kwa zaidi ya miaka 12 na kwa kuwa Sheria za ‘Common Law’za Ardhi zinamruhusu mtu aliyetumia ardhi kwa zaidi ya miaka hiyo kuendelea kutumia ardhi hiyo, ingawa itakuwa inamilikiwa na mwenye ardhi.
Kamati yetu inaishauri Idara hii kufuatilia zaidi suala hili katika Afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kupata zaidi ushauri wa kisheria.
Aidha, tunaishauri Serikali kutafuta eneo jengine kwa lengo la kujenga ofisi mpya ya Idara hii itakayoendana na hadhi na majukumu ya Idara.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kadhia hiyo Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala inaiomba Serikali kuwa makini na maeneo yake ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.
Mheshimiwa Spika,Kamati yetu iliripotiwa kuwa Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa kwa upande wa Pemba imeliomba jengo la zamani la Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake ili shughuli za Idara hii ziendelee kutekelezwa kwa ufanisi zaidi, kwani jengo wanalotumia hivi sasa (ambalo ni ndani ya Ngome Kongwe ya Chake Chake) halitoshi na pia, mazingira yake si mazuri kwa hifadhi ya nyaraka.
Mheshimiwa Spika, baada ya Kamati yetu kufuatilia hili tulielezwa kuwa mazungumzo bado yanaendelea baina ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapiunduzi na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Kwa kuwa muda mrefu umepita na maamuzi hayajatolewa, Kamati hii inaziomba Ofisi mbili hizi kukamilisha mazungumzo hayo haraka iwezekanavyo ili kuzinusuru nyaraka za Taifa ambazo kwa kipindi hiki hazikuhifadhiwa katika mazingira yanayostahiki.
IDARA YA MAFUNZO NA MAENDELEO YARASILIMALI WATU
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri katika kitabu chake cha hotuba katueleza kuwa Idara hii kwa mwaka wa fedha 2012/2013 imepanga kusimamia na kuratibu mafunzo ya Watumishi wa Umma.
Kamati yetu imetiwa moyo na kauli hiyo, hata hivyo, inaishauri Idara ya Mafunzo na Maendeleo ya Rasilimali Watu kuwa makini zaidi wakati wa kutoa nafasi hizo hususan za nje ya nchi kwani baadhi ya Watumishi wanailalamikia Idara hii kuwa inatoa nafasi kwa upendeleo (yaani kwa kujuana) zaidi na sio kwa kumuendeleza kiutendaji Mtumishi huo.
Mheshimiwa Spika, hapa tunamaanisha kwamba nafasi za mafunzo hupatiwa mtendaji ambaye hana taaluma na mafunzo husika au kwa lugha nyepesi sio kada yake, isipokuwa hupatiwa nafasi hiyo kwa kujuana.
Pamoja na hayo, Kamati hii inaishauri Serikali kuweka utaratibu wa kuwaalika Wakufunzi kutoka nje ya nchi kuja kutoa taaluma kwa Watendaji wetu kuliko kuwapeleka huko ili kupunguza gharama zisizo za lazima.
Mheshimiwa Spika, takriban Wizara nyingi za Serikali zinatoa nafasi za mafunzo ya nje ya nchi kwa Watumishi wake bila ya kufuata utaratibu unaoeleweka.
Kwa kuwa Idara hii ndio hasa yenye mamlaka ya kuwashughulikia Watumishi wa Umma kuhusiana na suala la mafunzo. Hivyo, tunaishauri Serikali kuweka utaratibu mzuri wa Idara moja tu kushughulikia suala hili na sio kuendelea na utaratibu unaotumika hivi sasa ambao hauleti tija iliyokusudiwa.
IDARA YA UTAWALA BORA
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu inaipongeza Idara hii kwa kuandaa Sera ya Utawala Bora. Tunalipongeza hili kwani litaiwezesha Idara ya Utawala Bora kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala inaishauri Idara hii kutumia Kamati zake kuchunguza na kufuatilia zaidi mwenendo mzima wa Serikali ili kuweza kupata kipimo cha Utawala Bora na sio kujikita tu katika kuandaa vipindi vya redio na televisheni.
