Na Salum Vuai, Maelezo
KUTOKANA na timu ya soka ya Jamhuri kuoneshwa kadi nne za njano kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Hwangwe ya Zimbabwe, Shirikisho la mchezo huo barani Afrika (CAF) limeitwanga timu hiyo faini ya dola 5000 za Kimarekani (shilingi milioni nane).
Mechi hiyo ya marudiano ilichezwa Machi 4, mwaka huu jijini Harare, ambapo wawakilishi hao wa Zanzibar, walichapwa mabao 4-0 na hivyo kutolewa kwenye michuano hiyo kwa jumla ya magoli 7-0 kufuatia kushindwa nyumbani kwa mabao 3-0.
Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Zanzibar Kassim Haji Salum, amekiri kupokea barua kutoka CAF iliyoandikwa Mei 31, mwaka huu, na tayari wameiwasilisha kwa uongozi wa Jamhuri kwa hatua zaidi.
Alipoulizwa sababu ya kuchelewa kuipeleka kwa uongozi wa Jamhuri mapema, Katibu huyo alidai kuwa hata ZFA imeipata Jumatano ya Julai 13.
Amefahamisha kuwa, kwa mujibu wa kanuni mpya za CAF, timu inayopata zaidi ya kadi tatu za njano kwenye mchezo mmoja wa mashindano ya shirikisho hilo huhesabika haina nidhamu na hutozwa kiasi hicho cha fedha ambacho hutakiwa kilipwe si zaidi ya miezi miwili, vyenginvyo hupandisha na kuwa mara mbili zaidi.
Meneja wa Jamhuri Abdallah Abeid 'Elisha', alisema licha ya klabu yake kuipokea barua hiyo, bado inailaumu ZFA ikiamini kuwa iliipokea mapema kutoka CAF na pia kutoieleza timu hiyo awali juu ya kanuni za shirikisho hilo ili iweze kujiandaa vyema, hasa ikizingatiwa kuwa ni ngeni kwenye michuano ya CAF.
Elisha alisema faini hiyo inatakiwa ilipwe si zaidi ya Julai 31, lakini kwa sasa klabu yake haina uwezo huo, na tayari wamewasilisha ombi kwa kamati iliyokuwa imeundwa kuzisaidia klabu za Jamhuri na Mafunzo katika ushiriki wao wa michuano ya klabu barani Afrika (KUMIZA), kutaka iangalie uwezekano wa kuinusuru timu hiyo.
"Ni jambo la kusikitisha kwamba barua imeandikwa tangu tarehe tano Mei lakini sisi tumeipata juzi, na hali zetu mnazijua, tuombe Mungu atusaidie", alieleza Elisha kwa majonzi.
No comments:
Post a Comment