Habari za Punde

Maoni Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari



MAONI YA KAMATI YA MIFUGO, UTALII, UWEZESHAJI NA HABARI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA KAZI, UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI NA USHIRIKA KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
Mheshimiwa Spika,
Napenda kuchukuwa fursa hii adhimu, kutanguliza shukrani zangu za  dhati kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa kutujaalia kukutana hapa katika Baraza letu, tukiwa katika hali ya uzima na afya njema, kwa lengo la kuwatumikia wananchi wetu na Taifa kwa ujumla. Aidha, napenda nikushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika, kwa kunipa fursa ya kusimama mbele ya Baraza hili, ili kutoa maoni ya Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari kuhusu Bajeti ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika kwa mwaka wa fedha 2012/2013.

Mheshimiwa Spika,
Kwa niaba ya Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari, natumia fursa hii kumpongeza sana Mhe. Marina Joel Thomas kwa kuteuliwa kwake kuwa mjumbe wa Bazara hili, uteuzi ambao umekamilisha jumla ya nafasi kumi za uteuzi wa Rais. Ni imani yetu kuwa Mhe. Rais amefanya maamuzi ya busara sana hadi kufikia uamuzi wake wa kumteuwa Mhe. Marina. Ingawa ni nafasi ya kumalizia lakini tunaamini kuwa nafasi hii ni “ the last but not the least”.
Mheshimiwa Spika,
Naomba kutumia fursa hii kuwatunukia taji la shukrani waheshimiwa Wajumbe wa Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari inayoongozwa na Nahodha shupavu Mhe. Asha Bakari Makame. Uongozi wake unathibitisha ile kauli isemayo “mama nambari wani wala hana mpinzani”. Naomba uniruhusu Mheshimiwa Spika kuwataja kwa majina Wajumbe hawa mmoja baada ya mwengine kama ifuatavyo:
1.     Mhe. Asha Bakari Makame              -        Mwenyekiti
2.     Mhe. Mohammed Said Mohamed     -        M/ Mwenyekiti
3.     Mhe. Assaa Othman Hamad             -        Mjumbe
4.     Mhe. Ali Mzee Ali                                      -        Mjumbe
5.     Mhe. Salim Abdalla Hamad              -        Mjumbe
6.     Mhe. Abdi Mosi Kombo                            -        Mjumbe
7.     Mhe. Viwe Khamis Abdalla              -        Mjumbe
8.     Mhe. Kazija Khamis Kona                -        Mjumbe
9.     Ndg. Haji Khatib Haji                       -        Katibu
10.                        Ndg. Asma Ali Kassim                     -        Katibu
Mheshimiwa Spika,
Tunaipongeza sana Wizara  kwa kutekeleza jukumu lake la msingi la kuvikagua na kuvisimamia vyama vya ushirika nchini, ili kuvipatia mwongozo unaostahiki kwa nia ya kuvikuza na kuviendeleza zaidi.
Aidha, Kamati imepokea kwa huzuni taarifa ya kwamba kati ya vyama 5,503 vilivyosajiliwa nchini, ni vyama 1,651 tu ndivyo vilivyo hai ambavyo ni sawa na asilimia 30%. Ili kuwa na vyama vya Ushirika vilivyo imara zaidi, Wizara haina budi kuchukuwa hatua za dharura za kuwasiliana na vyama visivyo hai kwa nia ya kuyajua matatizo yanayowakabili na kuangalia uwezekano wa kuvifufua upya, na ikishindikana basi kuwe na utaratibu wa kuvifuta.
Halikadhalika, ni vyema kuwa na utaratibu wa usajili wa vyama vya ushirika utakaowaweka karibu zaidi wanaushirika na Idara ya usajili kwani hali ya sasa ya usajili ni mbaya na Kamati imebaini kuwa urasimu katika mpangilio wa kufanya usajili ndiyo kikwazo kikuu cha wanaushirika kutojisajili.