Tunashauri hili baada ya kubaini kuwa Idara ya Utawala Bora bado haijayatambua makujumu yake na inafanya kazi kama Jumuiya Isiyo ya Kiserikali.
Mheshimiwa Spika, tunadiriki kutamka hivyo, baada ya baadhi ya Watendaji wa Idara hii kutamka bayana na kushangazwa na masuala mbali mbali ambayo Kamati yetu inayafuatilia na kuona kuwa hatuna mamlaka ya kufanya hivyo.
Kutokana na hayo Kamati yetu inawashauri Watendaji wa Idara kuitumia Sera ya Utawala Bora kama ni chachu katika kutekeleza majukumu yao kwani Idara hii ina jukumu la kushughulikia Utawala Bora katika Wizara zote.
Aidha, Idara hii inapaswa kufuatilia masuala yote ya ukiukwaji wa misingi ya Utawala Bora katika utendaji wa Serikali na hata Jumuiya Zisizo za Kiserikali.
IDARA YA MIPANGO NA RASILIMALI WATU
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu pia imetiwa moyo na utendaji wa Idara hii kwa kuanzisha zoezi la kuwahakiki Watumishi wa Umma, zoezi ambalo lilibaini mapungufu mbali mbali yakiwemo ya baadhi ya Wizara kutowathibitisha kazi Watendaji wake, mikataba ya ajira kutosainiwa, na mengi mengineyo.
Mheshimiwa Spika, tunawaomba Makatibu Wakuu kupitia Wakurugenzi wa Idara ya Utumishi na Uendeshaji kuwa na utaratibu wa kuyafuatilia majalada ya Watumishi kila baada ya muda fulani, ili kuhakikisha kuwa kila taarifa muhimu inayotakiwa kuwemo katika jalada hilo inapatikana.
Mheshimiwa Spika, aidha, Kamati hii inaishauri Serikali kuanzisha utaratibu wa kuwajazisha mikataba watendaji wanaokwenda masomoni, ili kuwabana wale wote wenye nia ya kuacha kazi au kutafuta kazi katika eneo jengine baada ya kurudi masomoni.
Hatua hii inaweza ikasaidia kuwadhibiti Watumishi wa Umma kuondoka afisini kiholela, pia, itasaidia kuokoa fedha za Serikali zisipotee ovyo.
OFISI KUU PEMBA
Mheshimiwa Spika, Kamati ilipata nafasi ya kutembelea Ofisi Kuu Pemba pamoja na Idara zake inazoziratibu na kujionea hali halisi ya utendaji wake wa kazi kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
Mheshimiwa Spika, kwa kiasi fulani tumeridhika na utendaji wa Ofisi hii ingawa baadhi ya Idara zake zinatekeleza majukumu yake katika mazingira magumu; kwa mfano Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa, lakini kutokana na umakini, ubunifu na umahiri wa Kiongozi wa Idara hii Ndugu Kombo Khamis Bakari basi Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa – Pemba ilifanikiwa kutekeleza malengo yake kwa asilimia kubwa.
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu inazishauri Taasisi za Serikali kufuata nyayo za kijana huyo kwani anafanya kazi kwa kujitolea zaidi na kuweka kando maslahi yake binafsi.
Mheshimiwa Spika, Watendaji wa Ofisi Kuu Pemba waliilalamikia Kamati yetu kwamba endapo Ofisi Kuu Unguja itaandaa shughuli yoyote Pemba inawafanya Watendaji wa juu wa Kitengo husika kuwa kama mwaalikwa wa shughuli hiyo wakati kiuhalisia wao ndio wenyewe.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kasoro hiyo tunashauri kuwe na mashirikiano mazuri baina ya Watendaji hawa ili kuleta tija iliyokusudiwa.
AFISI YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa 35 wa kitabu cha Hotuba ya Mheshimiwa Waziri, tumeelezwa kuwa Afisi hii itaendelea na jukumu la kukagua mahesabu ya Serikali na Taasisi zake kwa kupindi cha mwaka 2011/2012.
