Na Mwantanga Ame
MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mwanamwema Shein, amewataka wazee kushiriki kutunza amani ya nchi, ili kuiwezesha serikali kuweza kutekeleza vyema ilani ya Chama cha Mapinduzi juu kuwapatia matunzo bora wazee katika makaazi yao.
Mama Mwanamwema aliyasema hayo jana wakati akikabidhi msaada wa vyakula na nguo kwa ajili ya Wazee wa vituo vya Welezo na Sebleni ikiwa ni kwa ajili ya kujikimu katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Akitoa nasaha zake kwa niaba ya Mama Shein, Mama Asha Suleiman Idd, alisema suala la amani ndani ya nchi ni moja ya jambo msingi ambalo litaiwezesha serikali kupata utulivu na kuweza kuihudumia jamii wakiwemo wazee.
Alisema nia ya serikali kupitia sera yake ya Ilani ya uchaguzi ni kuona inakuza huduma za jamii kwa wananchi wake wakiwemo wazee, lakini inaweza kuwa ndoto kufanikisha hilo ikiwa nchi itakosa kuwa na amani.
Kutokana na hali hiyo Mama Shein alisema ni vyema kwa wazee kuona wanatumia nafasi yao kuiombea nchi ibakie katika amani ili iweze kuwapatia huduma bora.
Alisema serikali ya Zanzibar hivi sasa imetangaza dhamira ya kuwapatia huduma bora wazee katika nyumba za Wazee ya Sebleni kwa kuwapatia milo mitatu kwa siku jambo ambalo litawawezesha wazee hao kuwa katika hali nzuri ya maisha yao.
Alisema maisha bora kwa Wazee ni moja ya jambo la msingi kwani wengi ya wanajamii wanategemea kupata maarifa mapya na ulezi kutoka kwao na haitakuwa busara kuanza kuwadharau ama kutowapa huduma ili waweze kuishi maisha bora.
Mama Mwanamwema alisema kwa kuthamini wazee serikali na Umoja wa Wake wa viongozi utaendelea kuona unawapatia misaada mbali mbali wazee wa nyumba hizo ili waweze kuwa na maisha mazuri.
Alisema hatua hiyo serikali itaiendeleza kwa kuulinda msingi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya1964, ikiwa ni sera iliyorithiwa na Chama cha Mapinduzi.
Mama Shein, aliwapatia wazee hao vya vyakula vya nafaka ukiwemo mchele, unga, sukari, tende na vifaa vya usafi zikiwemo sabuni za kufulia na kuogea pamoja na nguo zikiwemo kanga kwa wanawake na seruni na fulana kwa wanaume ambapo thamani yake ni shilingi milioni 2,000,000.
Mapema Mkuu wa Utawala katika kituo cha Welezo, Sister Gemma Rodrigues, akizungumza na gazeti hili alisema hali ya matunzo ya Wazee katika vituo vyao bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali likiwemo suala la kuwa na bajeti ndogo.
Alisema hivi sasa bajeti wanayoingiziwa ni shilingi milioni 3,000,000 kwa mwezi kiasi ambacho ni kidogo kwa vile kiwango hicho kimewekwa kwa muda mrefu na hakikuangalia upandaji wa gharama za uendeshaji wa maisha kwa hivi sasa.
Alisema ili kuweza kumudu sehemu ya maisha ya Wazee hao ingelihitajika kituo hicho kupatiwa wastani wa shilingi milioni 4,000,000 kwa mwezi kwa vile hivi sasa wamekuwa wakitumia shilingi 90,000 kwa ajili ya kununulia maji ambayo hutumia siku mbili jambo ambalo huwapa ugumu kuwapa huduma nyengine wazee hao.
Kutokana na hali hiyo Sister Gemma, ameiomba serikali kuona namna ya kuweza kuwapunguzia matatizo yaliomo ndani ya kituo hicho, ili kuweza kuwapa nguvu wafanyakai wanaojitolea kuwatunza wazee hao.
Katika makabidhiano hayo Mama Shein alifuatana na wake wa viongozi kutoka katika majimbo mbali mbali ya Zanzibar akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mjini Abdalla Mwinyi Khamis ambaye aliwataka wazee hao kuendelea kushirikiana na serikali yao kwa vile bado itaendeleza msingi wa Mzee Karume wa kuwahudumia.
No comments:
Post a Comment