Habari za Punde

Masheha Watwishwa Lawama Utoaji Vitambulisho


Na Husna Mohammed
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wamechoshwa na tabia ya baadhi ya masheha kuweka vizingiti katika kuidhinisha utoaji wa vitambulisho vya Mzanzibari (ZAN ID), ambapo wamedai kuwa vimekuwa vikitolewa kwa naizi na kumuangalia mtu anakotoka.

Wajumbe hao walitoa kilio hicho jana katika hicho jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi uliopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar walipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Wajumbe hao walisema masheha wanawaekea vizingiti wananchi katika kupewa haki yao ya vitambulisho vya Mzanzibari, jambo ambalo linawakosesha haki zao mbali mbali za msingi.

Akichangia hotuba hiyo Mwakilishi wa jimbo la Wawi (CUF), Saleh Nassor Juma, masheha hawapaswi kuvitoa vitambulisho hivyo kwa naizi na kwa kujuana kwani kunawanyima haki wananchi ya kuvipata.

Alisema hivi sasa vitambulisho hivyo vimekuwa vikitumika katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuombea kazi, usafiri, masomo na mambo mengineyo muhimu.

Alisisitiza kuwa vitambulisho hivyo vitolewe kwa Wazanzibari wazaliwa na wasipewe watu wasiohuika kwani si haki yao.

Aidha Mwakilishi pia aliishutumu Idara ya Vitambulisho kuwa nao inachangia hali hiyo huku akimtishwa lawama Mkurugenzi na kueleza kuwa haafai.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Nafasi za Wanawake, Farida Amour Mohammed, alisema masheha wamekuwa ni kikwazo kikubwa katika kuwapitia wananchi vitambulisho hivyo.

“Masheha wengi wamekuwa wakiwakwamisha wananchi kupata vitambulisho vya mzanzibari wakaazi kwa njia moja au nyengine jambo ambalo limekuwa likiwavunjia mstakabali mzima wa maisha yao,” alisema.

Mwakilishi huyo alisema kuwa vitambulisho hivyo ni nusu ya maisha ya watu wa Zanzibar kwa kuwa vimekuwa vikitumika kwa shughuli mbalimbali za kitaifa.

“Masheha bado ni vikwazo katika kuwapa haki ya kupata vitambulisho wazanzibari wakaazi jambo ambalo ni kumuharibia mtu maisha yake ipo haja ya Serikali kutueleza hapa ni kwa nini masheha wanafanya hivyo”, alihoji.

Aidha Mwakilishi huyo aliiomba serikali kuwafikiria madiwani, kwa kuwa nao ni watu muhimu katika mchango wa maendeleo ya Zanzibar.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni, Jaku Hashim Ayoub, alihoji juu ya matumizi ya fedha zinazochangishwa na Baraza la Manispaa kuwa zinatumika vipi huku ikizingatiwa kuwa mji wa Zanzibar imekuwa mchafu.

“Mazingira ya soko nje na ndani ni mbaya sana jambo ambalo limekuwa likitoa hofu hata kwa wananchi na wageni wanaotembelea katika mji huo”, alisema.

Nae Nassor Salim Ali, Mwakilishi wa Jimbo la Rahaleo, akichangia bajeti hiyo, alisema ipo haja ya Baraza la Manispaa kutathmini hali ya kuweka mji katika mazingira safi kwa lengo la kuwavutia zaidi watalii.

Alisema mji wa Zanzibar ni kivutio na haiba kubwa kwa wageni na watalii wanaotembelea mji huo.

“Mji huu ni kitovu cha utalii na mkoa mama kwa shughuli mbalimbali, hivyo kuweko hali ya uchafu kunaweza kuharibu mambo mengi ya kimaendeleo,” alisema.

Kwa upande wake Mwakilishi wa jimbo la Micheweni Subeit Khamis Faki alitaka kujua wafungwa katika vyuo vya mafunzo bangi wanaipata wapi na kueleza kuwa inavutwa kwa wingi.

“Kule vyuo vya mafunzo kunavutwa bangi sana, wafungwa naipata wapi bangi, wanaipata kwa kuuziwa na askari kwa sababu mnawapa mishahara midogo”,alisema Mwakilishi huyo.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.