Tunaipongeza hatua hiyo, hata hivyo, tunaishauri Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuimarisha Ripoti ya Ukaguzi wanayoitoa kwa kuingiza kipengele kinachohusiana na misamaha ya kodi, kuingiza kipengele kitakachopendekeza maeneo ya kupata mapato na maeneo mengine yatakayosaidia kuonesha maeneo ya uvujaji wa mapato na yale yanayoweza kuongeza mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, tunashauri hili baada ya kugundua kuwa Ripoti za Mkaguzi kila mwaka zinaripoti mambo hayo hayo, jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya nchi. Kwa msingi huo si vibaya kutamka kwamba, ingawa Kamati ya Kuchunguza Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC) miongoni mwa majukumu yake ni kuchunguza na kutoa taarifa juu ya hesabu za mwaka za matumizi ya Serikali na Mashirika yake na hesabu nyengine zozote zitakazowasilishwa mbele ya Baraza la Wawakilishi kupitia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mujibu wa kanuni ya 118(2)(a) ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi, Toleo la mwaka 2012, Kamati yetu imegundua kuwa Kamati ya PAC inatoa taarifa yenye kina zaidi ukilinganisha na ile ya Mdhibiti.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo Kamati yetu inaishauri Afisi hii kukamilisha marekebisho ya Sheria yake kama ilivyoahidi haraka iwezekanavyo ili nchi yetu iande sambamba na nchi nyengine duniani kuhusiana na masuala ya utendaji wa Afisi hii muhimu, kwani muda mrefu umepita bila ya ahadi hiyo kutekelezwa kikamilifu.
Kuendelea kazi hii kusuasua kutaipelekea nchi yetu kushindwa kufuata miongozo inayotolewa katika Maazimio mbali mbali na Jumuiya za Ukaguzi duniani (Lima and Mexico Declaration).
Mheshimiwa Spika, katika kuifanyia marekebisho Sheria hiyo Kamati yetu inapendekeza pamoja na mambo mengine uingizwe pia utaratibu wa kupitishwa kwa bajeti ya Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili tuachane na mfumo unaotumika sasa na badala yake bajeti ya Afisi hii ipitiwe mbele ya Kamati ya Kuchunguza Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC) na kisha kuwasilishwa Baraza la Wawakilishi kwa kuidhinishwa.
Mheshimiwa Spika, utaratibu huu sio mgeni kwani hata wenzetu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanautumia.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Afisi hii inatakiwa kuwa huru katika utendaji wa kazi zake, yaani ifanye kazi bila ya kutegemea msaada wowote kwa wakaguliwa na kwa kuwa Afisi hii ndio msimamizi na mkaguzi wa hesabu za Serikali, Kamati hii inaiomba Serikali iwaongezee maslahi Watendaji wa Afisi hii ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Spika, tunatoa pendekezo hili baada ya kubaini kwamba Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo katika mwaka wa fedha 2011/2012 imewaongezea Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani maslahi yao kwa asilimia kubwa, wakati Afisa anayemkagua Mhasibu huyu analipwa mshahara wa Mtumishi wa kawaida.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba huwezi kumkagua mtu kwa kufuata misingi ya kazi yako ikiwa wewe Mkaguzi maslahi yako ni madogo kuliko unaemkagua.
CHUO CHA UTAWALA WA UMMA
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu imesikitishwa sana na taarifa iliyopewa na Chuo hiki ya kwamba Wizara za Serikali zinashindwa kuwalipia wafanyakazi wake ada ya mafunzo wakati Baraza la Wawakilishi kila mwaka linaidhinisha Kasma 221100 inayohusiana na Gharama za Mafunzo kwa kila Wizara na Idara ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, Chuo cha Utawala wa Umma kupitia wanafunzi wake ambao ni Watumishi wa Umma, kinazidai Wizara za Serikali si chini ya Tsh. 26,433,000/-na Wizara inayoongoza kutowalipia Watumishi wake ni Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, ambayo katika mwaka wa fedha 2011/2012 tuliidhinishia Ofisi hii Tsh. 308,750,000/- kama ni fedha za Mafunzo ya Ndani na Tsh. 245,250,000/- za Malipo ya Ada.
