Habari za Punde

Mbelgiji Yanga aanza kwa kichapo. Atletico 'vibonde' waiduwaza Yanga, APR yapiga saba. Leo ni mnyama Simba, URA na Ports, Vita Club.

DAR ES SALAAM
TIMU ya Atletico ya Burundi ambayo vyombo vya habari vya Tanzania vimeibatiza jina la kibonde, jana ilionesha soka safi na kuilaza Yanga mabao 2-0 katika mchezo wa Kombe la Kagame uliopigwa wakati wa saa kumi jioni kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika siku ya kwanza ya mashindano hayo ya klabu za nchi za Afrika Mashariki na Kati, Atletico walitumia mbinu za kuibana Yanga kwa muda mwingi na kuwanyima fursa washambuliaji wake mahiri kulitia kashikashi lango lao.

Kipindi chote cha kwanza na nusu saa ya ngwe ya pili, timu hizo zilishambuliana kwa zamu na kumiliki mpira kwa asilimia zinazolingana.

Licha ya kosakosa nyingi za kufunga magoli, miamba hiyo ilikwenda mapumziko wakiwa hawajafungana,

Mnamo dakika ya 62, kocha mpya Tom Saintfiet wa Yanga aliyekuja kutoka Ubelgiji, alimtoa nje Jerry Tegete ambaye kwa siku ya jana hakuwa katika kiwango kizuri, na kuingia Said Bahanuzi ambaye ni mchezaji mpya katika kikosi cha Yanga, lakini mabadiliko hayo hayakuweza kuzaa matunda yoyote.

Jahazi la Yanga lilianza kuzama mnamo dakika ya 80, pale safu yake ya ulinzi ilipokatika na kumruhusu mchezaji Didier Kavumbagu kuandika bao la kwanza.

Bao hilo lilitosha kuwatia majonzi mashabiki wa Yanga na kocha wao mpya, kwani wakati mchezo ukielekea ukingoni, hakukuwa na dalili yoyote kama wachezaji wao wangeweza angalau kuambulia sare.

Huku mashabiki wakianza kutoka uwanjani, Kavumbagu tena alizichana tena katika dakika ya mwisho kati ya nne zilizoongezwa na mwamuzi, na kuwafanya Atletico waliopondwa na vyombo mbalimbali vya habari kwamba ni vibonde watoke kifua mbele kwa ushindi huo muhimu.

Na katika mechi iliyotangulia saa nane mchana ya kundi hilo, APR ya Rwanda iliifanyia mauaji ya kimbari Wau El Salaam kwa mabao 7-0.

Michuano hiyo inaenedelea tena leo kwa mchezo wa kwanza saa nane kati ya Ports ya Djibouti na Vita Club ya DRC, ambapo mnyama Simba ataivaa URA ya Uganda wakati wa saa kumi jioni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.