Jumanne, Julai 3, 2012
Kazi ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya inayofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupitia mikutano iliyoanza siku ya Jumatatu, Julai 2, 2012, katika mikoa minane imeanza vizuri.
Mikutano hiyo inayofanyika mara mbili kwa siku, inafanyika katika mikoa yaDodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga. Mikutano hii inatarajiwa kumalizika siku ya Jumatatu, Julai 30, 2012.
Taarifa ambazo Makao Makuu Tume imezikusanya kutoka kwa Wajumbe na Waratibu wanaosimamia mikutano hiyo huko mikoani hadi jana (Jumatatu, Julai 2, 2012) jioni zinaonyesha kuwa mikutano yote 14 iliyopangwa kufanyika siku ya kwanza, yaani jana, Jumatatu, Julai 2, 2012 ilifanyika kama ilivyopangwa na wananchi walijitokeza kwa wingi na kutoa maoni yao kwa amani na utulivu.
Katika mikutano hiyo, wananchi waliwasilisha maoni yao kwa kuongea na kwa maandishi kwa Wajumbe wa Tume walioendesha mikutano hiyo.
Pamoja na kuwapongeza wananchi kwa ushiriki wao, Tume inapenda kusisitiza tena kuwa wananchi wajitokeze katika mikutano inayoendelea na kutoa maoni kwa amani, utulivu na katika hali ya kusikilizana.
Kwa upande wa Dodoma, Tume inaendelea kukusanya maoni katika Wilaya ya Bahi; Katika mkoa wa Kagera Tume inaendelea kukusanya maoni katika wilaya ya Biharamulo; katika mkoa wa Manyara Tume inaendelea kukusanya maoni katika wilaya ya Mbulu wakati katika mkoa wa Pwani Tume inaendelea kukusanya maoni katika wilaya ya Mafia.
Mkoani Shinyanga Tume inaendelea kukusanya maoni katika wilaya ya Kahama; mkoa wa Tanga Tume inaendelea kukusanya maoni katika Wilaya ya Lushoto wakati kwa upande wa Zanzibar, Tume inaendelea kukusanya maoni katika mkoa wa Kusini Unguja katika wilaya ya Kusini.
Pamoja na kuwasilisha maoni kupitia mikutano inayoitishwa na Tume, wananchi pia wanaweza kuwasilisha maoni yao kwa Tume kupitia tovuti ya Tume (www.katiba.go.tz) au barua pepe maoni@katiba.go.tz au kwa njia ya posta kupitia anuani zifuatazo:
i. Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Makao Makuu, Mtaa wa Ohio, S.L.P 1681, DAR ES SALAAM, Simu: +255 22 2133425, Nukushi: +255 22 2133442; Au
ii. Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Ofisi Ndogo, Jengo la Ofisi ya Mfuko wa Barabara, Mtaa wa Kikwajuni Gofu, S.L.P. 2775, Zanzibar, Simu: +255 224 2230768, Nukushi: +255 224 2230769
Mwisho.
Imetolewa na:
Bw. Assaa A. Rashid,
Katibu,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Mtaa wa Ohio,
DAR ES SALAAM
Simu: 022 2133425
Cell: 0757 500 800
0717 084 252
0777 505 508
No comments:
Post a Comment