. Balozi wa
Tanzania nchini Marekani bibi Mwanaidi Maajar akitoa ufafanuzi juu ya maendeleo
mbali mbali ambayo Zanzibar na Marekani zinaweza kushirikiana wakati wa
mazungumzo yake na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif
Hamad huko nyumbani kwake Mbweni Zanzibar. (Picha, Salmin Said OMKR).
Hassan Hamad, OMKR.
Balozi wa Tanzania nchini Marekani bibi Mwanaidi Maajar
amesema Zanzibar inaweza kupiga hatua kubwa katika kukuza sekta ya utalii iwapo
itaimarisha miundombinu ya uwekezaji katika sekta hiyo.
Balozi Maajar ameeleza hayo leo alipokuwa na mazungumzo na
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad huko nyumbani
kwake Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Amesema katika kukuza sekta hiyo ni lazima serikali itenge
fungu maalum litakalokidhi haja ya kuimarisha miundombinu ya utalii, ikiwa ni
pamoja na kuitangaza sekta hiyo katika nchi za nje.
“Ni lazima serikali ikubali kutenga fedha nyingi kwa ajili
ya kuutangaza utalii, sambamba na kuwekeza katika maeneo ambayo yanaweza
kuwavutia watalii”, alifafanua balozi Maajar.
Amesema Zanzibar ina vivutio vingi vya utalii vikiwemo
mashamba ya viungo, na kwamba iwapo vitatumiwa vizuri vinaweza kuwavutia
watalii wengi zaidi na kuinyanyua Zanzibar kiuchumi.
Kuhusu kilimo, balozi Maajar ameishauri serikali kuandaa
program zinazolenga kuendeleza kilimo na kuzituma kwa taasisi zinazojihusisha
na kilimo nchini Marekani, ili ziweze kutoa msukumo katika kilimo hasa cha
umwagiliaji.
Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif
Hamad amesema kwa sasa serikali imeweka mkazo katika kuiendeleza sekta ya
utalii ambayo inatoa mchango mkubwa katika upatikanaji wa fedha za kigeni na
uchumi wa Zanzibar kwa ujumla.
Amesema malengo ya serikali ni kufikia watalii milioni moja
katika kipindi cha miaka kumi ijayo, na kuelezea haja ya kuimarisha miundombinu
na soko la utalii nchini.
Kwa upande mwengine
Maalim Seif amesema serikali inaangalia uwezekano wa kuweza kushirikiana
na jumuiya za kimataifa katika kukabiliana na wimbi la uingizaji wa dawa za
kulevya nchini.
Amesema kuna uwezekano kwamba baadhi ya dawa zinaingizwa
Zanzibar kama njia ya kupitishia dawa hizo kwenda nchi nyengine, lakini baadhi
ya wafanyabiashara wakorofi wamekuwa wakitumia ujanja kuziingiza dawa hizo na
kuwaathiri vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.
Amesifu ushirikiano uliopo mzuri kati ya Zanzibar na
Marekani, na kuishukuru nchi hiyo kutokana na misaada mbali mbali inayoito kwa
Zanzibar ambayo inasaidia kutatua kero
za wananchi na mipango ya maendeleo.
Amesema Marekani imekuwa ikitoa misaada mbali mbali hasa
katika sekta ya elimu, na kuiomba nchi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
mipango yake ya maendeleo na kukuza uchumi.
No comments:
Post a Comment