Mheshimiwa Spika,
Kamati yetu inatoa wito kwa Wizara kupitia Idara ya Ushirika kutafuta wafadhili wengine ili kupata fedha za kutekeleza miradi ya vyama sita vya ushirika ambapo kwa mwaka wa fedha 2011/2012, ni mradi mmoja tu wenye thamani ya shilingi 7,450,000/= ndio pekee ulioweza kutekelezwa.
Aidha, Wizara isimamie vyema mwenendo mzima wa SACCOS Banks zilizoanza kufanya kazi ili kuhakikisha kwamba zinatekeleza majukumu yao ipasavyo na hatimaye kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika,
Katika kutafuta suluhisho la tatizo la ukosefu wa ajira nchini, tunaipongeza Wizara kwa kufanikiwa kupata fursa za ajira kwa vijana wetu nchini Oman. Aidha, vijana 20 wa Zanzibar wanatarajiwa kupatiwa mafunzo nchini humo ili kujiweka tayari kuuzika kwenye soko la ajira. Kamati inashauri kuwa taarifa zitolewe kwa vijana wote kwa uwazi kabisa ili waweze kujitokeza kuitumia fursa hii kwani imebainika kuwa vijana wengi huishia mitaani tu bila ya kufahamu fursa zinazotolewa na Serikali yao pamoja na taasisi binafsi. Aidha, wakati utakapofika wa kuanza mpango huu vijana wapewe nafasi hizo kwa kuzingatia sifa zao “academic qualifications” ili kujiepusha na kupeleka vijana wasio na sifa zinazostahiki, jambo ambalo linaweza kupelekea kufutwa kwa nafasi hizi kwenye miaka michache ijayo na hiyo itakuwa ni hasara kubwa kwa Taifa hili.
Mheshimiwa Spika,
Ni ukweli usiopingika kwamba waajiriwa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wale wa sekta binafsi nchini wanakabiliwa na mazingira magumu ya kiutendaji kutokana na kutokuwepo kwa vifaa vya kinga na usalama katika maeneo yao ya kazi. Sambamba na hilo, Kamati imegundua kwamba mafunzo ya jinsi ya kuvitumia vifaa vya kinga yanahitajika kwa watendaji wa taasisi hizo ili kuwajengea uwezo wa kujinusuru wakati wa dharura.


Mheshimiwa Spika,
Tunatoa shukrani za dhati kwa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Hadi kufikia tarehe 30 Juni 2012, jumla ya shilingi Milioni mia moja na ishirini na tatu, laki mbili sabini na sita elfu, mia tisa na sabini na tano (123,276,975/=) zimekusanywa, ambazo ni sawa na asilimia 180 ya makadirio. Ni matumaini yetu kwamba, Wizara itaendeleza jitihada hizi za kukusanya mapato vizuri kwa mwaka huu wa fedha ili kufanya matumizi mazuri kwa mwaka unaofuata kwa nia ya kujenga Taifa.
Mheshimiwa Spika,
    Kamati inatoa pongezi maalum kwa Wizara kwa kutekeleza programu ya Kazi nje nje katika mwaka wa fedha 2011/2012.  Kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO), Wizara imeanza kutekeleza Programu hiyo kuanzia mwezi wa Machi 2011 na inalenga kuwawezesha vijana kuwa na muamko wa kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea kuajiriwa kwani hali ya upatikanaji wa ajira nchini inazidi kuwa ngumu. Katika awamu ya kwanza programu hiyo imetoa mafunzo ya wiki mbili kwa vijana 32 juu ya ujasiriamali na kubadili tabia kwa lengo la kujiajiri.
Mheshimiwa Spika,
Kuwepo kwa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ni muhimu sana katika kupima utekelezaji wa mipango ya Wizara. Kamati yetu inaipongeza sana Wizara kwa kuuona umuhimu huo na kuandaa mfumo wa tathmini ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi wa Agosti 2012. Ni dhahiri kuwa kupatikana kwa kipimo cha mafanikio ya miradi mbalimbali kutawafanya watendaji wawe imara zaidi ili kuhakikisha wanafikia kiwango kikubwa pindi watakapotathminiwa na hivyo kusukuma mbele gurudumu la maendeleo nchini.

