Habari za Punde

Spika awakemea Wawakilishi wachelewaji


Na Himid  Choko
 SPIKA wa Baraza la Wawakilishi,  Pandu  Ameir Kificho  amewahimiza Wajumbe wa baraza hilo kufuatilia kwa makini hotuba zanazowasilishwa, sambamba na kukemea  taabia ya baadhi ya wajumbe kuchelewa wakati wa vikao ya baraza hilo.
Alisema hali hiyo inasababisha  wajumbe kukosa umakini wa kusikiliza na kufuatilia hotuba zinazowasilishwa na hivyo, kushindwa kuchangia ipasavyo  wakati wa mijadala ya vikao vya baraza.

Spika Kificho  alikua akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo kwaWajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika hoteli ya Coconut Tree Village Marumbi, Mkoa wa  Kusini Unguja.

“Kuna mtindo unaojitokeza wakati Waziri anaanza kuwasilisha hoja yake , ukumbi unakuwa mtupu,  sasa njoo ikiwa hakuna yule aliyesikiliza kwa makini,inapelekea  hoja hiyo kukosa wachangiaji  hasa mwanzoni wa mjadala wa hoja,” alisema.

Alisema ni vyema wajumbe wakawepo  muda wote wakati wa uwasilishaji wa hotuba ndani ya baraza hilo , kwani kuwepo kwao kunasaidia kuwajengea uelewa mpana zaidi  wa hoja inayowasilishwa.

Kuhusu jinsia, Spika Kificho amesema akinamama ni kundi muhimu katika jamii hivyo mipango imara inahitajika wakati wa kupanga bajeti ya serikali.

Alieleza kutoridhika kwake na baadhi ya waajiri  hasa makampuni binafsi ambao wamekuwa wakiwanyanyasa wanawake katika ajira kutokana na maumbile yao.

Alisema maumbile ya akinamama yasitumike kama ni kigezo cha kuwakosesha ajira badala yake  waajiri kwa wingi ili kulisaidia kundi hilo ambalo ndilo mara nyingi walezi wa familia  katika jamii.

Wakitoa mada kuhusiana na stadi za mawasiliano, Wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Cha Zanzibar (SUZA)  Said Khamis Juma na Haroun Maalim walisema tatizo kubwa linalowakabili wachangiaji ni  kupambanunua kati ya ukweli  na dhana  kwa kushindwa kuthibitisha hoja zao  kwa kutumia taarifa halisi.

“Hata ukweli unaweza kukosa nguvu , unaweza usikubalike pale panapokosekana  hoja au taarifa za kuunga mkono , badala yake watu wakahisi kuwa ni fikra ama mawazo ya mtu tu,” alisema Haroun.

Hivyo Mhadhiri huyo aliwahimiza Wawakilishi hao  kujenga hoja zao kwa kutumia takwimu, mifano na nukuu  wakati wa mijadala kwa lengo la kuvuta ushawishi  nakuaminika  kwa hoja zao.

Nae ndugu Said Khamis Juma amewahimiza Wawakilishi hao kuzingatia uteuzi wa maneno, kujiamini na kudhibiti jazba  hasa wakati wa vikao vya baraza.

Wakiwasilisha mada inayohusu  jinsia na masuala ya bajeti, wanaharakati wa jinsia, Asha Aboud na Munira Hamoud wamesema ni muhimu kwa Wawakilishi kuibua hoja za masuala ya jinsia katika sekta muhimu kwani zitasaidia wakati wa uaandaaji wa mipango na ugawanaji wa rasilimali ziliopo katika kila sekta.

Walisema mapengo ya jinsia yanapoonekana katika kufanya upembuzi yakinifu inasaidia pia kutambua  mahitaji ya wanawake na wanaume pamoja na makundi mengine  katika sekta mbai mbali.

Mapema akitoa maelezo  kuhusiana na mafunzo hayo, Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad alisema afisi ya Baraza la Wawakilishi itaendelea na juhudi za kuwajenge uwezo Wajumbe wa baraza hilo ili waweze kutekeleza vyema majukumu yao waliyokabidhiwa na wananchi.
Mafunzo hayo ni mfululizo mafunzo yanayoandaliwa na afisi ya Baraza la Wawakilishi kwa lengo la kuwajengea uwezo wajumbe wake chini ya ufadhili wa shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)  katika mradi wake wa kusaidia mabunge LSP.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.