Kauli yetu hii inathibitishwa na ukurasa wa 232 wa Buku la Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Kazi za Kawaida na Maendeleo kwa mwaka 2011/2012 wakati Watumishi wake wanadaiwa na Chuo Tsh. 2,340,000/-.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla deni linalodaiwa Serikali na Chuo kupitia Watumishi wake ni kubwa sana kutokana na uasili ‘nature’ wa Chuo hiki.
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu inaziomba Taasisi za Serikali kukamilisha madeni hayo haraka iwezekanavyo hasa tukizingatia kuwa Chuo hiki kinakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ya ukosefu wa usafiri kwa Mkurugenzi wa Chuo, jambo ambalo linampa usumbufu mkubwa sana Mtendaji huyo.
Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa 44 wa kitabu cha hotuba cha Mheshimiwa Waziri, tumeelezwa kuwa Chuo cha Utawala wa Umma kitaendelea na ujenzi wa Chuo chake huko Tunguu. Mheshimiwa Spika, Kamati yetu haikuridhishwa kabisa na kiwango cha gharama ya fedha kilichotumika hadi hatua ya ujenzi ilivyofikiwa, ingawa hatuna ujuzi‘skill’ wa ujenzi, lakini tunauzoefu wa kutosha kuhusiana na masuala ya ujenzi, kwani kwenye baadhi ya mambo uzoefu unaweza ukatumika na ukakusaidia au ukakuelekeza ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, kutokuridhishwa kwetu huko tunadiriki hata kutamka kuwa, kuna ubadhirifu wa fedha umefanyika. Kamati yetu katika kufuatilia hili, ilijibiwa na Watendaji wa Chuo kwamba kuna baadhi ya gharama hazikuwemo kwenye ‘Bill of Quantity – BOQ’ ambazo pia zilizopelekea kuonekana kutumika kiasi kikubwa cha fedha.
Gharama zenyewe ni pamoja na ujenzi wa kisima. Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu hayo Kamati yako bado haijaridhika na inaiomba Wizara kufuatilia kadhia hii kwa kina hasa tukizingatia kuwa Ofisi hii nayo pia haikuridhika na gharama hizo.
Mheshimiwa Spika, naomba kulikumbusha Baraza lako Tukufu kwamba kabla ya Chuo cha Utawala wa Umma kuwa chini ya Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kilikuwa chini ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na huko ndiko kunadhaniwa kuwa kulifanyika mchezo mchafu.
Mheshimiwa Spika, endapo itabainika kuwa kuna wajanja wamezitumia fedha za wavuja jasho wa nchi hii kinyume na utaratibu, basi Serikali isisite kuwachukulia hatua zinazostahiki Watendaji hao.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wizara hii ina jukumu la kusimamia Utawala Bora, ni imani yetu kwamba suala hili litafuatiliwa haraka iwezekanavyo ili kuzinusuru na Tsh.300,000,000/- tunazomuidhinishia tena Mheshimiwa Waziri kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kazi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kadhia hii na nyengine nyingi ambazo zimesharipotiwa mbele ya Baraza hili, tunaiomba Serikali kwa ujumla kuwa makini na kufuatilia kwa karibu zaidi Matumizi yote ya fedha za Kazi za Maendeleo za Taasisi zake ili kuzinusuru fedha za walipa kodi wa nchi hii pamoja na fedha za Washirika wa Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kifungu cha 7(1)(b) cha Sheria ya Chuo cha Utawala wa Umma ya mwaka 2007 kinatoa mamlaka kwa Baraza la Chuo kusimamia masuala ya fedha na mali nyengine za Chuo baada ya kuidhinishwa na Waziri.
Kamati yetu inaishauri Wizara kuliachia Baraza la Chuo kusimamia ujenzi wa Chuo ili kuzithamini na kuzipa nguvu Sheria zetu tunazozitunga wenyewe. Sambamba na hilo Baraza la Chuo ndio chombo cha karibu zaidi katika kufuatilia changamoto za Chuo.
Hivyo, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti kuendelea kusimamia suala hili ni kinyume na matakwa ya Sheria hii.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala inaunga mkono maamuzi yaliyofanywa na Ofisi hii ya kuipa kazi ya ujenzi Chuo cha Mafunzo baada ya Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo – KMKM kushindwa kulitekeleza hili ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuunga mkono kwetu huko, tunakiomba Chuo cha Mafunzo kufanikisha ujenzi huo mapema iwezekanavyo ili kiweze kutumika kuanzia mwezi huu wa Julai, 2012.
