Habari za Punde

Kutoka Baraza la Wawakilishi.


Na Ramadhan Makame

ZECO Yaagizwa Kuzifungia Tukuza Taasisi za Serikali

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee amelitaka shirika la umeme Zanzibar (ZECO), kuzifungua mita za tukuza taasisi zote za serikali.

Alisema chini ya utaratibu huo, ambao utaliwezesha shirika hilo kupata fedha za kwa wakati na kuepuka kukopwa, ni likaeupuka kufunga mita hizo kwenye taasisi nyeti na zenye umuhimu mkubwa ikiwemo hospitali.

Waziri huyo alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa kijibu suali lililoulizwa na Mwakilishi wa nafasi za Wanawake Salma Mussa Bilal.


Alisema kufungwa kwa mita hizo kutalifanya shirika hilo kutopata hasara inayotokana na kutolipwa huduma za utoaji wa umeme kwa  taasisi za serikali.

Katika suali lake la msingi Mwakilishi huyo alitaka kujua mikakati ya iliyopo kwa taasisi za serikali kulipa madeni ya shirika la umeme kutokana na huduma ya nishati hiyo inavyotumiwa katika taasisi hizo.

Alisema wizara pamoja na taasisi zote za serikali zinapaswa kufahamu kwamba sheria ya fedha za umma ya mwaka 2005 inasisitiza wizara na taasisi za serikali kutotumia huduma ya aina yeyote ile kwa njia ya mkopo.

Alisema wizara na taasisi za serikali zinapaswa kutumia huduma kutokana na mpango kazi wa mwaka husika na kulipia huduma inazozipata kutoka kwa taasisi nyengine ikiwemo umeme.

Alisema wizara fedha itahakikisha inazipatia fedha taasisi za serikali kwa mujibu wa mpango kazi ili ziweze kukidhidhi na manunuzi ya huduma ikiwemo ya umeme.

Hisa za Zanzibar BoT hazieleweki
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee amesema kuwa moja ya kero ya Muungano ambayo haijapatiwa ufumbuzi ni usahihi wa hisa za Zanzibar kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Waziri huyo alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi alikuwa akijibu suali la nyongeza lililoulizwa na Mwakilishiwa jimbo wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu.

Katika suali lake Mwakilishi huyo pamoja na mambo mengine alikataka kujua usahihi wa hisa za Zanzibar katika uanzishwaji wa benki hiyo.

Waziri huyo alifahamisha kuwa kero ya kutambuliwa kwa usahihi wa hisa za Zanzibar katika uanzishwaji wa BoT, bado haijapatiwa ufumbuzi na majadala wa mazungumzo ya kero hiyo yanaendelea.

Katika hatua nyengine waziri huyo alisema kuwa muundo wa kiuongozi katika benki hiyo hauna sura ya kimuungano.

Alisema mbali ya uongozi wa juu wa benki hiyo kuwa unateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, lakini pia nafasi za chini na za utendaji hazina sura ya kimuungano.

 
Matemwe Kupatiwa Maji Safi, Salama

WIZARA ya Ardhi Makaazi Maji na Nishati, imesema kuwa wananchi wa Matemwe wako mbioni kumaliziwa kero inayowakabili ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Naibu waziri wa wizara hiyo, Mwadini Haji Makame alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa kijibu suali la Mwakilishi wa Nafasi za Wanawake, Kazija Khamis Kona.

Katika suali lake Mwakilishi huyo alitaka kujua mipango iliyopo ambayo itahakikisha wananchi wa Matemwe wanapatiwa ufumbuzi dhidi ya tatizo la maji safi na salama.

Naibu huyo alisema tatizo la maji katika eneo hilo litamalizika kutokana na Mamlaka ya Maji (ZAWA), kuchimba kisima kipya ambacho kipo katika hatua za mwisho za kumalizika na kutoa huduma.

Alisema kisima hicho kiko kwenye hatua za mwisho ikiwemo kufungwa pampu hali ambayo kwa kiasi kikubwa itamaliza tatizo la maji katika eneo hilo.

Naibu huyo alifahamisha kuwa suluhisho la kudumu la matatizo ya maji kwa wananchi wa Matemwe litamalizika kabisa baada ya mradi huyo unaofadhiliwa na AFDB kukamilika.

Alisema mbali ya Matemwe maradi huo utahudumia vijiji vyengine vinne.


Barabara Mjini Kiuyu – Pengewani Hufanyiwa Matengenezo

NAIBU waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Ussi amesema barabara ya Mjini Kiuyu – Pengewani imekuwa ikifanyiwa matengenezo kila mwaka.

Naibu huyo alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa akijibu suali la Mwakilishi wa Nafasi za Wanawake, Viwe Khamis Abdalla.

Katika suali lake la msingi, Mwakilishi huyo alitaka kujua mpango ulipo wa ujenzi wa barabara hiyo ili kuwaondoshea kero ya usafiri wananchi wa Mjini Kiuyu.

Naibu huyo alisema katika mwaka wa fedha uliomalizika wizara iliweka kalvati mbili, ikiwa ni hatua ya kuiwezesha barabara hiyo kupitika.

Aidha alisema kiasi cha shilingi milioni 4,106,000 zimetengwa kwa ajili ya kuifanyia matengenenzo barabara hiyo hasa kwenye sehemu korofi.

Naibu huyo alifahamisha kuwa serikali itaifanyia matengenezo ya mara kwa mara barabara hiyo ili iweze kutumiwa vyema na wananchi wa Mjini Kiuyu.




No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.