Mheshimiwa Spika,
Ili kupata dira ya kutuelekeza kwenye utatuzi wa masuala ya kiuchumi, Wizara imefanya tafiti katika maeneo muhimu ya kiuchumi ili kubaini fursa zilizopo na mahitaji halisi ya kuwawezesha wananchi kiuchumi. Kamati inatoa pongezi za dhati kwa hatua hii na inashauri matokeo ya tafiti hizi yafanyiwe kazi kikamilifu, katika mwaka huu wa fedha 2012/2013 ili tupate tija kwa maslahi ya Taifa.
Mheshimiwa Spika,
  Kamati imefarajika sana na mpango wa program ya kuifanya sekta isiyo rasmi ya usafiri wa umma kuwa bora na endelevu ili   kuwawezesha vijana walioajiriwa katika sekta hiyo kuwa na ajira za uhakika zenye mikataba inayoendana na Sheria za Kazi. Hii ni hatua muhimu ambayo itawasaidia vijana wetu kufaidika na jasho lao wenyewe, badala ya kuwatajirisha waajiri wao pekee kama mfumo wa sasa ulivyojengeka. Aidha, mazingira mazuri ya kazi yatatusaidia kujenga tabia ya uaminifu baina ya waajiri na waajiriwa na hivyo kuzidi kudumisha amani, utulivu na umoja wetu.
Mheshimiwa Spika,
Hatua iliyofikiwa na Wizara kuwaunganisha wamiliki wa mahoteli na wazalishaji wadogo wadogo pamoja na wajasiri amali inatoa mwelekeo wa kuanza kulipatia ufumbuzi tatizo la ukosefu wa soko la bidhaa za wajasiri amali nchini kwa mwaka huu wa fedha wa 2012/2013. Katika zoezi hili, jumla ya hoteli kumi na moja zimetembelewa na Wizara na kufanya mazungumzo na uongozi kuhusu umuhimu wa kutumia bidhaa za ndani badala ya kuagiza bidhaa zinazoweza kuzalishwa nchini.
Kamati inatoa wito kwa Wizara kuuendeleza mpango huu mzuri waliouanzisha na kuufanyia utaratibu mwafaka ili wajasiri amali wengi zaidi waweze kufaidika na soko hilo.

Mheshimiwa Spika,
Pamoja na kuendelea na harakati za utowaji wa mikopo nchini, Kamati inasisitiza kwamba, Wizara itowe mikopo ambayo itawawezesha kikweli wananchi kiuchumi.
Tunamaanisha kuwa mikopo hiyo iwe ya kiwango kinachostahiki kwa mujibu wa mradi unaokusudiwa kutekelezwa, isiwe na riba kubwa, na miradi inayotekelezwa iwe imeibuliwa kitaalamu na kuhakikishwa kuwa italipa baada ya muda fulani.
Aidha, Kamati yetu imefarajika sana na mpango wa Serikali wa kuanzisha Benki ya Wanawake nchini. Hatua hii ni muhimu katika kuleta ukombozi wa mwanamke kutoka katika hali ya utegemezi na kufanya shughuli ndogo ndogo za kiuchumi hadi kufikia kuwa wamiliki wa biashara kubwa kubwa zenye kutoa fursa za ajira kwa wengine. Ni dhahiri kuwa hii ni nyota njema inayohitaji kuendelezwa kwa maslahi ya wananchi wa Taifa hili.
Mheshimiwa Spika,
Ili kutimiza malengo ya Wizara kwa mwaka huu wa fedha, nawaomba waheshimiwa Wajumbe waichangie, waijadili na hatimaye waipitishe bajeti ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika kwa mwaka wa fedha 2012/2013, ambayo ni jumla ya shilingi za Kitanzania 2,679,000,000/=.
Mheshimiwa Spika,
Mwisho kabisa, natoa shukurani zangu za dhati kwako wewe binafsi, pamoja na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwa utulivu na usikivu wao, tunamuomba Mola mtukufu awape nguvu na hekima katika kuliongoza Taifa hili kwa umakini na uadilifu mkubwa.
Kwa niaba ya Kamati yangu, na wananchi wangu wa jimbo la Mtambwe naunga mkono bajeti hii ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika kwa mwaka wa fedha 2012/2013 na naomba kuwasilisha.



Ahsante,


.................................
Mhe. Salim Abdalla Hamad,
Kny: Mwenyekiti,
Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.