Mheshimiwa Spika, tunashauri hili ili kuondosha usumbufu kwa Watendaji wa Chuo hiki, kwani kwa hivi sasa Chuo cha Utawala wa Umma kinatoa huduma katika mikondo minne kama ifuatavyo; Katika jengo lake la Mizingani, Wanafunzi wanaanza kusoma saa 2:30 asubuhi hadi saa 6:00 mchana na wengine wanaingia saa 10:00 jioni hadi saa 2:00 usiku.
Ama kwa upande wa Wanafunzi wanasoma Skuli ya Hamamni, wanafunzi hao wanaanza kusoma saa 7:30 mchana hadi saa 10:45 jioni na wengine wanaingia saa 11:00 jioni hadi saa 2:00 usiku.
Mheshimiwa Spika, Chuo kuendelea kutumia utaratibu huu ni kwenda kinyume na matakwa ya Mikataba ya Kimataifa inayohisiana na masuala ya Kazi Duniani‘International Labuor Organisation – ILO’ kwani Watumishi wa Chuo hiki hutumia karibu saa 55 kufanya kazi kwa wiki badala ya saa 40 zinazotakiwa.
Sambamba na hilo kumalizika kwa ujenzi wa Chuo hiki kutawaondoshea usumbufu Wanafunzi wake, kwani Rais wa Chuo hiki pamoja na Watendaji wake watapata sehemu ya kufanyia shughuli zao pamoja na kupata sehemu mahsusi ya kutoa huduma ya kwanza ‘First Aid’ endapo mtu atafikwa na ugonjwa wowote kwani mambo haya kwa sasa hayapatikani Chuoni hapo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa baadhi ya Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vinajihusisha pia kwenye masuala ya ujenzi. Tunaviomba Vikosi hivi vitekeleze pendekezo la Baraza la Wawakilishi la kuviandikisha vitengo vyeo vya ujenzi kama Wakandarasi.
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu katika kutekeleza majukumu yake ya kawaida ilielezwa na aliyekuwa Kaimu Waziri wa Ofisi hii ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Mheshimiwa Omar Yussuf Mzee kuwa, Serikali kwa mwaka huu wa fedha imetenga baadhi ya fedha kwa ajili ya kurekebisha kasoro mbali mbali zilizojitokeza kwenye mambo ya mishahara.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo Kamati yetu inaiomba Serikali kuyaangalia kwa kina maslahi ya Wakufunzi wa Chuo cha Utawala wa Umma ili kuwe na uwiano baina ya Vyuo vya Serikali. Kwani imebainika kwamba Chuo hiki Wakufunzi wake maslahi yao yapo chini sana ukilinganisha na Vyuo vyengine.
Mheshimiwa Spika, naomba nithibitishe hili kwa kuiomba Serikali kuangalia Vyuo viwili vya Serikali vya hapa Zanzibar jinsi vinavyowalipa Wakufunzi wao.
Vyuo vyenyewe ni; Chuo cha Habari na Chuo cha Uongozi wa Fedha – Chwaka na baadae ilinganishe na maslahi anayolipwa Mkufunzi wa Chuo cha Utawala Umma.
Mheshimiwa Spika, tunaiomba Serikali kulitekeleza hili haraka iwezekanavyo kwani kwa hivi sasa Chuo kinatumia fedha za Matumizi Mengineyo ‘Other Charge – OC’ kwa kulipa tofauti ya fedha za mishahara ya Wakufunzi.
Mheshimiwa Spika, Chuo cha Utawala wa Umma kuendelea kutumia fedha za Matumizi Mengineyo kwa ajili hiyo ni kinyume na utaratibu, sambamba na hilo, kunakifanya Chuo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, tunatamka hivyo kwa kuwa Ruzuku inayopatiwa Chuo ni ndogo, ingawa kwa mwaka huu wa fedha imeongezeka lakini Mheshimiwa Waziri katueleza kuwa hadi robo ya tatu ya mwaka Chuo kimepatiwa Tsh. 261,466,301 wakati Baraza la Wawakilishi limekiidhinishia Chuo cha Utawala wa Umma Tsh. 470,000,000/.
