Habari za Punde

Mafungu Yaliyonona Yawapa hofu Wawakilishi

Pesa za Semina, Tv,m Jokofu , Balaa 

Wamtaka Waziri atoe ufafanuzi wa kina 

Na Mwantanga Ame

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wamemueleza waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala bora, Haji Omar Kheir kujiandaa kuwapa majibu ya kina na yenye kuwatosheleza ili waweze kumuidhinishia matumizi ya fedha za bajeti alizoomba. 

 Wajumbe hao walieleza hayo walipokuwa wakichangia bajeti ya wizara hiyo, ambapo wameonesha wasi wasi juu ya fedha zilizoombwa kwenye vifungu vya baadhi ya wizara. 

 Wajumbe hao walisema kuna mafungu ya matumizi katika Idara za wizara hiyo yanahitaji maelezo ya kina kwani yameombewa fedha nyingi ikilinganishwa na hicho kinachoombewa fedha kutaka kununuliwa. 

Wakitoa mfano walisema matumizi televisheni, mafriji posho za semina, mikutano, makongamano na vinywaji yamevimba ikilinganishwa na kazi za maendeleo. 


Wajumbe hao walieleza juu ya kupatwa na hofu hiyo, baada ya kuona mafungu ya Idara yameombewa fedha nyingi zilizoongezeka asilimia kubwa ikilinganshwa na mwaka uliopita. 

Mwakilishi wa Nafasi za Wanawake, Mgeni Hassan Juma, alisema alisema ameingiwa na hofu juu ya matumizi ya vinywaji, semina na mikutano kwani yameombewa fedha nyingi ikilinganishwa na mwaka jana. 

Akitoa mfano alisema fungu la semina katika Idara Tume Utumishi, zimeombwa shilingi milioni 98,400,000 ambapo kiuchambuzi inaonesha kila semina watatumia shilingi milioni 5,000,000. Alisema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa, ikilinganishwa na hali halisi ya mahitaji ya nchi ukiwemo ya ukosefu wa vikalio kwa wanafunzi wa skuli za Zanzibar na haipendezi kuona fedha hizo zinatumiwa kwa njia hiyo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, alisema hatakuwa tayari kuipitisha bajeti hiyo hadi pale atapopewa majibu maridhawa kutokana na baadhi ya mafungu ya bajeti hiyo kuvimba. 

Alisema ameshitushwa na fungu la matumizi ya ukodishwaji kumbi za mikutano katika Idara ya Utawala na Raslimali Watu ambao wizara hiyo imeomba shilingi milioni 186,872 kutoka shilingi milioni 1,000,000 za mwaka uliopita. 

Akichambua bajeti hiyo alisema ndani ya bajeti hiyo, kuna mafungu ambayo yameongezeka kwa kiasi kikubwa yakiwemo ya ununuzi wa televisheni, ambazo zimetengewa shilingi milioni 28, 000,000 ndani ya Idara ya Nyaraka. 

 Alisema Ofisi Kuu Pemba Wizara hiyo imepanga matumizi kwa ajili ya kompyuta ambapo zimeombewa shilingi milioni 30, 000,000 kutoka shilingi milioni 9,650,000 na Mradi wa E-goverement ukiwa na shilingi milioni 33 wakati mwaka jana mradi huo ukiwa bado haujaanza ulitengewa fedha kidogo. 

Mwakilishi huyo pia alihoji juu ya fungu linalohusu ununuzi wa jokofu ambao umetengwa zaidi ya shilingi 662.5 milioni huku fedha za safari za nje zikiwa zimetengwa shilingi 95 milioni na kuhoji ni kwanini eneo hilo liwe na kiasi hicho cha fedha wakati kimsingi kazi zao ni za ndani ya nchi zaidi. 

Matumizi mengine ambayo aliyataja Mwakilishi huyo kuonesha kuwa yanamtia hofu ni yale yanayohusu matengenezo ya vifaa ambayo yamefikia shilingi milioni 9.4 huku friji katika Idara ya Utawala Bora, imewekewa shilingi milioni 10. 

Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Mkwajuni Mbarouk Wadi Mtando, alisema kwa wizara hiyo kuifanyiakazi ripoti ya kamati teule kwani imewagusa moja moja baadhi ya watendaji. 

 Nae Mwakilishi wa Mkoani, Abdalla Mohammed Ali aliitaka wizara hiyo kucha kuajiri wastaafu ili kuwapa nafasi vijana kupata ajira hizo hoja ambayo pia ilipendekezwa na Mwakilishi wa jimbo la Chake Chake, Omar Ali Sheh.

2 comments:

  1. Ndugu mwandishi,

    Kwa heshima kabisa naomba uangalie sana unapoandika tarakimu (nambari) hasa zinazohusu fedha katika hii blog yetu. Kwa mfano umeandika "....ununuzi wa televisheni, ambazo zimetengewa shilingi milioni 28, 000,000 ndani ya Idara ya Nyaraka". Nadhani kiusahihi ulitakiwa uandike milioni 28, au useme 28,000,000 bila ya neno milioni. Hio uliyoandika hapo juu ina maanisha "milioni 28 milioni" kiswahili ambacho siyo sahihi. Na kosa hilo umelirejea mara nyingi kwenye habari hii na habari nyengine zilizopita.

    Naamini mchango huu utasaidia kuboresha blog yetu tuipendayo.

    ReplyDelete
  2. Bajeti za namna hii ni changa la macho, Zanzibar bado tuna safari ndefu hadi kuweza kupata viongozi waadilifu ambao wanajali maslahi ya wananchi. Kimsingi sura ya bajeti hii inalenga ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma ambao kwa kiasi kikubwa unaathiri maisha ya mwananchi wa kawaida. Viongozi wetu chonde chonde kuweni na huruma japo kidogo huku mkitambua hio ni dhima ambayo siku moja itaanguka juu ya mogongo yenu.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.