Habari za Punde

Kesi za udhalilkishaji zaongezeka


Na Mwashamba Juma na Gilbert Massawe AJTC
WIZARA wa Ustawi wa  Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto imesema jumla ya kesi 215 za udhalilishaji watoto kijinsia zilifikishwa wizarani hapo katika kipindi  cha 2012 / 2013.

Kesi hizo zikiwemo za kubaka, kulawiti, kupewa ujauzito, kukashifiwa pamoja na kudhalilishwa kimwili ziliripotiwa sambmba na  kesi 689 za udhalilishaji watoto zilizoripotiwa katika kituo cha mkono kwa mkono pamoja na idadi ya kesi 393 za malalamiko yanayohusu matunzo na kugombania watoto Unguja na Pemba.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Wizara hiyo, Zainab Omar Mohammed katika hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/2013 barazani mwishoni mwa wiki.

Waziri Zainab alisema katika mwaka wa fedha 2012/2013 wizara yake inaendelea kupokea malalamiko ya wanawake na watoto kuhusu udhalilishaji, na unyanyasaji watoto, ambapo kwa mwaka wa 2011/2012 jumla ya malalamiko  132 yalipokelewa wizarani hapo, na kupatiwa ushauri na malekezo yanayofaa katika maeneo ya Unguja na Pemba.


Alifahamisha kuwa baadhi ya malalamiko yaliyopokelewa wizarani hapo ni pamoja na kutelekezwa watoto, kwenye mgawanyo wa mali, mimba nje ya ndoa, kupigwa, shambulio la matusi, kukashifiwa pamoja na shambulio la vitisho.

Aidha alisema wizara yake ilizindua rasmi matokeo ya utafiti wa udhalilishaji watoto (VAC) mwezi  Juni 2011 ambapo wadau kutoka sekta za Afya, Elimu, Polisi, Ustawi wa jamii pamoja na asasi za kiraia walichukuliwa dhamana ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji kupitia taasisi zao.

Akizungumzia suala la utekelezaji sera ya maendeleo ya vijana, Waziri Zainab alisema wizara yake imelenga kuwawezesha vijana kwa kujiimarisha kiuchumi, kiutamaduni na kijamii.

Wakichangia hutuba ya wizara hiyo wajumbe wa baraza la Wawakilishi walisema wizara hiyo licha ya kupiga hatua kimaendeleo lakini inakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na washine ya vya vipimo vya vinasaba vya DNA.

Mwakilishi wa Muyuni, Jaku Hashim Ayoub alisema haoni sababu ya wizara hiyo kushindwa kuwa na mashine hiyo wakati kesi nyingi za udhalilishaji watoto hasa za ubakaji zinashindwa kufikiwa kwa kukosekana kwa mashine hiyo.

Aidha waziri Zainab aliwataka wajumbe wa baraza la wawakilishi kuijadili hutuba yake pamoja na kuwapa ushauri ikiwa ni pamoja na maelekezo ili wapitishe makadirio na kuidhinisha jumla ya shilingi 2,409,000,000 zikiwa ni fedha za kazi za kawaida na ikiwemo  mishahara.

Sambamba na shilingi 1,606,600,000 fedha za kazi za maendeleo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.