Aidha, fedha za Matumizi Mengineyo zinatumika kwa kulipa tofauti ya Wakufunzi na pia, Wanafunzi wa Chuo ambao ni Watumishi wa Umma wanashindwa kulipa ada ya mafunzo. Kwa ujumla mambo yote hayo matatu yanachangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha utendaji mzuri wa Chuo.
KAMISHENI YA UTUMISHI
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu inaipongeza Serikali kwa kuitengea Fungu Kamisheni ya Utumishi kama Sheria inavyoelekeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kamisheni hii ndio chombo cha juu kabisa kwa Tume zote za Utumishi, chenye mamlaka ya kusimamia na kuratibu mambo yote ya utumishi wa umma kwa Zanzibar.
Hivyo, Kamati yetu inaiomba Kamisheni iandae kikao cha pamoja na Tume ya Utumishi ya Idara Maalum ili kuondosha tatizo la kuwakatia fedha zao kiholela Wapiganaji wa Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, Wakuu wa Vikosi hivi wanazikata fedha za Wapiganaji kinyume na Sheria; kwa mfano wanalazimishwa kuingia kwenye SACCOS wakati moja kati ya msingi ya Ushirika unasema kuwa uanachama lazima uwe wa hiari ‘voluntary membership’, sambamba na hilo hulazimishwa kulipia gharama za michezo jambo ambalo linahitaji zaidi utashi wa mtu mwenyewe. Tunapendekeza hili kwa kuwa maslahi yenyewe ni madogo na endapo yataendelea kukatwa kiholela tutawasababishia Wapiganaji wetu kuwa omba omba pamoja na kujiingiza kwenye mambo yasiyokubalika.
Mheshimiwa Spika, Kwa ujumla Kamati imeridhika na Bajeti ya Wizara hii na inaziomba Wizara zote za Serikali kuzisimamia vyema fedha za Posho Maalum, Viburudishaji, Stationary, Mafuta na Vilainisho kwani imebainika kuwa baadhi ya Watumishi wa Umma huzitumia vibaya Kasma hizi.
Mheshimiwa Spika, Aidha, tunaiomba Ofisi ya Rais, Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo kuwa makini wanapoandaa Buku la Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Kazi za Kawaida na Maendeleo kwani kuna baadhi ya Taasisi majina yake yameandikwa kinyume na yanavyotamkwa; kwa mfano, Kamisheni ya Utumishi, Fungu Namba 47, ukurasa wa 673 maneno “Katibu Mkuu wa Kamisheni ya Utumishi” yasomeke “Katibu wa Kamisheni ya Utumishi”.
Mheshimiwa Spika, baada ya maoni hayo ya Kamati, niwaombe sasa Wajumbe wenzetu wa Baraza lako Tukufu, wayakubali na kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Kazi za Kawaida na Maendeleo kwa mwaka 2012/2013, kama tulivyoidhinisha kwenye Kamati yetu, ambapo Ofisi hii imepanga kukusanya jumla ya Tsh. 1,450,000,000 /-.
Aidha, kwa upande wa Matumizi ya Kazi za Kawaida, Ofisi imepanga kutumia jumla ya Tsh. 6,240,484,000/- na kwa upande wa Kazi za Maendeleo, Ofisi imepanga kutumia jumla ya Tsh. 1,408,506,000/.
Mheshimiwa Spika, napenda sasa kuwashukuru Wajumbe wote kwa kunisikiliza kwa makini na utulivu, pia napenda kukushukuru kwa mara nyengine tena wewe binafsi kwa kuniruhusu kutoa maoni ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo napenda kutamka kwa niaba ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala na kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mfenesini ninaunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Aidha, nawaomba tena Wajumbe wote wachangie na kuunga mkono Makadirio ya Bajeti ya Ofisi hii kwa ajili ya utekelezaji bora wa majukumu na malengo waliyojipangia.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Ahsante,
……………………………
Ali Abdalla Ali
Mwenyekiti,
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.
No comments:
Post a Comment